Monday, April 12, 2010

Za Kale vs Maisha ya Sasa....DUNIA IMANI IMEKWISHA

Nimewai eleza sababu kuu ya kuwa na kipengele hiki (na hata cha I & Them) ni kuhusisha miziki hii muhimu na maisha yetu tuishiyo. Miziki hii iitwayo ZILIPENDWA kutoka kwa wasanii waliotumia muda mwingi mwema kuielimisha jamii huonekana kupuuzwa na hata kutojaliwa licha ya KUTUMIWA KAMA CHOMBO CHA STAREHE CHA VIONGOZI kama ambavyo nilieleza HAPA
Na ndio maana ninapenda ku-enzi miziki iliyo na uhalisia wa maisha yetu ya kila siku, yenye kuielewa na kuieleza jamii na pia iliyo sehemu ya matatizo ya jamii. Na kwa Jumatatu huwa nafanya hivyo katika miziki hii ambayo inaitwa ZILIPENDWA.
Hii ni kwa sababu mimi pia ni mpenzi wa miziki halisi inayogusa maisha ya jamii yetu. Muziki wenye kuikomboa na / kuielimisha jamii. Ambao unasisitiza kwenye kujitambua na kuwawezesha wananchi kunyanyuka na kupiga hatua mbele badala ya kukaa na kubweteka kuisubiri serikali kufanya kila kitu.
Na tunapozungumzia miziki ya zamani badi hatuwezi kumuweka kando Jabali la Muziki Marijani Rajabu. Akiwa mmoja wa watunzi mahiri wa muziki nchini Tanzania, Marehemu Marijani aliweza kuyaeleza kwa ufasaha kabisa yale ambayo yanaikumba jamii nyakati hizo (na kwa bahati mbaya mengi bado yanaendelea tena kwa aina na kiwango kipya na kikubwa).
Tunafungua naye dimba hili kwa kibao chake DUNIA IMANI IMEKWISHA. Humo utamsikia Jabali na wana Dar International walivyoelezea jinsi nyoyo za watu zilivyobadilika, kupungua ama kuisha kwa uaminifu na hata namba ya binadamu ilivyo ndogo ukilinganisha na watu. Pengine wapo ambao hawakutambua namna unavyoweza kuwa mtu usiwe na ubinaadamu. Si tunawaona wanavyoiba pesa ya uma na kuwatesa waliowaweka kwenye nafasi hizo? Si tunaona wanavyowaua ndugu zetu albino ili wawe na mali? Si tunawaona wanavyowaua wenzi wao ili wasigawane mali walizochuma pamoja? Ama huwaoni wanaodhulumu watoto na wajane kwa kuwa hawana mtetezi wa mali zao? Si tunaona wanavyofilisi makampuni ya umma kwa starehe zao binafsi?
Hayakuanza jana wala leo, walishayaona kina Marijani.
Sikiliza Dar International wana Super Bomboka wakisema DUNIA IMANI IMEKWISHA

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mitandao shirika hapa** . Ama ili kuweza kujua tasnia nzima ya muziki na wanamuziki wa Tanzania BOFYA HAPA

1 comment:

Albert Kissima said...

Naam,nakifurahia kipengele hiki kwani chanipa hamasa kubwa ya kuzidi kufuatilia kazi hizi za wasanii wa enzi hizo. Napenda namna uhusishavyo kazi hizi (kulingana na ujumbe ulikusudiwa) na maisha ya kawaida ya sasa na hata ya baadae.