Saturday, March 27, 2010

Asemalo kaka Freddy Macha......NALO NENO

Picha kwa hisani ya ukurasa huu wa mahojiano yake na mtandao wa BONGO CELEBRITY
Wiki hii imekuwa na BARAKA kweli kwangu. Achilia mbali ugumu wa maisha ambayo yako kila mahali na pengine kwa asilimia kubwa ya watu hivi sasa, lakini nimeendelea kuona baraka za aliye juu kwa kukutana na kufunzana na wengi. Na kati ya ambao nimebahatika kuwasiliana naye kwa mara ya kwanza ndani ya juma hili ni Mwandishi Makini na mkongwe Kaka Freddy Macha ambaye baada ya mawasiliano mafupi, nilimuomba apitie "kibaraza" hiki nikiamini kuwa atapata mambo atakayonishauri kuweza kuboresha. Niliamini hivyo kwa kuwa nimeona akifanya hivyo katika blogu kadhaa alizotembelea na amekuwa akishauri kile ambacho ninaamini ni sahihi. Na ndivyo alivyofanya. Alipopata nafasi aliipitia na kushauri mambo ambayo nimekubaliana na ushauri wake na naanza kuyatendea kazi.
Lakini alikwenda zaidi ya hapo na kutoa ushauri / changamoto (katika mfumo wa maoni) katika toleo lililopita hasa kuhusu AJALI ZA BARABARANI. Nakumbuka tarehe 2 Disemba mwaka jana niliweka toleo hapa lenye kichwa cha habari Blogu ni shule. Wafunzao ndio wafunzwao (bofya hapa kujikumbusha) na hilo limedhihirika zaidi kwa changamoto hii aliyoitoa Kaka Freddy aliposema
"Kuna haja ya wanahabari na waelemishaji jamii wote kuungana na kuanza kampeni kabambe kuhusiana na udereva wa kizembe, rushwa, magari yasiyofaa kuwa barabarani, nk. Mpaka jamaa wa nchi jirani zilizokuwa mbovu zamani kutuzidi, leo wameanza kuulizia mitaani Ulaya: "Oh nasikia ajali za magari zimezidi kwenu Matizedi."
Hii si aibu? Tanzania nchi ya amani imegeuka nchi ya ajali za vipanya, fuko na nzige? Kampeni yaweza kufanywa hivi. Wanahabari, waandishi, waalimu na waelemishaji kupiga kelele, kuungana kukemea hili tatizo. Mbona UKIMWI umekemewa (Oh vaeni mipira na soksi) ; mbona wanasiasa wabovu (mafisadi) wanasemwa...vipi vibaka wanapigwa hadi wakauawa kwa kuiba nyanya mbili sokoni? Kwanini dereva anayekimbiza kipanya cha "Hiace" hadi akaua hakemewi na waandishi na wale wenye "mikono" ya waelemishaji na vyombo vya habari? Mbona abiria wanakufa na tai, wanajikaza kisabuni; wanakubali eti ajali na uzembe huu eti ni sehemu ya majaaliwa ya " Ubongo" na "Wanabongo"?"


Kaka Macha kasema "KUNA HAJA YA WANAHABARI....." na naamini sisi ni sehemu yao. Na hii iwe CHANGAMOTO YETU sote tulio katika tasnia ya habari kusaidia kuzuia ajali zizuilikazo
ASANTE KWAKO KAKA FREDDY KWA CHANGAMOTO HII

Kaka Freddy Macha ni mwandishi na mtunzi mahiri ambaye anajitambulisha kama mtu apendaye "michezo, afya, lugha, sanaa, fasihi na kuukomboa ulimwengu dhidi ya ujinga, umaskini na maradhi". Mkusanyiko wa habari na kazi zake waweza kuupata kwa kuanzia HAPA

3 comments:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

anachokisema yaweza kuwa sawa. ila mimi kuna basi moja iliyokuwa ikipata ajali sana siku za nyuma, siku hizi iko bomba na naihusudu sana hiyo, haikimbii na madereva wametulia mno

ila hii nichangamoto inahitaji kufanyiwa kazi

kwa hiyo macha hatembelei blogu za watz mpaka haalikwe>>????

hiyo kali

Albert Kissima said...

Padre Privatus Karugendo katika makala yake kwenye gazeti la Raia mwema toleo namba 126 ameielezea Serikali ya Tanzanzania kuwa ni serekali inayotazama lakini haioni na yenye masikio yenye kusikia lakini haitaki kusikia. Ni kweli tunachoshwa na salamu za rambirambi kila kukicha,tunachoka kuomboleza kwa ajali nyingi za barabarani.

Kama serikali inatazama na haioni,kama inamasikio yasikiayo na haitaki kusikia kuhusu vilio na majonzi kwa wasafiri na huduma nyingine nyingi za muhimu,nini kifanyike?

Kuhusu hili la ajali nyingi za barabarani,binafsi naona abiria tunatakiwa kufanya kazi ya ziada. Ajabu sana abiria wakati mwingine wanaweza kuwa ni chanzo cha ajali. Kuna abiria ambao hupenda gari liende kwa kasi bila kujali athari za mwendo mkali. Abiria wanapaswa kuchukua hatua mahususi kwa dereva ambaye anaonekana kuendesha gari katika hali ya kuhatarisha maisha na pia abiria wanaoonekana kumuunga mkono dereva mzembe nao waadabishwe. Abiria waungane kwa pamoja kumuamuru dereva ambaye ameonekana kuhatarisha maisha asimamishe gari na abiria wawasiliane na kitengo cha usalama barabarani ili dereva husika achukuliwe hatua kali za kisheria. Ni vema pia kila abiria akawa na mawasiliano sahihi ya usalama barabarani. Kimsingi ni kuwa abiria sisi wenyewe ndio tukakaoweza kuokoa nafsi zetu. Tatizo kubwa ni kuwa abiria wengi hatujali nafsi zetu bali kuwahi kule tunapotaka kwenda.Kumfuatilia dereva mzembe wengi wa abiria wanaona ni upotezaji wa muda.Mimi nadhani abiria kuwa makini na namna ya uendeshaji basi wa dereva na kureact pale waonapo maisha yao yawekwa hatarini wakati wanasafiri ni suluhisho la pekee ktk kupunguza na hata kutokomeza ajali nyingi za barabarani. Madereva wa malori na magari binafsi nao wazidishe umakini.

Mzee wa Changamoto said...

@Kamala. Nafurahi kusikia kuwa hao wamejirekebisha. Lakini bado tukingali na wengi wanaohitaji kujirekebisha.
Kuhusu kualikwa, hata mimi hualikwa kusoma baadhi ya blogu ambazo wenye nazo hawana hakika kama nimeshazitembelea. Na hii haimaanishi kuwa huwa sisomi blogu za waTz.
Kwa hiyo labda yangu hakuwahi kuisoma kama ambavyo mimi sijaweza na sitaweza kujihakikishia kuwa nimesoma zote za waTanzania.

Kaka Albert. Umenena vema na nakubaliana na ushauri na mshangao wako hasa pale ambapo abiria twawa sehemu ya uchochezi wa chanzo cha ajali.
Blessings