Thursday, April 15, 2010

Wastaafu wa AFRIKA MASHARIKI wasubiri, wabunge ni "express pay"....

Februari 22 niliandika habari isemayo Tanzania Yangu....Yenye wabunge wa wananchi wawanyonyao wananchi. (Isome hapa)
Leo wakati najiandaa kuweka bandiko la Alhamisi nimekutana na habari hii nikaona ni vema kukumbushana kuhusu nililosema huko nyuma. Habari hii ni kutoka mtandao wa IPP Media.
Kwa muhtasari tu ni kuwa Wazee hawa wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaendelea kudai mafao yao wanayosema kufikia kiasi cha shilingi bilioni 450 ambazo ni mafao yao waliyostahili kulipwa baada ya kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977. Ni miaka 33 sasa imepita, lakini wabunge ambao bunge lao litafungwa mwezi Julai, wamehakikishiwa kuwa pesa zao (zinazoweza kufikia kiasi cha shilingi mil 46 kwa kila mbunge aliyemaliza mhula mzima) watazikuta kwenye akaunti zao ifikapo mwisho wa mwezi wa nane.
MUNGU ATUSAIDIE SOTE....


Endelea na habari hii toka NIPASHE

Wazee wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki jana walizua tafrani kubwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania wakati wakipinga uamuzi wa mahakama hiyo wa kuahilisha tena kesi yao, hali iliyowalazimisha polisi kufanya kazi ya ziada kuwandoa mahakamani hapo.

Kabla ya kuanza kwa tafrani hiyo, wazee hao zaidi ya 200 jana walifika mahakamani hapo kusikiliza hatma ya mwisho ya kesi yao ambalo liko katika hatua ya kukaza hukumu ya kesi yao ya madai dhidi ya Serikali.

Baada ya kuingia mahakamani, Jaji Njengafibili Mwaikugile ambaye aliamua kuahilisha kesi hiyo hadi Aprili 30, mwaka huu na kuwataka wazee hao ambao wanadaiwa kugawanyika katika makundi mawili kuketi pamoja na kuelewana kabla mahakama haijatoa uamuzi.

Uamuzi wa Jaji Mwaikugile ndio uliosababisha wazee hao kuja juu, huku baadhi yao wakisema kuwa hawawatambui baadhi ya wenzao ambao mahakama inawataka wakae pamoja kuelewana.

Mmoja wa wa wazee hao, Mchimu Bakari, alisema katika kesi hiyo wanaidai Serikali Shilingi bilioni 450 ambazo ni mafao yao waliyostahili kulipwa baada ya kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.

Alisema baada ya hukumu hiyo, kundi la wazee wenzao saba liliibuka kupinga hukumu hiyo, na kuamua kukata rufaa ambayo baadaye ilitupiliwa mbali.

Alisema wakati wa mwenendo wa kesi hiyo Jaji Aisha Nyerere aliwahi kulikataa kundi hilo na kusema kuwa mahakama hailitambui, lakini wanashangaa leo mahakama hiyo hiyo kuwataka wakae na kuelewana.

Baada ya kuzuka kwa tafrani hiyo, iliwalazimu polisi kuingilia kati kuwatuliza bila mafanikio, hali iliyowasababisha kuomba msaada wa FFU.

FFU walipowasili, askari wengine kwa kushirikiana na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Kati, Wilbrod Mutafungwa, walijaribu tena kuwatuliza wazee hao, kwa madai kuwa walikuwa na tangazo muhimu la kuwaeleza.

Wazee hao waliponyamaza, Mutafungwa alianza kuwaeleza kuwa njia wanayoitumia ya kupiga kelele mahakamani hapo haiwasaidii kumaliza tatizo lao na badala yake wanapaswa kukaa chini na kujenga hoja za kuieleza mahakama kupitia kwa wanasheria wao.

Baada ya maelezo hayo, aliamuru mlango mkubwa wakuingilia mahakamani ufunguliwe na wazee wote watoke nje ya eneo la mahakama.

Wazee hao walitolewa nje ya uzio wa mahakama chini ya usimamizi wa FFU na baada ya hapo walianza kutawanyika taratibu na baada ya muda eneo hilo lilibaki wazi.

Baadaye polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wazee hao baada ya kukusanyika nje ya jengo la Polisi Kati muda mfupi baada ya kutoka Mahakama Kuu.

Hata hivyo, hatua hiyo ilishindikana na watu hao waliendelea kukaa hapo huku wakishangilia kwa kuimba nyimbo mbalimbali.

Kundi la wastaafu hao likiongozwa na viongozi wake sita pamoja na wakili wao, Pius Chabrama ,walifika jana eneo hilo majira ya saa 6:30 mchana kwa lengo la kuongea na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.

Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCO), Charles Mkumbo, alitoka ofisini na kuwaambiawatawanyike lakini walikaidi.

Bada ya hapo polisi walinza kufyatua mabomu kuanzia saa 6:50 na kudumu takribani dakika tano.

Hata hivyo, kikao cha dharura kilichodumu zaidi ya saa moja kilichohusisha Kamanda Kova na viongozi sita wanaoongozwa na Mlaki pamoja na wakili Chabruma, kilifikia makubaliano kuwa, wastaafu hao waheshimu uamuzi uliotolewa na mahakama.

CHANZO: NIPASHE

2 comments:

Koero Mkundi said...

Niliwaona wazee wale.... kwa kweli inasikitisha kwa jinsi wanavyotendwa na watawala watawala wetu...

Hii inatosha kabisa kuwanyima kura zetu, lakini Je ni watanzania wangapi wanijua dhulma hii? au nfdio yale yale ya kupewa Vitenge khanga na fulana ili tuwape kula warejee kututawala?

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Mwenye nacho ataongezewa na asiyenacho hata kile alichonacho atanyang'anywa.

Fungu nimelisahau. Pengine Koero atanisaidia....