Monday, January 4, 2010

Tanzania yangu niipendayo..........Barabarani

Februari 10 mwaka jana niliandika bandiko hili. Na kwa kuwa mabandiko ya hapa hayapitwi na wakati (kama hayajashughulikiwa), nimeona nilirejeshe kwani nililosema miezi 11 iliyopita, ndilo litokealo sasa hivyo nimeona niirejeshe ikiwa na taswira za karibuni
Pamoja
Kama kuna miundombinu muhimu katika nchi (na pengine niseme nchi nyingi duniani) basi barabara ni mojawapo. Hiki ni chanzo cha mawasiliano, chanzo cha mahusiano na hata mzunguko wa pesa katika nchi nyingi na hasa zinazoendelea. Kwa ujumla, mfumo mzima wa sehemu kubwa ya wananchi unategemea zaidi aina hii ya miundombinu.

Ukweli huu unajidhihirisha nchini Tanzania ambapo barabara ni njia kuu ya usafiri kwa walio wengi. Ni namna ya kutumia katika kusafiri kwenda kujuliana hali, kufanya tafiti, kusambaza huduma mbalimbali kama za afya, kusambaza mazao na biashara na kugusa maisha ya walio wengi iwe ni kwa maombi ama mahubiri ama kuwajulia hali ama hata wanasiasa wanaokwenda kueleza nia zao za kutaka kuchaguliwa. Na pengine ndio njia pekee ya usafiri ambayo kila mwananchi wa Tanzania atakwambia kuwa ameshawahi kuitumia.

Lakini bado umuhimu wake hauonekani miongoni mwa viongozi wetu. Wameamua kuukana ukweli wa manufaa yake na wameamua kutokubali kuwa kuboresha barabara ni njia kuu ya kuboresha maisha maisha ya kujitegemea ya watanzania walio wengi. Bado hawaonekani kukubali ukweli kuwa wakiwekeza kwenye miundombinu kama barabara kutawawezesha wananchi kujiweza katika biashara na kilimo, katika kusambaza huduma mbalimbali na hata kupunguza tamaa ya wengi kukimbilia mijini

Nakumbuka mwanzoni mwa miaka ya 2000 serikali ilisamehe kodi kwa wananchi. Hii ilionekana kama jambo bora maana watu walikuwa wakikimbizana na mgambo na wengine kuvunjika na hata kufa kwa ajili ya kukwepa kukamatwa kwa kukosa kulipa Shs 5,000 za kodi. Msamaha ulipambwa na ukaonekana wawafaa wananchi. Mwaka 2003 nikabahatika kwenda wilaya ya Karagwe mkoani Kagera ambapo pia nilipata bahati ya kuhoji watu (kwa ajili ya kipindi cha Kazi kilichokuwa kikirushwa na Redio Times Fm) na kwa mshangao wangu na wa wengi nikakutana na kilio ambacho sikutegemea.

Watu walinionesha rundo la ndizi ziiviazo maeneo ya gulio kwa kuwa hakuna hata wa kubadilishana nao kwa paketi ya chumvi ya sh 50/= na kwa kuwa kuna nyingine zinazoiva shambani basi hakuna haja ya kurejesha hizo maana ni "kazi mara mbili". Nilipouliza sababu ya yote wakasema MVUA ZIMEANZA NA BARABARA HAZIPITIKI


Walichoniambia ni kuwa kama Dar mkungu unauzwa makumi ya maelfu na wao wanashindwa kupata hata wa kubadilishana naye kwa chumvi, basi hata msamaha wa kodi haufai. Wao (na mimi pia) tuliamini kuwa wa kama barabara zingekuwa nzuri, ina maana wangeweza kuuza bidhaa, kupata pesa, kununua chumvi na mengine wahitajiyo na hata kama kodi ingekuwa Sh 10,000 wangeweza kumudu. Nikaona kweli barabara mbaya ni kero.

Lakini nikakumbuka mara nyingi na tumekuwa tukishuhudia kilio cha wenye barabara mbovu na nzuri na vyote ni juu ya uhai. Unakumbuka El Nino ilipotenganisha mawasiliano ya nchi na hasa barabara na ni wakati huo ambako watu walikuwa wanaozewa na mazao yao ghalani ilhali wengine wanakufa kwa njaa. KISAAA?? Mawasiliano na hasa barabara

Kisha nikakumbuka "utamu" wa barabara nzuri ulivyo mchungu kwa wengine maana kila kukicha wanaona wenzao wanavyopukutika kwa ajali zitokanazo na uzembe wa madereva wanaokimbiza magari kuliko kawaida kwa kuwa tu BARABARA INARUHUSU na wenye dhamana ya kuwadhibiti wanabadilisha kazi zao kuwa mtaji na kupokea rushwa wakipuuza umuhimu wa maisha, mali za wasafiri na miundombinu ya wananchi?
Unadhani serikali haijui hilo? INAJUA NA INAJUA KUWA KILA MWAKA INATOA KAULI ZISIZO VITENDO na hili limedhihirishwa kwenye Hotuba ya kufunga mwaka ya Rais Kikwete kwa waTanzania (Isome hapa)aliposema
"Ndugu Wananchi,
Nasikitika kwamba bado hatujafanikiwa kudhibiti ajali za barabarani licha ya wito wangu wa kila mwaka katika salamu kama hizi na ule wa viongozi wenzangu kila zitokeapo ajali mbaya za magari barabarani.
Mwaka huu, hadi mwezi Septemba jumla ya ajali zilizotokea ni 15,798 ikilinganishwa na 13,405 zilizotokea katika kipindi kama hicho mwaka jana. Ajali hizo zimesababisha vifo 2,685 ikilinganishwa na vifo 2,040 vilivyotokea mwaka 2008. Idadi ya majeruhi imeongezeka kufikia 15,508 ikilinganishwa na majeruhi 12,508 mwaka 2008.
Kwa mara nyingine tena narudia wito wangu kwa watumiaji wa barabara hasa madereva kuzingatia Sheria ya Usalama barabarani waendeshapo magari. Ningependa kuona mwaka 2010 ukiwa mwaka wa mabadiliko mema kwa maana ya kupungua kwa ajali za barabarani.
Narudia wito wangu kwa Askari wa Usalama Barabarani kuwa makini katika kusimamia Sheria ya Usalama Barabarani na kuwawajibisha ipasavyo madereva wazembe. Aidha, naomba wahakikishe kuwa ukaguzi wa ubora wa magari yatembeayo barabarani unafanywa kwa dhati na siyo wa kurashiarashia. Na, kwa magari ya abiria ukaguzi ufanywe mara kwa mara. Pia, nawahimiza Wizara ya Mambo ya Ndani kukamilisha mchakato wa kuongeza adhabu kwa madereva wazembe. Nawaomba SUMATRA watafute namna ya kuwawajibisha wamiliki wa magari wasiojali uimara wa magari yao yatembeayo barabarani."


Hiyo namba ni kubwa saaana achilia mbali USAHIHI WA NAMBA HIZO (kwani sisi tulipopata ajali mpaka tunaondoka hospitali tulishashuhudia maiti 12 na kesho yake niliposikiliza habari Tanzania wakasema idadi imeongezeka na kufikia 8)
Ni barabara hizo hizo ambazo mwaka jana pekee zimeshakatisha maisha ya mamia ya watu katika ajali ambazo zinasikitisha hata kuangalia taswira zake na kutufanya kuwekwa katika kundi la nchi zenye barabara ziuazo zaidi duniani kama ilivyoripotiwa HAPA
.
Na viongozi wetu KAMA KAWAIDA YAO WANATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI, WANATOA MAAGIZO WASIYOFUATILIA na KISHA WANASONGA kama hakuna lililotokea.

Ni wakati wa kuamka, ni wakati wa kujali maisha ya wasioweza kuendesha maisha yao kwa kuwa barabara ni mbaya na kutetea na kuokoa uhai wa wale wanaopoteza maisha kwa kuwa
barabara si nzuri
Tuangalie baadhi ya taswira nilizoziona hivi karibuni toka kwenye blog njema ya Kaka Bennet ya MITIKI-KILIMO KWANZA (Ifuate hapa)
Tanga
Rukwa
Manyara
Ruvuma
It's 2010 MY PEOPLE. Election year. Let's Rise Up, Wise Up, Wake Up and Shake Up

Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA
Tuonane "Next Ijayo"

1 comment:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

duh, picha za baraabara hizi zinanikumbushambaali sana na meengi pia.

nilisafiri kwa basi kutoka Dar kwenda bk mwaka 2001. basi lilikukwa linaruka sarakasi. nilikaa siti ya mwisho. huuuuuuwi, mara liliruka juu lilipoa tua nikamkalia jirani yangu mwanamke, weeeeeeeeee hata hatukulalamika kwani tutafika lini ikizingatiwa dereva alitembea hivyo ili tufike bk ndani ya siku nne na sio zaidi