Sunday, April 25, 2010

Tunapojidanganya kuwa "mawazo tutakayo" yatabadili ukweli

Labda twajidanganya kuwa tuna sura nzuri, lakini akuangaliaye ANASOMA NINI usoni mwako? Tazama usomalo usoni mwa hiyo taswira na ndivyo tusomwavyo
Unapoangalia KUWAZA KWA BINADAMU na ukajitahidi kuwaza kwa undani wawazalo, wanenalo na kutenda unaweza kujikuta wawaza mara kadhaa kama kuna uhusiano wa kweli baina ya mawazo na maneno.
Hivi umeshatambua kuwa kama kuna kitu ambacho binadamu anakilipia ama niseme anawekeza lakini hataki kuona kikitumika juu yake ni "BIMA YA MAISHA"?
Niliwahi kuuliza ni kwanini bima ambayo haitumiki mpaka ufe yaitwa BIMA YA MAISHA badala ya Bima ya Kifo na sikubahatika kupewa jibu. Lakini huo waweza kuwa mfano halisi wa bin'adamu ambao licha ya kujua ukweli wa mambo bado twajitahidi kuishi kwa kuogopa kuujua ukweli huo (hata kama hilo halibadilishi ukweli wake). Yaani binadamu anapenda saana kuwaza jambo lakini namna alifanyavyo ni ile aaminiyo kuwa inaweza kubadili matokeo yake.
Umeshaambia habari ya kifo cha mtu ambaye amefariki ghafla (labda kutokana na ajali) ambaye mmeonana muda mfupi uliopita? Nini huwa wazo lako la kwanza? Najua wengi husema HAIWEZEKANI, wakiamini kuwa kwa kuwaza kuwa kifo hicho hakijatokea kunaweza kubadili lile aliloambiwa kuwa vile awazavyo. HUWA TUNAWAZA NINI?
Labda nigeukie huku "majuu". Jaribu kuuliza maisha ya huku kwa mtu na utasikia MAGUMU KWELIKWELI BORA NYUMBANI na kisha jaribu kuwa MKARIMU na kumshauri mtu huyohuyo arejee nyumbani anakoamini kuwa maisha ni bora zaidi ya hapa utashangazwa na atakachosema. Jibu laweza kuwa na lugha tofauti lakini kwa asilimia kubwa tegemea jibu la kuendelea kubaki hapahapa. Na hii ni ata kwa aliye Mwanza akahusisha Mwanza na Bukoba ama aliye Dar akaifananisha na Mwanza ama Bukoba ama hata Nachingwea.
Ni hili linaloweza kukufanya uwaze kama tunasema tunachowaza ama tunawaza sahihi na kusema kile ambacho twaamini kutatuwezesha kupata matokeo tofauti na tutegemeayo.
Umeshaangalia mahojiano ya mtu aliyekamatwa UGONI? Labda jikumbushe ya Tiger Woods yaliyofanyika wiki chache zilizopita na utaelewa ambacho nasema. Yaani mtu anakuwa mnyonge na mdogo na "KUJUTA" kwa alichofanya na kukiri kuwa alijua kuwa alichokuwa anakwenda kufanya si sahihi lakini alifanya akidhani matokeo yangekuwa tofauti.
Ukitazama video hii hapa chini (dk 4:47) anasema "I stopped living by core value i was taught to believe in. I knew my actions were wrong but i convinced myself that normal rules didn't apply. I never thought about who i was hurting, instead i thought ONLY about myself"
Labda la kujiuliza ni kuwa ni mangapi wawaza ukiamini kuwa kuwaza uwazavyo kutabadili kilichotokea?

LEO NAWAZA MIWAZO YA WAWAZAJI "BINADAMU" NA SIJUI HUWA WANAWAZA NINI NA HATA SIJUI NINAWAZA NINI KUWAZA BINADAMU WANAWAZA NINI?

***"Waliwaza nini ni kipengele cha kuelimishana tukifurahia. Hiki kitakuwa kikikuletea habari za kweli na kushangaza kuhusu watu ambao wamefanya yale ambayo unaweza kujiuliza kuwa WALIWAZA NINI? wakati wanatenda haya.
Kitakuwa na habari fupifupi kutoka ulimwenguni kote. Kwa habari zaidi kuhusu kipengele hiki
BOFYA HAPA"***

4 comments:

Fadhy Mtanga said...

Kila nipitapo hapa huachi kunifikirisha sana mkuu.

Yasinta Ngonyani said...

kwa kweli hata mie kuna kitu nawaza< lakini sijui nawaza nini. Kwani kusoma hii posti kumenifanya niwaze kitu. Ahsante, na jumapuli njema wewe na familia yako-

Unknown said...

Kwa mara nyingingine tena umewasilisha. Ahsante sana mkuu. Hata mimi mara nyingi sana nimejikuta njia panda kujaribu kufanya yale ambayo kama yakienda kombo basi utawaacha watu midomo wazi kuwa "aliwaza nini" Huu ni mstari mwembamba sana katika maisha yetu kama binadamu. Ni mwembamba kiasi kwamba kuuvuka ni rahisi mno... Na pindi ufanyapo makosa, majuto huwa hapoo kwenye kona... Mkuu ahsante sana.

SN said...

Hii imeakisi jambo fulani ambalo kama binadamu nashukuru kuwa na uwezo huu: KUFIKIRIA NA KUWAZA. Ukijaribu kutafuta jambo chanya kwenye hili suala utakubaliana nami kuwa ubongo au akili zetu zina "nguvu" ya aina yake (ingawa hatuwezi kutekeleza yale yote tunayowaza).

Nadhani mpaka sasa hivi hakuna maelezo mazuri ya sababu hasa ya sisi kuota.

Ingekuwa vipi kama tungeweza kutekeleza yote tunayowaza? Hilo ni swali dogo tu (lakini ni kama brain gymnastics)...