Niliwahi kuandika kuwa hata kama hukubaliani na mtu ama watu ama kundi fulani, haimaanishi kuwa hakuna lolote unaloweza kujifunza toka kwao.
Nilimaanisha kuwa kama mtu ni mchoyo, anaweza kukufunza kujipenda kisha ukaweka KIASI katika kujipenda huko kwa kuwa MCHOYO HUJIPENDA KULIKO KIASI. Na hili laweza kuwa katika nyanja zote ikiwa ni pamoja na siasa.
Nimekuwa nikiwaza mara kwa mara juu ya sababu ya kuwa tulivyo hasa kwa siasa tulizonazo. Nahisi tatizo kubwa kwetu ni kwa kuwa tunachagua watu ambao tunawapa dhamana ya kutuongoza kwa miaka mitano na kisha tunasahau. Kwa bahati mbaya, hakuna mwaka ama muhula ambao Rais ametoka katika chama ambacho kina wabunge wengi.
Mara nyingi nyakati hizi ndizo ambazo hupima uwezo wa Rais na Bunge na kuonesha makali halisi katika kusimamia na kutekeleza ILANI za uchaguzi.
Tumeona ambavyo wingi wa wabunge walio upande mmoja na Rais usivyo na manufaa kwa nchi yetu na naamini ni wakati ambao tunaweza kuiga siasa za wenzetu ambazo zimeonesha kuleta manufaa kiasi. Kama kuna mwenye shida na kuiga siasa za nje, nikumbushe tu kuwa hata hizi tulizonazo, tusizozimudu na zisizoonesha tija kwa wananchi wetu ni za kuiga na kama kuna linaloweza kuleta maendeleo hakuna ubaya wa kulifuata.
Nchini Marekani kuna utaratibu ambao "wabunge" wao wanachaguliwa katikati ya muhula wa Rais na kinakuwa kipimo tosha kujua kama rais anahitaji wabunge wa aina gani kuipeleka nchi inakotakiwa kwenda. Katika uchaguzi huu wauitao mid-term election, wananchi huangalia msimamo wa wawakilishi wao na kuangalia wanavyosimamia maslahi yao kulingana na sera za serikali na hapo huwachagua ama kuwaweka kando ili kuendeleza ukamilisho wa mahitaji yao.
Naamini hili ni moja kati ya yanayohitajika nyumbani Tanzania. Kwa sasa tunaona miaka minne ya Rais Kikwete ikielekea kumalizika na hatuna hakika na utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi wa 2005.
Labda ukamilishaji ama utekelezaji huo unazuiwa na baadhi ya wabunge ambao wanapinga baadhi ya mambo, ama unazoroteshwa na baadhi ya wabunge ambao wakishaingia madarakani wanajipa miaka kama mitatu ya "kula shushu" kabla ya "kufufuka" mwaka wa nne na "kuzibuka" ule wa tano tayari kututimulia vumbi (wakidai wanatengeneza barabara), kuweka oda za khanga, vitenge na vi-Tshirt tayari kuwapumbaza wananchi kuwachagua tena.
Kwa kuwa na uchaguzi wa nusu muhula, wananchi wataweza kuangalia kama Rais anahitaji wabunge wa kutosha kumsaidia kuendeleza maendeleo kwa wananchi wake, ama kama anahitaji wabunge wenye kuona uozo wake na kwenda kumwamsha katika usingizi wa kutotekeleza aliyoahidi.
Gharama za kutenganisha chaguzi haziwezi kuwa kubwa kuliko gharama za kutotekeleza lolote lililoahidiwa na wabunge kwa wananchi na pia kutoshughulikia mambo mengi ambayo yanaweza kuwawezesha wananchi kujishughulisha na mambo ambayo yanaweza kuwasaidia wananchi kujiendeshea maisha yao bila kutegemea msaada wa serikali.
Wananchi wanateseka na kupoteza maisha na hata matumaini kwa kuwa watu wenye dhamana ya kushirikiana nao kunyoosha njia zao za mafanikio, wanatumia nafasi hiyo kujinufaisha na kwa hakika yahitajika namna ya kuwaamsha hawa WATAWALA.
Na ndio maana nasema NIONAVYO MIMI... UCHAGUZI WA RAIS NA WABUNGE UTENGANISHWE
Uchaguzi Tanzania ni "label" inayozungumzia namna niionavyo nchi yangu ya Tanzania ijiandaavyo na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010. Kwa maandishi mengine juu ya mada hii katika "label" hii BOFYA HAPA
5 comments:
Ahsante sana kaka.
Umeongea mengi tena kweli tupu. Sitaki kuharibu utamu wake. Naunga mkono hoja yako kwa asilimia mia.
Ila la kutimuliwa vumbia umenikata maini. Jana nimepita eneo moja katika wilaya ya Kisarawe. Kuna barabara muhimu sana waliyoahidiwa kwenye kampeni ya 2005 lakini haikujengwa. Mwezi uliopita ndo tingatinga limeanza kuuza sura.
Ni hayo tu!
Yote mmeshasema nami nakubaliana nanyi.
mimi simo, nasema tena; SIMO!!!
Mara nyingi visingizio huwa ni oooh gharama kubwa, lakin hawajui maendeleo huletwa kwa kutumia gharama. Naunga kwa mikono na miguu kama inawezekana
Ndugu yangu hapo umesema ukweli kwa sababu kuna mambo huwa yanafanyika katika chaguzi hizo ninaogopa hata kukusimulia.
Ki ukweli ni kwamba raisi angechaguliwa kivyake kama usemavyo na waheshimiwa wengine wangechuka ustaarabu wao mwingine ili tuepukane na haya ya aibu yanayotokea kwenye kadamnasi.
Post a Comment