Tuesday, June 9, 2009

Tukithamini kila "kidogo" tufanyacho, tutafanikiwa.

Mmoja wa waelimishaji wetu wakubwa Prof. Mbele aliwahi kuandika kuhusu KUWATHAMINI WALIMU WA ELIMU YA AWALI (Bofya hapa kujikumbusha). Sijui watu walilionaje hili, lakini kwangu lilikuwa na maana, ukweli na pia mantiki ndani yake. Kuna haja ya kuthamini kila tuonacho kuwa ni "kidogo" maana ndio asili ya hayo mengi. Luciano aliwahi imba kuwa "the journey of thousands miles begin with just one step" na akaendelea kuelimisha kuwa kuna kila haja ya kuithamini hata hatua ya kwanza kwani kwa kufanya hivyo tutaweza fanikiwa kuifikia ya pili na kuzikusanya mpaka tamati ya safari yetu.
Kutothamini kile kionekanacho kuwa kidogo (ambalo ndio chimbuko ya hayo makubwa tuyaonayo) ni tatizo mojawapo linalotufanya tushindwe kuendelea tukithamini zaidi makubwa na kupuuza mwanzo wa mengi. Kuna mifano mingi kuonesha ukweli wa thamani ya hata vile vionekanavyo vidogo ambavyo kwa hakika vikiendelea kuthaminiwa na kukusanywa vinaleta maendeleo. Mfano mmojawapo ni ule wa kuamini kuwa matajiri wengi ni wabahili na hawatoi hata visenti vidogo kirahisi. Ukweli ni kuwa wamekuwa na pesa nyingi kwa kukusanya visenti hivyo hivyo na kwa kuvigawa ukividharau unaweza kukuta hautimizi hata shilingi maana ni mkusanyiko wa visenti hivyo ukuundiao shilingi kamili.
Kuna ndugu zangu ambao wakimaliza vyuo vya (hiyo wanayoiita) elimu ya juu wanakosa ajira waitakayo, na kisha wanaamua kukaa na kutumia pesa walizonazo kujikimu kimaisha badala ya kuanzisha miradi "midogo" ambayo sio tu itawafanya wawe katika mzunguko wa kusaka pesa na kazi, lakini pia inaweza kuwakutanisha na wenye mawazo na mipango mizuri ya kazi na miradi na kukutana na mwanzo wa mafanikio yao huko. Wanajikosesha "maendeleo" kwa kuwa tu wanaamini katika kile waitacho kutofanya "biashara ndogo".
Upande wa Serikali nao ndio balaa. Umeamua kuyafumbia macho mazingira wayaonayo kuwa ni "madogo" na kusahau kabisa kuwa ndiko lililo chimbuko la hayo makubwa wayathaminiyo (japo hawaonekani kuyatenda).
Serikali haiwezi kupinga ukweli kuwa HAIWATHAMINI WAALIMU ambao wana mchango mkubwa wa kuwafanya hao waendelezao dharau hizo kuwa hapo walipo.
Haionekani kuwajali wale wanaoendesha maisha yao kwa kilimo kidogokidogo huko vijijini na kung'ang'ania kujenga na kuboresha mijini bila kujua kuwa wanawavuta wasio na ajira mijini ambako wanashindwa hata kujiajiri kihalali na kuishia kwenye ajira potofu kama wizi.
Serikali haiwathamini askari wa vyeo vya chini na maisha hasa makazi yao ni tofauti na wito ama dhamana waliyopewa. Sina shaka kuwa ni kati ya mambo ambayo kwa ujinga kabisa yanachangia rushwa kwao.
Serikali haiwapi kipaumbele wafanyabiashara ndogondogo ambao badala ya kutengenezewa na kutayarishiwa mazingira (na hapa namaanisha masoko na mifumo ya uuzaji na ununuzi) ya kuwawezesha kusonga, inawatumia ma"Askari-njaa" wa jiji ambao wanawapora wafanyabiashara hawa na mbaya zaidi hawaonekani kuwasikilisha waporavyo kwenye sehemu husika.
Hakuna malengo mema kwa watoto ambao wanaonekana kuwa ni taifa la leo (japo wanalazimishwa kuwa taifa la kesho isiyofika) na mbaya zaidi SERIKALI HAIONEKANI KUWEKA MKAKATI MZURI WA KUWAJALI WENYE UHITAJI MAALUM ambao maisha yao yanazidi kuwa magumu kila iitwayo leo na hata wale walelewao kwenye vituo maalum hawajengewei msingi wa maisha baada ya kufikisha umri wa kuondoka vituoni humo na matokeo yake ni kuwa wakifikisha umri wa kuondoka, hawana mbinu na msaada wa kupambana na maisha na wanaishia kujiingiza kwenye "msako-haramu wa pesa" unaojumuisha matendo mabovu na ya kuhatarisha maisha yao.
Serikali haitakiwi kugharamika kufanya yote haya, bali inatakiwa kuonesha njia na kuonesha nia na imani kwa wananchi kuwa inaweza kuweka mikakati ama kuratibu maoni ya wenye nia njema (badala ya kulinda wenye kuwanyonya wananchi) ili wananchi waweze kujitutumua kuendeleza kile ambacho kitakuwa na faida kwao.
Hakuna kilicho kidogo kama kinawekwa na kutumika kwa kadri ya uwezo wake, bali mtazamo wa kukidogosha ndio ufanyao kionekane kuwa ni kidogo. Lakini kwa mtazamo huohuo, CHANGAMOTO YETU ni kuvithamini vyote viitwavyo vidogo ili kuweza kufanikiwa.
Blessings