Wednesday, July 1, 2009

Wasanii wetu wanajipoteza katika harakati za kujitafuta

Adolph Mbinga, Sister V (Much Respect to you Sis) Mimi na Rogert Hegga baada ya mahojiano 100.5 Times Fm 2002
Labda tafsiri ya mafanikio ndio kizingiti cha kuwepo kwa makubaliano ya nani anafanya nini ili kiwe nini.
Yaani wakati fulani mtu anafanya afanyalo na kuonekana anazidi kujipoteza, lakini kwa mtazamo wake, kile atendacho na mahala alipo ama anapoelekea vyaweza kuwa tafsiri njema ya mafanikio.
Kwa muziki wa nyumbani Tanzania tumeshuhudia HAMAHAMA za wasanii ambazo zinawafanya kuwika katika wiki ama miezi ya mwanzo ya bendi zao mpya wakiwa na nyimbo mpya (ambazo mara nyingi ni vijembe vya walikotoka) na kisha wakikaa muda mchache wanafifia. Na hakuna ambaye ameendelea kuhamahama na kuendelea kukua kimuziki. Asilimia kubwa ya wasanii hawa (kwa namna nionavyo mimi) wanazidi kujipoteza katika kutafuta ilipo sehemu yao.
Lakini pia mbali na kuhama bendi, wasanii hawa wanajipoteza wanapokimbia kueleza ukweli wa maisha ama visa vilivyo katika jamii na kuendekeza majungu na kuimbana ambapo baada ya muda nyimbo zao huwa hazina mvuto kwa kuwa (pengine) kisa kilichoimbwa hakivuti hisia za watu.
Hakuna ubishi kuwa kuhamahama kwa wasanii kama Mwinjuma Muumini, Ali Choki, Banza Stone, Hussein Jumbe, Waziri Sonyo, Mhina Panduka, Amina Ngaluma, Badi Bakule na wengine niliowasahau waliokuwa wakitamba miaka kadhaa iliyopita kumewashushia uwezo kwa kuwa kila waendapo wanakutana na umiliki mpya, uongozi mpya, mazingira na masharti mapya na kazi mpya.
Pengine wakitulia na kutuliza vichwa kutunga yahusuyo jamii zaidi kutakuwa na manufaa kwa jamii husika badala ya kuendeleza mabishano na majungu ambayo "yanaua" uwezo wao kikazi.
Mfano halisi ni wasanii kama Mwinjuma Muumini "Kocha wa Dunia" aliyetamba na vibao kama Mgumba I & II, Kilio cha Yatima, Maisha Kitendawili, ama Rogert Hegga "Katapila" aliyetunga Fadhila kwa Wazazi I & II, ama Adolph Mbinga na hata Banzastone ambao baadhi ya vibao vyao vilizungumzia maisha halisi ya jamii (hata kama uandishi wao ulitokana na matukio yaliyowakumba wao) na tukashuhudia wakiijingiza kwenye vijembe na mabishano yanayowapa umaarufu wa wiki kadhaa kisha wanapotea. Hakuna ubishi kuwa kati ya nyota wote niliowataja hapo, hakuna anayetamba tena baada ya kubadili mtazamo wa tungo zao na kufuata washabiki badala ya WITO wao kwa jamii. Wanasahau lililosemwa na Cyril Connolly aliyesema "Better to write for yourself and have no public, than to write for the public and have no self."
Sikiliza nyimbo hizi FADHILA KWA WAZAZI toka kwao Mchinga Sound na MGUMBA II toka kwa Double M Sound uone ubunifu na uadilifu uliotumika katika tungo upangiliaji wa ala za muziki na viitikio, vitu ambavyo sasa vimepotea licha ya washiriki karibu wote katika nyimbo hizi kuendelea na muziki.
Ni mtazamo tu katika muziki

1 comment:

Masangu Matondo Nzuzullima said...

Tunafahamu ni kwa nini wasanii hawa wanahamahama sana? Pengine tusiwalaumu kabla ya kujua sababu hasa inayowafanya wafanye hivyo. Kuhusu kuimba nyimbo za maseng'enyo badala ya zile za kuelimisha jamii nafikiri kwamba, kama bendera, wanafuata upepo unakoelekea kwa wakati ule. Ni lazima pia tukiri kwamba majungu, umbea, vijembe na udaku vinapendwa zaidi (tazama hata katika magazeti, taarabu, kanga n.k) na pengine wanafanya hivyo wakidhani kuwa watajipatia umaarufu zaidi, japo wa bandia na wa muda mfupi tu. Kama kawaida mada nzuri na ya kufikirisha Mzee wa Changamoto!