Thursday, October 29, 2009

Tanzania yangu .....Na DHIHAKA ya kuenzi Oktoba 14

Kiongozi wa mbio za mwenge 2009 Ndg Kheir Ahmada Mwamalo akiukabidhi mwenge wa Uhuru kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika kilele cha mbio hizo kilichofanyika Butiama mkoani Mara Oktoba 14, 2009.
Rais Kikwete na Mama Slama wakizungumza na Mama Maria Nyerere huko Butiama
Picha zote na Freddy Maro wa Ikulu
 Hakuna anayeweza kuzungumzia UHURU wa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara (kwa usahihi) akasahau juhudi za nchi yangu ya Tanzania katika ukombozi huo. Na pengine isingewezekana kama Tanzania yenyewe isingekuwa huru. Na kuzungumzia Uhuru wa Tanzania bila kumzungumzia Baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere hutakuwa hujakamilisha mazungumzo hayo. Na kama kuna kubwa alilofanya Mwalimu Nyerere basdi ni KUTUUNGANISHA waTanzania kwa namna mbalimbali na kutufanya kuwa na nia na kauli moja kwa mbinu mbalimbali mojawapo ikiwa ni MBIO ZA MWENGE.
Mbio za mwenge zilitufanya waTanzania kuamini kuwa tuna nia moja. Ya kuutumia kama "kimulikio" kutuonesha nini chaendelea wapi na ni nani aliye tofauti na sisi katika UMOJA WA KITAIFA. Tuliambiwa kuwa mwenge ulitakiwa umulike mpaka nje ya mipaka yetu. Ulete TUMAINI pale ambapo hakuna matumaini. UPENDO mahali ambapo pana chuki na HESHIMA ambapo pamejaa dharau.
Watu walikesha wakifanya kazi kwa pamoja ili mwenge ujapo uzindue na wakati huo TULIJIVUNIA UMOJA WETU.
Na katika KUENZI HARAKATI, MAANA NA NIA nzima ya mwenge, uongozi wa nchi ukaamua kubadili siku ya hitimisho hilo kuwa Oktoba 14 katika kuunganisha na siku ya kukumbuka kifo cha Mwl Nyerere. Mwalimu naye alikuwa na yake mema aliyotenda na kusema. Sina haja ya kuyarejea hapa bali ntaelekea kwenye Oktoba 14 zetu.
Nikiiangalia Tanzania yangu na kuangalia SIASA ziendeshwazo nchini na kuweka mkabala na kauli mbiu ya mwenge na mipango na falsafa za Mwalimu Nyerere, naona kama NI DHIHAKA
Ni dhihaka kwa nchi inayonuka UFISADI na RUSHWA na UONGOZI M'BOVU na UMASKINI USIOSTAHILI kuendelea kuenzi siku hiyo tena bila aibu.
Hivi kuna mwenye tumaini kwa waTanzania wa kipato cha chini?
Kuna upendo gani ikiwa wachache wenye madaraka wanaendelea KUWANYONYA wengi wasionacho?
Ni heshima gani tunayozungumzia iwapo watu wanaendelea kuiba na kujilimbikizia mamilioni na hawawajibiki?
NI DHIHAKA
Ni dhihaka kumkumbuka Mwl Nyerere na nchi ambayo inazungumza u-Dini kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Ni dhihaka kumkumbuka Mwl Nyerere na nchi ambayo inazungumza Umoja na kuwekeza katika utengano
Ni dhihaka kumkumbuka Mwl Nyerere tukiwa na nchi ambayo viongozi wake wanaweza kusema bayana kuwa anayemshutumu kiongozi yeyote kwa ufisadi atashughulikiwa
Ni dhihaka kumkumbuka Mwl Nyerere tukiwa na nchi ambayo wapo wanaoishi maisha ya dhiki kuliko ilivyowahi kutokea na licha ya malighafi na uwekezaji unaotendeka, hakuna mwananchi wa chini anayenufaika.
Nahisi MWANGA WA MWENGE WA UHURU unamulika nje ya mipaka na kuwaonesha wajanja mahala pa kuja kuiba kwa kisingizoo cha uwekezaji.
Nahisi MWANGA WA MWENGE WA UHURU unawapa MAFISADI NA VIONGOZI WANAOISABABISHIA SERIKALI NA NCHI HASARA matumaini ya kutokamatwa, kutoshitakiwa na hata kuwajibishwa.
Kwa ujumla sioni lolote linalotendeka nchini linaloendana na KAULI MBIU ASILIA ya Mwenge wa Uhuru na hata falsafa za Mwl Nyerere na ndio maana naamini kuwa NI DHIHAKA KUMUENZI MWALIMU Nyerere kwa namna tumuenzivyo na kumuongezea mzigo wa maumivu wa maumivu tunapoweka hitimisho la mwenge siku hiyo ilhali tunatenda tofauti nao.
Najiuliza huko aliko anateseka namna gani kuona namna ambavyo anaenziwa namna ambavyo hakuwahi kuishi??? Mzee NDIMARA TEGAMBWAGE amesema bayana kuwa hataki kumkumbuka mwalimu Nyerere kwa njia isiyofanana na matendo na fikra zake alipokuwa kiongozi wa nchi (bofya hapa kumsoma). Hata Kaka Matondo alizungumza namna ambavyo jumbe za Mwl zinaendelea kuwasuta rohoni wakizisikia ama kuziona na kuanza kuwatisha wenye kuzirejea na kuziweka hewani kuwa hawana hakimiliki yazo (soma hapa) nami nasema kama hatubadili namna tunavyoenzi OKTOBA 14, basi HAKUNA HAJA YA KUIENZI KWANI NI DHIHAKA KUENZI MWENGE WA UHURU NA FIKRA ZA MWALIMU NYERERE KWA NAMNA TUFANYAVYO.
Hebu fikiria kama Mwl akifufuka leo akosikia kipande cha hotuba yake (anzia dk ya 2:49) kwenye wimbo huu na kwa namna nchi ilivyo, angejisikiaje???

Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA
Tuonane "Next Ijayo"

2 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima said...

Umenena; na tuko pamoja katika hili. Ninashangaa kwamba mambo hayaendi vyema na badala ya kumtumia Mwalimu kuwakumbusha Watanzania misingi hasa ya taifa letu; na athari za udini na ukabila ambao sasa unafukuta chini kwa chini, badala yake tumekazania kukatazana hata kusikiliza hotuba zake. Kama alivyohoji Mwalimu - udini na ukabila utatusaidia nini hasa sisi kama Watanzania? Acha pia tucheze na haya matabaka tunayoyalea - matajiri wa kupindukia wachache sana na wengi hohehahe kabisa wasio na cho chote. Ipo siku (kutumia msemo wa Mwalimu) - msingi wa nyumba hii nzuri iitwayo Tanzania "utatikisika". Sijui utakuwa ni mtikisiko wa aina gani.

Inabidi viongozi wetu wafumbue macho, waone nchi inakoelekea na kuchukua hatua. Vinginevyo - kama titanic - tumekaa tukihubiri amani na upendo na kumbe mbele yetu jilima kubwa la "iceberg" ya mfarakano wa kitabaka, udini na ukabila lipo linatujia.

Fadhy Mtanga said...

Hakika ulinena vema