Wednesday, July 29, 2009

MSAADA

Nimeona OMBI HILI LA MSAADA kwenye
Blogu ya Kaka Maduhu nami nimeona niungane naye kusaidia kufikisha ujumbe huu.
Habari yote ni kutoka blog ya Maduhu kama alivyoiandika.


Sala Abdallah Matewa akiwa kitandani eneo la Mtawala Manispaa ya Morogoro wakati akiongea na blog BLOG YA MTANGAZAJI juu ya kuomba msaada kwa wasamalia wema ili kuweza kupatiwa matibabu
Fatuma Abdallah Matewa akiwa amenyanyua mguu wa mdogo wake Sala Abdallah Matewa(19)wakati akiwaonyesha jinsi ulivyoharibika na kuomba msaada kwa wasamalia wema wa kutibiwa.

BINTI Sala Abdallah, Matewa (pichani) mkazi wa eneo la Mtawala katika Manispaa ya Morogoro anaomba msaada wa kitabibu ili kuweza kupatiwa huduma ya kukatwa miguu yake yote miwili baada ya kupata ulemavu wa miguu hivyo kulala kitandani kwa miaka nane bila kufanya shughuli yoyote za uzalishaji mali na kukosa kupata elimu ya msingi.
Akizungumza na blog hii nyumbani kwao Mtawala mjini hapa wakati akijielezea juu ya historia yake ya kupatwa na ulemavu huo, Sala Matewa, alisema huku akiwa amekaa kitandani kuwa kabla ya kupatwa na hali hiyo hakuwa na ulemavu wa aina hiyo bali aliupata mara baada ya kuvunjika mguu wake wa kushoto mwaka 2002 na kupelekwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro ambapo alitibiwa na kufungwa P.O.P na baada ya kupatiwa matibabu aliruhusiwa na kurudishwa nyumbani kujiuguza.
Sala alisema baada ya kupata matibabu hayo siku ya tatu mguu huo ulivimba sana na kwamba kutokana na hali hiyo ililazimika kurudishwa tena hospitali ya Rufaa ya mkoa huo na kulazwa katika wadi namba tatu ili ufanyiwe uchunguzi zaidi kuweza kupaini tatizo linalomsibu.
“nikiwa nimelazwa katika wadi hiyo kwa miezi mitano nilipatwa na mshangao kwa sababu nyama za mguu wangu zilianza kulika kidogo kidogo huku mifupa na mishipa ya mguu wangu huo ukianza kuonekana kama vile nimechunwa ngozi ” alisema Sala.
Aidha alisema kuwa hali ambayo iliwashangaza sana madaktari ambao walikuwa wakinitibu hospitalini hapo hata hivyo hakuweza kuwakumbuka majina yao na kwamba walilazimika kumpeleka katika chumba cha upasuaji a na walimchuna ngozi ya mguu huo kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili kuweza kubaini chanzo cha tatizo hilo jipya la kulika kwa ngozi na nyama za mguu.
Pia Sara alisema pamoja na jitihada zote hizo za madaktari wa Hospitali hiyo ya mkoa wa Morogoro za kumpima vipimo vyote na kumfanyia uchunguzi wa kina juu ya tatizo lake lakini tatizo bado halikugundulika na hali ya mguu wake ukizidi kuwa mbaya madaktari walilazimika kushauriana na baba yake mzazi Mzee Abdalah Matewe ili mgonjwa wake arudishwe nyumbani.
Alisema baada ya kurududishwa nyumbani,alijaribu kutumia Tiba za asili ambazo hata hivyo, hazikufanikiwa, badala yake mguu mwingine wa kulia, ulivimba, baadaye ulipasuka na kumsababishia vidonda vikubwa na kwamba,tangu hali hiyo itokee, ni kipindi cha miaka Nane sasa, yuko kitandani, hajawahi kutembea wala kutoka nje kwa vile, hawezi kutembea tena kutokana na miguu yake yote miwili kupatwa na ulemavu wa kudumu.
Ukiangalia miguu yangu ilivyo panda pinda na kukonda naona kama miguu hii imekuwa ni mzigo na kero kubwa kwangu kwa vile haiwezi kurudi tena katika hali ya kawaida imeisha na imeharibika na imekufa kabisa ni heri ikatwe ili niondokane na mzigo huu kwa majonzi na katika hali ya kukata tamaa huku akionyesha miguu yake hiyo. Alisema Binti huyu.
Kutokana na uzito wa tatizo hilo dada yake mkubwa, Fatuma Matewa, akizungumzia juu ya hali ya mdogo wake alisema familia yao imekaa na kufikia maamuzi ya kuwaomba wasamalia wema ikiwemo serikali na wadau wengine kumpatia msaada wowote utakao muwezesha kupelekwa kwa wataalamu wa viungo vya binadamu ili kungalia uwezekano wa kumsaidia ndugu yao kupatiwa msaada huo wa matibabu na kama itashindikana ni heri akatwe miguu yake yote miwili na kuepukana na tatizo hilo linalomkabili kwa muda mrefu sasa.
Aidha Fatuma Matewa amewaomba viongozi wa serikali, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa kidini na mtu yeyote atakayeguswa kuswa na tatizo hilo kumtembelea mahali anapoishi mtaa wa Mtawala ili kuangalia hali halisi ya uzito wa tatizo lake na mazingira anayoishi.Pia waweza kutoa mchango wa mawazo,mapendekezo ama mali kwa ajili ya kumsaidia
Waweza kuwasiliana na blog ya Mtangazaji (Ya Kaka Maduhu) kwa email ya maduhu@gmail.com ama kwa simu namba +255 713 309 314

Asante sana kwa kujali

1 comment:

Fadhy Mtanga said...

Nami naongeza kuomba watu tumsaidie binadamu mwenzetu.