Thursday, December 3, 2009

Nguvu ndani mwetu isiyo na nguvu kwetu bila nguvu miongoni mwetu.

March 5 niliandika kuhusu Nguvu baina yetu isiyo na nguvu ndani mwetu, yenye nguvu kwetu. (Isome hapa). Lakini katika kuishi nimeigundua nguvu nyingine ambayo ningependa kushiriki nanyi leo. Nayo ni ile iliyo ndani mwetu lakini haina nguvu bila nguvu ya wenzetu kwetu. Nianze kwa swali.
Ni wangapi umekutana nao sasa ambao wakati mkiwa shule ya "vidudu" walikuwa wakisemwa ni wajinga na sasa wamefanikiwa?? Ama wangapi waliitwa werevu na maisha yao si kama ambavyo walitabiriwa??
Unadhani kuna wangapi wakati mkiwa shule walionekana kuwa "wana akili" na sasa maisha yao ni ya kubahatisha? Unadhani akili zimepotea? Na kama zimepotea ni vipi zipotee kwa mtu mwenye akili? Kwani kuna asiye na akili?
Ninaloamini kuwa kila mtu ana nguvu za kufanikiwa ndani mwake japo nguvu hizo zahitaji msaada mkubwa wa wale wazionao kuziwezesha kuwafanikisha wenye nazo. Na ndio maana yule mwanafunzi aliyekuwa "akipendwa" na mwalimu nanii alionekana mwenye akili kwake kwani alipata msaada wa kutosha kutoka kwake. Na kweli akaonekana ana akili.
Lakini tuna mifano halisi ya wale ambao walikuwa wakiishi maisha yasiyo na muelekeo mpaka walipokutana na wale walioweza kuwasaidia. Napenda kutoa mifano miwili halisi ya Dadangu Koero aliyoitoa wa kwanza kumhusu YASINTA, MJASIRIAMALI ALIYESEMA HAPANA KWA WANAUME WAKWARE (Bofya hapa kuisoma) ama kuhusu KISA CHA SAIDI WA MBEKENYELA (Bofya hapa) ambao wote hawakuwa na maisha waliyotaka ama waliyoota kuwa nayo lakini baada ya "nguvu iliyo nje yao kufungua ile iliyo ndani mwao" wakaweza kufanikiwa na kufanikisha ndoto zao.

Labda wengi uwaonao "hawana" wanahitaji "msukumo mdogo" toka kwako kuwafanikishia ndoto zao ama nawe unaweza kuwa wahitaji kiasi kidogo cha msukumo kukufanikishia mema zaidi maishani mwako.
Kwa ufupi, MAISHA TUISHIYO YANATEGEMEA UWEPO WA WENZETU HIVYO NI VEMA KUPEANA A HELPING HAND

BLESSINGS

4 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Ni kweli. Wengi wetu tusingeweza kufika hapa tulipo bila kupewa msukumo na watu wengine. Mimi huwa nauchukulia kama wajibu wangu kuwasukuma (kwa namna yo yote niwezayo) wengine wanaohitaji msukumo wangu - wawe ndugu, marafiki au watu wasionifahamu. Hakuna ridhiko kuu kama kufahamu kwamba umemsukuma mtu akasukumika. Na mara nyingi usitegemee shukrani

Fadhy Mtanga said...

Kaka, mwalimu wangu mmoja alipenda kuniambia, 'if you don't use; you lose.' Akiwa na maana kuwa nguvu ama karama yoyote kama hutoitumia utaipoteza. Hivyo katika maisha yetu twapaswa kuzitumia vema nguvu ndani yetu na nguvu za wenzetu ndani yetu pamoja nguvu zetu kwa wenzetu. Kwa kufanya hivyo tunajihakikishia kutozipoteza nguvu hizo.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

nililazimika kukaa mbali na wale walioonekana kustahiri kunipa msukumo maishani (familia yangu ) na sasa naendelea vizuri kuliko nilipokuwa karibu nao!

Yasinta Ngonyani said...

Hakika, kupewa msukumo, kutiwa moyo ni kitu muhimu sana. Kwani kuna watu utakuta wanawaambia wengine we nini eti anataka kufungua duka utaweze kweli???? Badala ya kumwambia nakutakia mafanikio mema hata kama sio ndugu yako mpe moyo, mpe msukumo na uone nini kitatokea. Na kuna wengine wanasema kwani akiwa tajiri atanigawia na mimi sio hivyo tenda mema usingoje shukrani hapa duniani. Na wala usidai.