Monday, April 26, 2010

Za Kale vs Maisha ya Sasa...........VIP

Hayati JERRY NASHON "Dudumizi" Picha: Wanamuziki Tanzania Blog
Umeshawahi kuhitaji kitu na usiweze kukipata licha ya kuwa tayari kutoa lolote kukipata? Mbaya zaidi ni unapohitaji kitu ambacho kinaendelea "kukuandama" kila uendapo? Basi haya si mambo mageni maishani mwa wengi kwani suala la kupenda kitu usichokuwa na uwezo wa kukimiliki ni miongoni mwa sehemu za maisha.
Laki pale ambapo kipendwacho ni PENZI LA DHATI, basi maumivu yake huwa mabaya ama magumu zaidi.
Na ni hapa ambapo wengine huwaza kila aina ya njia inayoweza kuwapatia wahitajilo. Wenye pesa nao hujitahidi "kutumia pesa kama fimbo" ili kuwawezesha kupata wahitajilo.
Lakini ukweli ni kuwa kuna baadhi ya vitu VISIVYONUNULIKA kama PENZI LA KWELI.
Kakangu Mfalme Mrope ama Mzee wa Kustaarabika amejadili jitihada za wanadamu Tunapohonga ili kupata penzi.. (ifuate hapa) na inavyoweza kuwashangaza wengi namna ambavyo "tunawekeza" katika kile tunachofikiri ni upendo.
Haya hayajaanza leo. Yalishazungumzwa na kuimbwa na wengi na mmoja wa aliyefanya hivi kwa ustadi mwema saana ni JERRY NASHON "DUDUMIZI" (msome hapa kwa Uncle Kitime) ambaye akiwa na kundi zima la VIJANA JAZZ BAND walizungumzia haya.
Hapa Jerry anaanza kwa kueleza kwa machungu yasiyopimika akisema "akhera hakuendeki, dunia haikaliki, nimepatwa na mfadhaiko. Si maji wala soda vitakavyozima kiu yangu, ila ni wewe V.I.P"
Na katika kiitikio cha wimbo huo, Jerry Nashon anaeleza namna ambavyo anatamani kama angekuwa na nafasi ya kuweza kumpata VIP lakini anatambua kuwa hilo halitendeki hivyo kwenye mapenzi anapoimba akisema "binadamu hanunuliwi kama nguo VIP, ungekuwa dukani ningekununua nikuweke ndani lakini nikikuchukua bila mapenzi yako, utanitoroka"
Na kisha anaonesha "nia ya kuwasha moto wa mapenzi" kwa VIP na anaeleza mengi mema anayotamani kuyatenda japo anajua kuwa mawazo yake hayana usahihi wala suluhisho kwa yale awazayo.
Sikiliza kibao hiki MURUA ambacho kilishiba (hasa kwenye ala) ambapo gitaa la solo naamini lilikung'utwa na mmoja wa wanaoaminika kuwa na utundu mkuubwa saana katika kulitumia "mhitajiwa / mtakiwa" SHAABAN YOHANA "Wanted" (mjue hapa)
Kwa bahati mbaya kibao hiki kina ubora wa chini kiasi

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mitandao shirika hapa** . Ama ili kuweza kujua tasnia nzima ya muziki na wanamuziki wa Tanzania BOFYA HAPA

5 comments:

jfk said...

Unajua mambo mengine ni ya ajabu sana. Nakumbuka toka mwanzo wa utunzi hadi kurekodiwa kwa kibao hiki na hata majaribio ya kutengeneza video yake, lakini katika kusoma uchambuzi wako ndo nimeanza kufikiri jinsi maneno ya wimbo huu yalivyo na falsafa kali. Ukianza kunyumbua sentensi kwa sentensi na kuitafakari, unakutana na ukweli ambao utabaki kuwa ukweli daima. Na huo ndo utunzi wa hali ya juu kwa mtazamo wangu. Na kuna somo la wazi penzi la kweli halinunuliki wala halipatikani kwa kuhonga vitu

Mzee wa Changamoto said...

Shukrani saana Uncle Kitime kwa KUTUNZA KUMBUKUMBU na pia kusaidia KUIHAMISHA toka kizazi chenu kuja chetu.
Mengi ambayo nilikuwa na utata nayo juu ya muziki na WANAMUZIKI TANZANIA umeyaweka bayana na kunisaidia kuyatambua vema hivyo kuuelewesha umma wetu kwa uhakika zaidi.
Umezungumzia namna ambavyo "mambo mengine ni ya ajabu sana" na kwangu ninaliona hilo. Kwani sasa nashindwa namna ya kukushukuru kwa kufanikisha suala zima la muziki na wanamuziki na kuacha / kuweka kumbukumbu sahihi isambaayo dunia nzima kwa urahisi na uhakika zaidi.
Kuona kuwa kuna kitu waweza kukumbushwa kupitia kipengele hiki yanifanya niwe speechless na nakushukuru wewe zaidi na WANAMUZIKI WOOOTE WEMA kwa kutuburudisha, kutufunza na kutukomboa kiakili.
Baraka kwako na nashukuru kwa kuendelea "kujishusha" na kusoma habari za muziki na TUNZI HIZI ZA HALI YA JUU toka kwetu vijana
Baraka kwako

Fadhy Mtanga said...

Kwa mshairi kama mimi, kitu cha kwanza kinachonivuta katika wimbo wowote, ni ufundi wa kuandika mistari. Huwa nawaambia rafiki zangu, napenda sana hizi nyimbo kutokana na ubingwa wa ushairi.
Halafu nashangaa kwanini wanamuziki hawa hawahesabiwi kama mafilosofia.
Ahsante sana kaka kwa tungo muruwa kama hii.

chib said...

Mkuu umenikumbusha mbali sana.

REEN said...

Hongera Mzee wa Changamoto,

umeelezea vizuri huo mwimbo wa VIP hata ule wa kupiga vita AIDS wa Philly B, kifupi umenikumbusha mbaaaaali...

Ubarikiwe zaidi