Tuesday, August 4, 2009

Kwani kazi ya jela zetu ni ipi????

Jumapili ya tarehe 9 mwezi Novemba niliandika hapa jamvini na niliuliza UBORA WA JELA NI NINI NA ZETU NI NAMBA NGAPI? (Bofya hapa kuisoma) ambayo ni mada iliyokuwa inahusiana na hii ninayotaka kuuliza leo.
Nimesoma kuhusu magereza za jimbo la hapa Maryland ambazo zinazalisha saana huku zikisaidia kubadili maisha ya maelfu ya wafungwa na kuwapa nyenzo na ujuzi ambao unawafanya waeze kujiendeshea maisha wanapotoka gerezani.
Mazao ama uzalishaji utokanao na magereza za hapa Maryland unathaminishwa kufikia dola milioni 51 na unaajiri wafungwa 1900 toka katika magereza 34 na wanatengeneza vitu mbalimbali kama Bendera zoote zipeperukazo jimboni, plate number za magari, uniform za baadhi ya wafanyakazi wa mamlaka za serikali na baadhi ya vifaa vingine maarufu vinavyotumika katika magari, boti na pikipiki zinazosajiliwa jimboni hapa.
Licha ya kupata mafunzo, wafungwa hawa hupata ujira mdogo wa dola 1.25 kwa saa ambazo huwapatia takribani dola 250 - 200 kwa mwezi.
Najua pato hilo linawatosha saana lakini kama serikali imewapa kandarasi magereza na pesa zake zinawekwa wazi namna zinavyozalishwa na hata kutumika na kuna faida katika hili, ni kwanini na sisi tusijifunze kutoka kwao?
Nimekuwa nikijiuliza kuhusu hali ya uzalishaji huko kwetu.
Najua kuwa kuna miradi mbalimbali inayoendeshwa na Magereza lakini ni wangapi wanaojua uendeshaji na uzalishaji wake?
Ni wangapi ambao wanaweza kuhoji kuhusu matumizi ya pesa zinazozalishwa kama hakuna anayejua zinazalishwa kwa kiasi gani na kutokana na nini?
Na ni nani anayeweza kutueleza mabadiliko yoyote yaliyofanywa na kitengo ama vitengo hivyo vya uzalishaji kwa Jeshi la Magereza?
Hakuna anayeweza kubisha kuhusu "kunona" kwa wakuu wa magereza na pengine ni kutokana na "kazi nzuri" wanayoifanya wakiwa wanaratibu mapato hayo. Sifa kubwa ambayo Askari magereza si kusaidia kuwafanya watuhumiwa na wakosaji kuwa RAIA WEMA watokapo gerezani, bali ni UNYANYASAJI na UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU kwa kuwasulubu watuhumiwa wakidhani ni wakosaji hata kabla hawajapelekwa mahakamani.
Ndio maana natamani wangeweza kuving'amua kama VYUO VYA MAFUNZO badala ya Magereza.
Nina hakika kuwa magerezani kuna watu weengi wenye ujuzi wa aina nyingi na ambao wangeweza kutumika kuzalisha vitu vingi na (angalau) kutupia pesa hizo kuboresha makazi na maisha yao. Serikali yetu HAIJENGI MISINGI MIZURI YA AJIRA NA KAZI NA PIA HAIBORESHI MAGEREZA. Sijui tunafikiria nini ilhali tunajua kuwa "usipojenga shule na kuweka misingi ya kazi na ajira basi ongeza magereza" kwani wasiokwenda shule na wakakosa kuishi "watajishughulisha" na ajira haramu na matokeo yake wataishia jela.
Mfumo mzima wa magereza unalalamikiwa. Watu kukaa muda mrefu wakisubiri kusikilizwa kwa kesi zao na wakati huo wakiishi katika maisha ya chini na hatari. Pesa ambazo zingezalishwa na Jeshi la Magereza zingeweza kusaidia kufanya ukarabati, upanuzi na hata ujenzi wa magereza mpya kama tu zingeweza kubuniwa, kusimamiwa na kupangwa vyema. Narudia, kama tu uzalishaji huo ungeweza kubuniwa, kupangwa na kusimamiwa vema kwa manufaa ya wananchi.
Kwa kutofanya hivyo, mwananchi wa kawaida anateseka kumlisha mahabusu anayetuhumiwa kuhatarisha maisha ya raia mwema (na pengine kwa kuwa huyo mahabusu hakuona maisha mbele yake) na kwa kipindi chote atakachokuwa mahabusu na hata gerezani, hatazalisha kiasi kinachomuwezesha kutimiza lengo la kumuweka mbali na jamii njema na kuondoa mzigo kwenye jamii.
Nilisahau kuwa hizi ni Hesabu za kisiasa ambazo Mara zote ni kinyume; wengi ndio wachache na wachache ndio wengi (Zisome hapa)
Labda wagombea urais nao wahojiwe kujua mipango yao juu ya hili, kwani serikali inatumia pesa nyingi kuendeleza vitu ambavyo vilistahili kujiendeleza na kuendeleza kwengine na kupuuza ambako kunahitaji uendelezaji halisi.

Naacha............Tuonane NEXT IJAYO
Uchaguzi Tanzania ni "label" inayozungumzia namna niionavyo nchi yangu ya Tanzania ijiandaavyo na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010. Kwa maandishi mengine juu ya mada hii katika "label" hii BOFYA HAPA

2 comments:

Fadhy Mtanga said...

Tungejifunza kwa wenzetu.

Ujue nini? Huku kwetu mfungwa ni mtu anaestahili kukandamizwa na kunyanyaswa. Si ndo ilivyo?

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

huwa sielewi sana kazi za magereza na kazi za maasikari woote. ni rahisi sana kuwakamata wananchi wema kuliko majambazi na matapeli na mara nyingi huwatumikia