Tuesday, December 8, 2009

Maswali yangu 10 kwa Rais Kikwete

Najua angewaza kisha angenijibu

Ningeweza kupata muda wa kukaa na Rais wangu Jakaya Kikwete hasa siku hizi za kumbukumbu kadhaa za nchi yetu ningefurahi kufanya naye mahojiano. Ningemkumbusha kuwa licha ya sherehe za UHURU kesho, pia ni mwezi unaokamilisha nne-ya-tano ya utawala wake. Ina maana mwaka ujao utakuwa na mengine kisiasa zaidi ya kuwatumikia wananchi. Utakuwa ni wakati wa kwenda kutimua vumbi la barabara (kusema wanatengeneza maana uchaguzi unakuja). Utakuwa wakati wa kusalitiana kwa wanasiasa (wakijifanya wanawajali na kuweka mbele maslahi ya wananchi) na kwa hakika hakutakuwa na utekelezaji wa lolote kubwa kwa jamii. Kwa hiyo KIMAHESABU huu ndio mwaka wa mwisho kiutendaji kwa rais kabla hawajaanza kuwadanganya wananchi kutaka wapewe nafasi ya kuendelea kuwanyonya na kujilimbikizia mali.
Anyway
Ningepata kukaa na Rais Kikwete ningekuwa mkarimu n mpole na kisha ningeanza maswali yangu kama ifuatavyo.
1: Ningemuuliza kuhusu MIAKA MINNE anayotimiza akiwa madarakani na kama anadhani ametimiza asilimia 80 ya ilani yake ya uchaguzi (Si mnajua miaka minne kati ya mitano ni 80%?)
2: Ningemuuliza kama ana IMANI NA VIONGOZI wake wasaidizi, na kama ndio basi kwa asilimia ngapi. Na kama hana anafikiri ni kwanini anaendelea kuwa nao na anakabiliana vipi na hilo?

3: Ningemuuliza ameweza KUTEMBELEA MIKOA MINGAPI (ukilinganisha na ile aliyotembelea wakati wa kampeni na anayopanga kutembelea kwenye kampeni zijazo) na ameweza kutambua matatizo makubwa mangapi ambayo hakuyajua kabla? Na baada ya kuyatambua anadhani ana suluhisho kiasi gani?

4: Ningemuuliza anapata na kuhakiki vipi taarifa za utendaji wa mikoani.

5: Ningemuuliza ni MABADILIKO gani amefanya ama kupanga kufanya baada ya kuona hali halisi ya JELA alizozitembelea na kunukuliwa akisikitishwa na hali ya huko.

6: Ningemuuliza juu ya TAKWIMU halisi za maendelea ya ELIMU (sio majengo "yanayoota" kila kata)na pia Takwimu za AFYA (sio zahabati zisizo na dawa wala wauguzi) Ningemuuliza namna anavyoamini Serikali inawajali wale waliojitoa mhanga kuitumikia kama wafanyakazi wa Jumuia ya Afrika Mashariki, Walimu na wengine.

7: Ningemuuliza kama bado anaamini kuwa KILIMO NI UTI WA MGONGO WA UCHUMI WETU na kama kuna mipango yoyote ya kukiboresha. Hapa ningemkumbusha kuhusu AHADI aliyoitoa Waziri Mkuu kuwa wasingenunua Mashangingi na badala yake wangenunua matrekta kwani shangingi moja ni sawa na gharama za matrekta 20.(Jikumbushe Hapa)

8: Ningemuuliza juu ya MIUNDOMBINU na MAWASILIANO na kama anajua kuwa kuna mazao yanayooza mikoani kwa kukosa usafiri wa kuyaleta "sokoni" wakati kuna wanaokosa chakula upande wa pili wa nchi. Ningemuuliza kama tunatumia rasilimali kama mvua, mito na jua kwa manufaa ya jamii nzima.

9: Ningemuuliza kuhusu RUSHWA na MATUMIZI MABAYA yanayosemwa kwa serikali na watendaji wakuu wake na kama kuna hatua zinazochukuliwa juu ya hilo. Labda ningemgusia kuhusu "msururu" wa watu wanaoongozana kwenye mikutano mbalimbali ambayo nchi nyingine zawakilishwa na watu wachache (kama ilivyonukuliwa HAPA )

10: Ningemuuliza juu ya ZIARA zake za nchi za nje na kama anawaelimisha wananchi jinsi ambavyo ziara hizo zinaisaidia Tanzania. Hapa sina shaka kuwa kuna manufaa kwa nchi, lakini yeye kama MWAJIRIWA WA WANANCHI ANALAZIMIKA KUWAELEZA WANANCHI MANUFAA YA ZIARA ZAKE na ningeuliza kama anajua kuwa Tovuti hii mfu Ya Ikulu na Blogu ya Mawasiliano Ikulu ni kati ya zile zenye habari chache kuhusu utendaji wake kuliko blogu zetu kina "kachwele"?

Labda ningemuuliza kama HABARI ZA MAENDELEO YA UTENDAJI WAKE NI HAKI AMA ANASA KWA WANANCHI WA Tanzania?

Sina hakina na muda kama ungetosha lakini ningepata wa ziada ningeuliza kuhusu maendeleo ya Ripoti za Richmond na nyingine ambazo ninaamini "wanazifanyia kazi", ila hawajatujulisha walipofikia.
Najua angekuwa (kwa hakika ANASTAHILI) kuwa na majibu maana "anatenda kazi yake".

Uchaguzi Tanzania ni "label" inayozungumzia namna niionavyo nchi yangu ya Tanzania ijiandaavyo na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010. Kwa maandishi mengine juu ya mada hii katika "label" hii BOFYA HAPA

6 comments:

Bennet said...

Hapo sina la kuongeza maana maswali yejitosheleza, huu pia unaweza kutumiaka kama mwongozo kwa raisi wetu

twenty 4 seven said...

nakuunga mkono mkuu..

Faith S Hilary said...

Nimelipenda swali namba kumi. Na kama ungepata huo muda "kumkong'oli" hayo maswali, angekuwa hivyo hivyo kama alivyo kwenye picha.

Anonymous said...

Kaka shughuli hii pevu.Naam kumekucha.
Nduguyo Mike Mhagama.

Mzee wa Changamoto said...

Kama ilivyo desturi, napenda kutoa shukrani kwa wale wote mupitia hapa.
Na zaidi kwa "mgeni" kwenye maoni Kaka Mike.
Heshima kwenu nyote
PamoJAH

John Mwaipopo said...

nilikuwa sijapost comment kwa kuwa nilikuwa nayasoma maswali haya taratibu kama vile naulizwa mimi. yaani ningeulizwa mimi ningejibu vipi nikiwa rais ama kwa niaba ya rais.

wewe ndugu muuliza maswali haya unaweza kuwa kilo moja ya sukari ambayo haiwezi kubadilisha ladha ya maji ya bahari. lakini ni wazi ujumla wa ujumbe uliopo katika maswali haya hauhitaji kuwa hata na diploma kuukubali. pengine walio karibu naye katu hawathubutu kumuuliza ama kumwambia ujumbe huu au unaofanana na huu.

nasikia rais wetu huwa anasomaga blogu. akisoma hapa itakuwa bomba sana.