Monday, March 29, 2010

Kwanini zilipendwa na vipi za sasa zitapendwa?

Kumekuwa na kutokueleweka kwa jina ZILIPENDWA ambako wapo waliodhani humaanisha nyimbo za kale sana na wengine wakiamini kuwa zimkuwa kiwakilishi cha nyimbo zote za kale huku wakiamini kuwa nyimbo zote za kale zilipendwa na kukubalika. Siamini katika fikra zote hapo juu.
Lakini licha ya kutokubaliana na kauli nzima ya ZILIPENDWA, ninaloona wasanii wetu wanapoteza ni KWANINI NYIMBO HIZO ZILIPENDWA NA NI VIPI ZA KWAO ZITAPENDWA.
Na leo ntajikita zaidi kwa wasanii wa "bendi za kisasa" na kuangalia kwanini tungo zao nyingi "zinapotea" katika ramani ya muziki kirahisi
Labda nianze kwa kuwarejesha nyuma kidogo mpaka Sept 30, 2008 ambapo niliandika nikiuliza Ni kipi tulichopoteza kwenye muziki wetu kisichorejesheka? (Irejee hapa) ambapo niliingia kwa kiasi kuuliza kama wasanii wetu wanafikiria kwa umakini kabla hawajabadili "midundo" ya miziki yao. Na nilitoa mfano wa Komandoo Hamza Kalala na Hussein Jumbe ambao wakiwa na bendi zao awali walivuma na kutunga nyimbo ambazo zinavutia kusikiliza hata sasa, lakini baada ya kuhamia "dansi ya kisasa" wamejikuta wakilazimika kufuata wapendacho mashabiki ambao hata hawajui wanapenda nini. Mwisho wa siku, wasanii WANAJIPOTEZA.
Ni sababu hii hii ninayoiona kwenye nyimbo hizi ziitwazo zilipendwa. Kwanza si nyimbo zote zilizoimbwa zamani zilizokubalika na kupendwa japo twajua kuwa kutokana na utaratibu uliokuwepo wa kuhariri kabla ya kurekodi, nyimbo nyingi zilizungumzia matatizo ama masuala halisi yaikumbayo jamii na hivyo KUPENDWA.
Haijalishi wimbo umeimbwa mwaka gani, kama utakuwa umeimbwa kugusa mahitaji na shida za jamii ni lazima utapendwa na kudumu. Ukisikiliza hizi ziitwazo "bendi za kisasa" na kusikiliza nyimbo zao zitokazo katika albamu za kwanza utafurahia mpangilio wa vyombo na maudhui (labda kwa kuwa huwa wana muda mrefu wa mazoezi) na mfano halisi ni nyimbo kama Mtaji wa Maskini wa TOT-Band ambao mpaka leo waweza hesabika kuwa kati ya nyimbo bora kabisa za bendi hiyo. Adolph Mbinga, Sister V (Much Respect to you Sis) Mimi na Rogert Hegga baada ya mahojiano 100.5 Times Fm 2002. Mbinga ameshiriki kupiga gitaa la solo katika nyimbo zote mbili za Fadhila kwa Wazazi
Lakini pia nyimbo kama Kisa Cha Mpemba uliobeba jina la albamu ya kwanza ya African Stars Band ulikuwa na bado una ujumbe wa kuelimisha leo hii. Lakini pia zipo nyimbo ambazo licha ya kuzungmzia masuala binafsi, bado zinaakisi maisha halisi ya wengi na mfano halisi ni nyimbo hizi zilizotungwa naye Rogert Hegga ziitwazo FADHILA KWA WAZAZI. Sehemu ya kwanza ilizungumzia mpango wa kuwatunza na kuwaenzi wazazi wakingali hai na sehemu ya pili yazungumzia namna ambavyo mambo yanaweza badilika kuliko tunavyodhani.

Kisha sehemu ya pili aliyoimba akiwa Mchinga Sound hapa chini

Mbali na Rogert Hega, tumuangalie Badi Bakule ambaye akiwa na African Revolution alitunga na kushiriki kuimba wimbo huu uitwao MTUMAI CHA NDUGU ambao hautachuja mpaka wale wote walio na tabia kama za CHANDE watakapobadilika na kuanza kufanya kazi. Na huu ni mfano wa nyimbo ambazo ZITAPENDWA milele kwani zimegusa meengi yaliyo ya kweli na halisi ndani ya jamii yetu.

Bendi walizopitia wasanii hawa baada ya kutunga nyimbo hizi zimerekodi nyimbo kadhaa lakini HAZITAMBULIKI kwa kuwa hazikugusa maisha halisi ya jamii na ndio maana hazikupendwa na hazitapendwa.
Ushauri kwa wasanii ni kukaa chini na kutunga nyimbo ziigusazo jamii na zenye kuisaidia jamii kujikomboa katika matatizo mbalimbali ikumbanayo nayo. Kwa kufanya hivi atakuwa wamekamilisha kazi yao kuu kama DARUBINI YA JAMII ionayo mambo na kuyachambua na pia kusaidia kuyatatua kwa njia iwagusao wengi kwa wakati mmoja.

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mitandao shirika hapa** . Ama ili kuweza kujua tasnia nzima ya muziki na wanamuziki wa Tanzania BOFYA HAPA

5 comments:

Born 2 Suffer said...

Za sasa pia zipo zitapendwa na zinapendwa kama nyimbo ya "Seya" haitasahaulika la hucoki kuisikiliza.

Fadhy Mtanga said...

Kaka umesema yote. Wasanii wanapaswa kutuliza akili wanapoandika nyimbo zao. Mimi hadi leo naupenda wimbo wa TOT wa elimu ya mjinga na huo mtaji wa masikini.

jfk said...

Hapa naona kilichotolewa ni mitizamo wa wasikilizaji na wapenzi wa muziki. Mtunzi wa kweli kamwe hautungi wimbo ili udumu milele, bali anatunga hisia zake za wakati ule. Hisia hizi zinaweza kutoa kitu kikadumu na zinaweza kutoa kitu watu hawakikubali kabisa. Ila tu mtunzi anaetunga kwa ajili ya kufurahisha soko hukuta nyimbo zake nyingi zikidumu kwa kipindi kifupi. Utunzi wa muziki wa kufuata soko huitwa 'bubble gum music' na kuna producers ambao hushughulikia muziki wa aina hii tu kwani huleta fedha za harakaharaka. Japo hutokea aina hii ya muziki ikajikuta inaingia katika nyimbo zinazodumu. Mtunzi wa kweli akitia hisia zake za kweli ndani ya wimbo wake mara nyingi wimbo hudumu. SANAA TABU YAKE HAINA SHERIA KUWA UKIFANYA HIVI MATOKEO YATAKUWA HIVI

Mzee wa Changamoto said...

@Kaka Born 2 Suffer. Ni kweli kuwa nyimbo za sasa zipo ambazo zitadumu kwa kuwa zimeigusa ama kuihusu jamii na pengine ndio sababu hazichokwi kusikiliza.
@Kaka Fadhy. Elimu ya mjinga ni majungu nao ni kati ya nyimbo njema ambazo (pamoja na Mtaji wa maskini) zinakumbukwa kama nyimbo zilizoipa TOT Band uhai. Nami husikiliza hizi ukilinganisha na nyimbo mpya zilizoimbwa hivi karibuni.
@ Uncle JFK. Kwanza karibu tena na asante kwa kutembelea. Nanukuu ulichosema "Mtunzi wa kweli akitia hisia zake za kweli ndani ya wimbo wake mara nyingi wimbo hudumu."
Na hili ni muhimu kwa wasanii KUWA WAKWELI KATIKA KILE WAANDIKACHO lakini pia kutoongozwa na hisia pakee. Mfano wa ulilosema ni wimbowa KILIO CHA YATIMA wake Mwinjuma Muumin ambao aliuimba kwa hisia kali baada ya kukataliwa likizo(kile alichosema) kuadhibiwa kwa kwenda kumuuguza babake.
Lakini hisia zetu pia zisifanye matatizo ya ujumla kuwa kama yetu pekee. Wimbo wa Mwinjuma na nyimbo Fadhila kwa wazazi za Katapila zote zazungumzia kuhusu wazazi, lakini Mwinjuma alikuwa too personal ilhali Katapila alilifanya lililomtokea kama FUNZO KWA JAMII NZIMA AMBAYO INAKUTANA NA TATIZO HILO.
Na (kwa mtazamo wangu) ni sababu nyingine kwanini Fadhila kwa wazazi zilizoimbwa miaka kadhaa kabla ya Kilio cha yatima zinafanya vema na kuweza kutumika kwa jamii nzima.
Blessings

John Mwaipopo said...

awali nimkumbushe born to suffer kuwa wimbo wa seya ulitikisha ulipotoka mwaka 2003 kwa sababu tu na wenyewe ni remix ya zilipendwa halisi ya miaka ya 80. sina kumbukumbu kama ilikuwa ni kundi la OSS(nikumbusheni). mvuvumko wake ulitokana na wapendi wa 'zilipendwa' hii kukumbushwa 'enzi zao'. hili la 'enzi zao' ndio nalieleza hapa chini.

kupendwa sasa na kupendwa baadae ili ziitwe 'zilipendwa' kutakuwepo tu.muziki ni kitu ambacho kinamkumbusha msikilizaji matukio na maisha ya wakati wimbo unatoka haraka kuliko picha, vitabu na hata magazeti. music brings back the memory more live and lively than photos, books etc.

pengine kinachotuhangaisha hapa ni ubora wa wa muziki kutokana na wakati. wakati muziki wa zamani ulitengenezwa na wanamuziki, muziki wa sasa unatengenezwa na waimbaji. vile vile, wakati wakina sisi na mubelwa tunadhani muziki bora ni ule uliotwangwa miaka ya 70 na 80 na pengine 90, watoto wa leo watakwambia ngoma tamu ni za kina Crazy GK, TID lady jaydee na mchizi mox (some names!). nao watakapokuwa kama akina sisi na mubelwa watakuwa wakitoa michozi watakapikuwa wakizisikia hizi. zitawakumbusha mengi waliyoshiriki wakiwa st. mary's na kungineko kwenye 'santa' na academy kibao