Saturday, January 2, 2010

Tunao wangapi magerezani mwetuuu?

James Bain (55) akitoka mahakamani baada ya kuachiwa huru. Bain alifungwa akiwa na miaka 19 kwa kosa la kubaka lakini baada ya kutumikia kifungo kwa miaka 35, vipimo vya DNA vimesaidia kuonesha kuwa hakutenda kosa hilo na sasa ni mtu huru.
Novemba 9 mwaka juzi niliwahi kuandika hapa kibarazani kuuliza Ubora wa jela ni nini na zetu ni namba ngapi? (Bofya hapa kuisoma) na niliuliza hivyo kutokana na simulizi ya Mhariri wa zamani wa gazeti la Family Mirror Bwn Zephania Musendo ambaye alieleza kile ambacho tumekuwa tukikisikia kila kukicha kuhusu Magereza yetu. Sikubahatika kupata jibu. Kisha August 4 mwaka jana niliuliza Kwani kazi ya jela zetu ni ipi???? (Irejee hapa) na hili swali lilitokana na makala niliyoisoma ya namna ambavyo Magereza katika jimbo hili la Maryland inavyotumika kufanya kazi za uzalishaji na kufundisha wafungwa stadi za kazi na maisha ili kuwasaidia watokapo. Napo kwa bahati mbaya sikupata majibu ya maswali yangu.
Lakini niliposikia kisa na mkasa wa huyu Mzee hapo juu ambaye kwa miaka 35 ametumikia kifungo asichostahili naanza kuwaza kuhusu idadi ya watu kama hawa tunayoweza kuwa nayo magerezani mwetu. Tunajua kuwa nchini mwetu kuna kubambikiziana kesi na hili halishangazai. Naamini viongozi wa juu wanalitambua (kama nao hawalifanyi) na nawaza ni kwanini wasitumie teknolojia iliyomsaidia mtu kama James Bain kuangalia upya wa kesi ambazo zina utata? Ni kweli kuwa nchini mwetu hatuna mashine za kufanya DNA kusaidia kuhakikisha tunawafunga watu waliotenda makosa? Sina hakika kama kuwafunga watu wanaotegemewa kurejea uraiani kuna faida katika magereza ya Tanzania kwani sidhani kama kuna wanalofunzwa wakiwa magereza kuwafanya warejee kama raia wema zaidi ya kuwaongezea usugu kwa adhabu na kukiuka haki za binadamu.
Kuna baadhi ya kesi ambazo zimeigawa jamii kutokana na utata wake na kama serikali ingeweza kuruhusu watu wakafanyiwa vipimo hivyo, labda tusingekuwa tunatumia pesa za wananchi kuwalisha na kuwatunza watu wasio na hatia katika mazingira ya wahalifu jambo linalowafanya nao wajikite kwenye fikra na mawazo ya kihalifu. Najiuliza kesi kama ya Babu Seya ambaye pamoja na watoto wake walihukumiwa kifungo cha maisha wakituhumiwa kuwadhalilisha kijinsia / kuwabaka watoto kumi wa Shule ya Msingi Mashujaa iliyopo Sinza Jijini Dar. Najiuliza kama walisema hawakutenda na wale watoto walikuwepo na Babu Seya na wanae wapo, ni kwanini serikali isingefanya vipimo kama hivi vya DNA kuangalia uhalali wa kesi na hukumu hiyo? Pengine Babu Seya na wanawe wote ni watu huru, ama kati yao kuna aliye / walio huru ama wote wana hatia, lakini kama kipimo hiki kingetumikabasi tusingekuwa na mgongano wa mawazo uliopo sasa. Watu wamehusisha kesi yake na mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na sanaa ya muziki na hata kuwahusisha vigogo wa serikalini.
Lakini ni kwanini tusifanye kitu kwa usahii kwa mara ya kwanza? Na kama kuna ambao ni watu huru huko magerezani (na kwa habari nilizokuwa nasikia kuhusu kubambikiziana keshi nina hakika wapo), ni kwa muda gani tutaendelea kuwashikilia? Na siku wakija kugundulika kuwa walifungwa kimakosa ni nania wa kubeba gharama za kuwafidia? James Bain sasa atalipwa $50,000 kwa kila mwaka aliokaa gerezani. Ina maana Jimbo la Florida litamlipa takribani dola milioni 1.75 muda mfupi ujao. Na hiyo ni kwa kuwa waendesha mashtaka walifanya makosa. Kama ulimwengu wetu wa Tanzania utabadilika (na naamini umeanza) na kupata watu watakaotetea haki za walio gerezani bila hatia, ni nani wa kulaumiwa?
Ni vipi tupate mabilioni ya kukarabati nyumba za watendakazi wa serikali na tukose vifaa kama hivyo kuamua kesi muhimu kama hizo?
Ni maisha mangapi yanawekwa pasipostahili kwa kuwa tu wenye dhamana hawajali HAKI NA USAWA wa wananchi wao?
Hebu msikilize James Bain alivyozungumza na CNN mara baada ya kuachiwa huru ambapo kilichowashangaza wengi amesema hana kinyongo wala hasira kwa kupotezewa zaidi ya theluthi mbili ya maisha yake kimakosa

Mahojiano ya kina kuhusu maisha, mabadiliko yake, hisia na kinachofuata baada ya kuachiwa huru unaweza kuyasoma na kuyasikiliza HAPA (na kwa wenzangu wapenda habari na waongoza mahojiano sikiliza anavyohoji mwanamama Michel Martin)
Blessings

Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA
Tuonane "Next Ijayo"

1 comment:

John Mwaipopo said...

inasikitisha. ninahofu familia ya nguza viking ilibambikizwa zigo hili kwa sababu fulanifulani. inawezekana mmoja wao ndio alikuwa fedhuli lakini kamwe haitaniingia akilini kuwa walifanya wote.