Wednesday, December 2, 2009

Blogu ni shule. Wafunzao ndio wafunzwao

Wengi wanadhani unapoandika huwa unafunza watu, lakini kwangu naandika kushiriki nijuayo ili nijifunze mengi zaidi. Nawashukuru wanandugu wanaochangia hapa kila siku na wale ambao hupitia hapa kujifunza kama nijifunzavyo mimi.
Nimejifunza meeengi sana tangu nilipoanza ku-blog na leo napenda kukiri kuwa nimejifunza mengi saaana katika maoni kuhusu mada HII HAPA ILIYOTANGULIA. Napenda kuwashirikisha nyote katika maoni niliyoyapata leo ambapo kwa hakika NIMEJIFUNZA MENGI.
Hasa UKWELI alioueleza Prof Mbele kwa ufupi na usahihi sana.
ASANTENI WASOMAJI WOOTE WA CHANGAMOTO YETU BLOG.
Kwangu mimi, BLOGU NI SHULE KWANI SISI TUANDIKAO KUFUNZA, TWAJIFUNZA PIA.
Na haya ni maoni ya wadau.

Fadhy Mtanga said...
Hii ndiyo Tanzania yetu... Kuna wakati huwa najiuliza kama viongozi wetu huwa wanafikiri kwa makini wanapofanya maamuzi yahusuyo mstakabali wa taifa letu. Na mbaya zaidi, kadri siku zinavyokwenda ndipo nionapo vipaumbele vinawekwa katika mambo yasiyobadili hali za maisha.
Ni kazi kwelkweli!

Wednesday, 02 December, 2009


Kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...
siasa zetu hizi. sasa wanakuwa vituko mbele ya vijana wa kizazi kipya wasiojua maana ya uhuru wasiojua umuhimu wa uhuru na sasa wanajiona utumwani kuliko ule wa zamani

Wednesday, 02 December, 2009


Chib said...
Mimi nasema... nashukuru kwa kunikumbusha ya kuwa siku ya uhuru wa Tz imekaribia. Nafikiri uzalendo umeanza kuniponyoka kwa sababu ya madudu mengi...

Wednesday, 02 December, 2009


Kissima said...
Tafsiri halisi ya uhuru ule wa mwaka 1961 si tafsiri ya uhuru unaokumbukwa leo . Kwa hali ya watanzania wachache kumiliki uchumi na njia za uchumi, hali ya ufisadi, rushwa zilizokithiri,mikataba mibovu ya madini na waliodai kutuacha huru,mikataba isiyokuwa na tija kwa wananchi na kwa taifa na mambo mengine mengi. Watanzania wachache wanatunyang'anya uhuru wetu kwa maslahi yao. Hatuko huru, twatawaliwa na wazawa(watanzania wachache wazawa), hivyo twalazimika tena kuingia vitani(vile vile bila kumwaga damu) ili hatimaye siku moja tujitangazie ushindi ulio na ukombo wa kweli dhidi ya wazawa wachache wanaotunyonya na kutukandamiza ki-manpower na ki-akili. Leo hii raisi akiulizwa kama malengo ya watanzania kuupigania uhuru na hatimaye kuupata na malengo hayo yametimizwa kwa kiasi gani, sijui kama ataweza kutoa majibu mazuri, kwani kadiri siku zinavyokwenda linabaki swala la "ni bora ya jana kuliko ya leo" japokuwa hata ya jana yalionekana kuwa mabaya kuliko yale ya juzi.Sikatai, kuna mazuri yaliyokwisha fanyika lakini kwa njenzo za uchumi tulizo nazo pamoja na UHURU WA MWAKA 1961 hatukutakiwa kuwa hapa tulipo hata kidogo.

Wednesday, 02 December, 2009

Prof Mbele said...

Mzee wa Changamoto

Tatizo ni jamii ya waTanzania. Wanapenda sherehe na makamuzi. Angalia takwimu ya ununuaji wa bia, utaona kuwa watu pesa iko sana mifukoni. Kila kona kuna baa, na baa zinazidi kuongezeka.

Hata katika vimiji vidogo, utaona baa zimejengwa kwa ubora sana, wakati shule hapo pembeni ni ya makuti na haina madawati. Watoto wanakaa sakafuni, au wanakalia mawe.

Watanzania hapo kwenye kamji utawakuta wanalamba ulabu bila wasi wasi, wakati shule ni ya makuti.

Watanzania hapo kwenye mji utawakuta wanajumuika kupanga sherehe za arusi ambazo ni za nguvu na gharama kubwa. Misafara ya arusi inapita hapo kwenye kashule ka makuti, na hakuna anayewazia kupunguza sherehe ili kukarabati shule.

Serikali ya Tanzania ikithubutu kusema baa zifungwe wiki nzima, ili watu wafanye kazi, serikali hiyo itaangushwa vibaya kwenye uchaguzi ujao. Watanzania wanataka starehe na makamuzi.

Ni kweli, wako ambao ni maskini, hawana hela. Lakini akili yao sio tofauti na ya wale wanaotanua na kukamua. Hao maskini nao ndoto yao ni siku moja kuwa watanuaji na wakamuaji.

Sasa katika kutekeleza hii ndoto, unaona watu wanafanya kila namna kujitafutia utajiri, hata kwa kuwachuna ngozi wengine.

Hatuna maadili kama yale aliyoongelea Mwalimu Nyerere, ya kujali utu kwanza, na kutoabudu mali. Nyerere alikemea mambo ya ulimbwende na matanuzi, tangu mara tulipopata Uhuru.

Leo, kuanzia viongozi hadi walalahoi, ndoto yao ni kukamua au kupata fursa ya kukamua.

Wednesday, 02 December, 2009

2 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Bado tunaruhusiwa kuchangia kuhusu michango hii ya wachangiaji?

Kama jibu ni ndiyo - mimi napenda kubainisha zaidi uangavu wa maneno ya Prof. Mbele kwani yamegusa kwa ufasaha kabisa tatizo letu mojawapo la msingi.

Kama tungeweza kuielewa - japo kwa asilimia 1 tu falsafa ya Kujitegemea ambayo Mwalimu Nyerere alikuwa anajaribu sana kuipandikiza mioyoni mwetu leo tungekuwa mbali sana. Kama alivyosema Prof. Mbele ndoto ya kila mtu ni "kuionja pepo" hapa hapa duniani potelea mbali hata kama ni kwa kuuza viungo vya zeruzeru. Baadhi ya harusi hapo Dar es salaam zinagharimu dola zaidi ya laki mbili hata laki tatu lakini jaribu kuomba mchango wa kupeleka mtoto wako shule, kununua madawati au kujenga ofisi nzuri ya walimu. Utaishia kuonekana kama fala tu. Halafu watu wanategemea wafanyiwe kila kitu na serikali - jambo ambalo haliwezekani. Kama mwamko uliopo katika mambo ya starehe ungekuwepo - japo kwa asilimia 1 tu - kwenye mambo ya maendeleo leo tungekuwa mbali sana. Pengine kusingekuwa na mtoto anayekaa chini au kusomea chini ya mbuyu! Nenda katika chuo kikuu cho chote hapa Marekani. Majengo mengi yamejengwa na watu binafsi na wameweka majina yao kama kumbukumbu. Matajiri wetu kweli hawawezi kujenga mabweni, mashule, na majengo mbalimbali yakatumiwa na umma? (Tazama http://matondo.blogspot.com/2009/08/kwa-nini-tusiwe-na-reginald-mengi-hall.html)

Hamu na tamaa hii ya "kuula" imezaa mashindano ya ajabu na ya kipuuzi, na mashindano haya ni uwanja wenye rutuba mno kwa rushwa, ufisadi na maovu mengine yanayoikumba jamii. Kama jirani yako amefanya harusi ya dola 50,000 basi wewe unajaribu kumpiku na kufanya harusi ya dola 100,000. Kama jirani yako anaendesha Toyota RAV4 basi wewe unampiku kwa kununua shangingi au Lexus. Jirani yako akijenga nyumba ya dola 200,000 wewe unampiku kwa kujenga ya dola 1,000,000. Kuhusu pesa hizi zinapatikanaje ni "Don't ask, don't tell". Vipi mashindano kama haya yangekuwepo katika dhana ya Kujitegemea mf. ujenzi wa mashule, uchimbaji wa visima vya maji, kusaidia walemavu na mayatima n.k. Tungekuwa wapi?

Serikali inayo lawama (vigogo huko nako wapo katika mashindano ya kuona ni nani atapokea lirushwa likubwa kumzidi mwenzake) lakini kama isingekuwa ni kutopenda haya maisha ya "peponi" ambayo ni ndoto ya kila Mtanzania matatizo mengine na hasa haya madogo madogo tungeweza kuyatatua sisi wenyewe hata bila kuisubiri serikali itufanyie kila kitu.

Nikienda nyumbani huwa nachekwa sana kwa kutokuwa na gari la kutembelea na badala yake kusafiri kwa daladala au Taxi. Utakaaje Marekani usiwe na shangingi la kutembelea unaporudi nyumbani? Mimi huwa nawauliza wachekaji wangu "ninunue shangingi halafu nimwachie nani?" Huwa nawaambia kwamba hata kama ningetaka kuwa na gari Tanzania pengine ningenunua Corolla tu - gari ambalo nalo pia nilishaambiwa kwamba ni gari la matineja wanaoanza maisha na si gari ya kuendeshwa na Profesa!

Falsafa hii ya "makamuzi kwanza" na mashindano ya kibubuza ni kipingamizi kikubwa kwa maendeleo yetu. Pengine inabidi tukumbuke maneno haya ya Kennedy "Ask not what your country can do for you, but what you can do for your country!"

Na ni kweli - blogu ni uwanja wa kujifunza na kupanua mawazo na hata kubadilisha misimamo ya muda mrefu. Kwangu mimi blogu imegeuka kuwa shule yenye manufaa sana na naamini kwamba nimebadilika tangu nianze kublogu. Tusongeni mbele!

Fadhy Mtanga said...

Rafiki yangu na kaka yangu Prof. Matondo nimeguswa sana na maoni yako. Dakika chache zilizopita nilikuwa nikiacha maoni kwa dada Yasinta kuhusiana na mambo ya kublog.
Nakiri nimebadilika sana tangu nilipoanza kublog mwezi Machi 2007. Zaidi nimejifunza kuwajibika bila kutegemea ujira.
Rafiki yangu mmoja alinikuta nyumbani nikiwa nimetingwa na notebook, vitabu na google nikichungua historia fulani ili niandike post. Rafiki yangu akaniponda napoteza muda kuandika katika blog nisikolipwa wakati historia ile ningeitoa magazetini 'ningeuza'.
Hapo nikajifunza jamii kubwa bado inaamini katika malipo ili iwajibike.
Kwangu katika kublog nimejifunza kuwa 'the first degree u need in ur life, is a degree of caring' hivyo kuwajali wengine ni pamoja na kufanya jambo pasipo matarajio ya malipo.
Wasioblog wanakosa mambo haya. Kufunza na kufunzwa. Daima huwa napenda kusema, sijutii kublog, na sitamani kuacha.
Kaka Mubelwa, na wanablog wengine, na wasomaji wetu, ninawashukuru sana kwa kunifanya nipende zaidi kuwajibika na kujiona nina deni kwa watembeleao blog zangu kila siku.
Nawashukuru pia kwa upendo wenu muuoneshao kila siku.
Pamoja daima.