Sunday, May 23, 2010

USWAHILI, MSWAHILI NA KISWAHILI

Tunatambulishana na kutambulisha vitu kwa namna ama mitindo mbalimbali (japo si lazima utambulishanaji huo uwe sahihi ama makini)
Mfano: Kuna mchekeshaji mmoja mwenye asili ya Amerika ya Kusini, aliwahi kusema kuwa si lazima uwe umezaliwa kwenye ukanda atokao yeye ili utambulike kuwa ni m-Latino, bali ukishafanya / kupata huduma za ki-benki (kama ku-cash check nk) kwenye liquor store, basi wewe ni m-Latino.
Nilifurahia tu sentensi yake kwa kuwa najua kinachowafanya ndiugu zetu hao wafanye hivyo, lakini jana nilipokuwa nasikiliza nyimbo kwenye mp3 yangu, nikakumbuka nilivyokuwa naitwa MSWAHILI.
Basi kama wako sahihi, hapa chini paonesha maisha na harakazi za kwetu

Na siwezi kupinga kilichonifanya kuitwa hivyo kwa kuwa nilijua fikra za walioniita MSWAHILI. Kwao waliamini kuwa kuongea kwa namna fulani ama hata kusikiliza miziki yenye mafumbo ama lugha fulani ni uswahili. Na mimi nilikuwa natimia kwenye tafsiri yao. Nilipenda na bado napenda maongezi yenye kueleza kitu kwa namna ya kibunifu. Nilipenda na bado napenda maongezi ambayo yana mifano na kuchangamsha akili. Nilipenda na bado napenda maongezi ambayo yana TUNGO TATA.
Yaani kwangu ningependa kusema "chupi ya maziwa" badala ya sidiria. Chumba cha bwenini ungesikia mtu akiulizwa kama fulani ni "bubu wa masikio" badala ya kiziwi kwa kuwa tu hakusikia ulichomueleza. Ni misemo miingi sana ya kueleza kitu kwa namna yake. "Mtoto' ingekuwa na maana nyingi kulingana na sentensi na sasa ukiongezea "mtoto si riz'ki" nayo ingemaanisha vingine. Ilikuwa raha.
Lakini pia nilipenda kusikiliza nyimbo zilizokuwa na MAFUMBO na hata TUNGO TATA. Sasa nikaambiwa hiz ni nyimbo za kiSwahili kwa kuwa zilikuwa zikisema vibaya na wengine kusema ati zilikuwa zikitusi. Lakini nililogundua ni kuwa nyimbo hasa MDUARA ni nyimbo za kufikirisha na pengine badala ya kuziita za kiSwahili, tujifunze kuuliza kisemwacho na kama kina utata basi tusiwe wepesi kuamua alichowaza muimbaji bali tuwaulize waimbaji.
Leo nimekumbuka haya baada ya kusikiliza albamu yangu yenye mkusanyiko wa nyimbo za mduara na nimeona nishirikiane nanyi mawazo haya. Nikisikiliza nyimbo SHANUO na SITISHIKI zao Chuchu Sound nafurahishwa na upangiliaji wa vina na matumizi ya kiswahili fasaha. Mfano wanaposema "maisha si mashindano japo kipato kikubwa unacho wewe". Lakini pia kuna tungo chache Tata ambazo waweza zisikiliza hapa

Pia maumbo yaoneshayo uhalisia wa maisha kama "ni rahisi kuteka maji kwa pakacha kuliko yeye kuniacha" ambalo ni funzo kuwa kuna sehemu nyingine si za kujisumbua "kuharibu"
Lakini kuna mengi ya kujifunza katika "kauli" zao mwishoni. Labda tusikilize ili kujua tujifunzalo na pengine uwaze NINA WAZA NINI nisikilizapo hizi na pia waweza KUWAZA kama wawazao akili zangu kuwa za "kiswahili" wako sahihi

Na sasa tuhamie kwenye SWEET BABY ya TOT-Plus. Kuna kauli ambazo zilikuza mashaka lakini moja ya ambayo nilibahatika kuwa na mdahalo ni ile ya "Anti" ambayo wamezungumzia ku"gonga hodi mara 2 mbele, kama kimya gonga kimya mara 3. Kama kimya mwaga mzigo wako hapohapo nje. Ataupata". Tofauti pekee niionayo kati ya kilichoimbwa hapa na kwetu uHayani ni kuwa sisi kama umegonga mbele na nyuma hujamuona mtu, waacha ka-jani ka mgomba ili wakirejea wajue kuwa kuna aliyekuja akawakosa. Hatumwagi mzigo wao (labda kama umeambiwa ama kukubaliana hivyo). Sikiliza mwenyewe na uwaze.

Katika nyimbo hizi, kuna misemo miiingi sana ambayo inaweza kwenda na maana halisi lakini ikanyambulishwa visivyo. Kama nilivyosema HAPA kwa Binti Mkundi, "Mfano wimbo wa Aungurumapo Simba RMX ambayo Banza aliweka uhalisia wa maisha yetu japo wapo waliotafsiri kama matusi. Alisema "RAHA YA CHUNGWA, UMENYEWE, KISHA UKATIWE". Mimi ni kati ya walaji wazuri wa chungwa, lakini kila ninapofikiria kulimenya na kubaki na harifu ya maganda baada ya kula najiuliza mara mbili kama "kweli nahitaji kula chngwa wakati huo ama la?'" Na nikimpata wa kulimenya na kukata, NAWEZA KULILA WAKATI WOWOTE. Katika wimbo huo huo, Banza akasema "RAHA YA DAFU, UKISHAKUNYWA YALE MAJI, SHARTI DAU LICHOKOLEWE". Sijui atakayepinga kuwa hu ni ULAJI wa asili wa dafu ni nani? Kama huna kichokoleo kizuri basi ndio ungehitaji "njia m'badala" kama kulivunja kisha ukatumia kichokoleo chako hafifu kulila. Na sehemu nyingine akasema "RAHA YA NANGA BAHARINI, MTONI ITASHIKWA NA TOPE." Kwa sisi tuliokulia kwenye misafara ya majini wajua nanga. Na kwa wavuvi wanajua karaha ya nanga yenye matope. Haimaanishi kuwahuwezi kushusha nanga mtoni (maana waliozoea kuvua mtoni wanafanya hivyo) ila SI KWA RAHA KAMA BAHARINI. Na huo ni ukweli ulio wazi. Sasa kutafsiri vingine na wanavyouliza watu nadhani si tatizo la muulizaji, bali la mtafsiri.
UKWELI NI KUWA NAWAZA SIJUI NINAWAZA NINI?

***"Waliwaza nini ni kipengele cha kuelimishana tukifurahia. Hiki kitakuwa kikikuletea habari za kweli na kushangaza kuhusu watu ambao wamefanya yale ambayo unaweza kujiuliza kuwa WALIWAZA NINI? wakati wanatenda haya.
Kitakuwa na habari fupifupi kutoka ulimwenguni kote. Kwa habari zaidi kuhusu kipengele hiki
BOFYA HAPA"***

10 comments:

Fadhy Mtanga said...

Kaka Mubelwa leo umenisuuza sana nafsi maana mie nazipenda sana tungo tata za Kiswahili. Watu wengi hawataki kukubali ukweli, na hao ndiyo wanaokidharau Kiswahili. Ninao rafiki zangu hawataki kusoma mashairi yangu kwa kuwa nimeyaandika kwa Kiswahili.

Huwa najiuliza saana, kwa nini tunakuwa watumwa wa kiakili kiasi hiki? Nalazimika kuwashangaa kwani Kiswahili ni lugha ilosheheni misamiati na mafumbo chungu mbovu. Kiswahili ni kitamu sana ati yakhee!

Mwezi January nilikutana na Sean Langan, mwandishi mashuhuri wa BBC. Wakati wa maongezi yetu, aliniambia anakipenda sana Kiswahili kwa kuwa ni Sing-song. Akimaanisha lugha tamu ilokaa kishairi. Hakuzungumza Kiswahili lakini aliniambia mkakati wake baada ya kumaliza kutengeneza documentary izungumziayo reli ya Uhuru (tayari inaoneshwa na BBC 4) ataanza mafunzo ya lugha ya Kiswahili. Nimempa nyimbo nyingi za Kiswa.

Mwaka juzi nilikutana na Marion Geiss, binti Mjerumani anayemwaga Kiswahili kama maji. Anapenza muziki wa Kiswahili. Nilimpa darasa kidogo la ushairi wa Kiswahili. Sasa yupo Ubelgiji anafundisha Kiswa..

Hao wenzetu wanakipenda Kiswahili. Sisi hatutaki hata kuwasoma akina Ben Mtobwa, Jackson Kalindimya, Edwin Semzaba na wenzao, kwa kuwa riwaya zao ni za Kiswahili. Wala hatuna mpango na akina Shaaban Robert, Saadan Kandoro, Moh'd Seif Khatib, Sudi Andanenga, na kizazi kipya kina Fadhy Mtanga, kwa kuwa tu mashairi yao ni ya Kiswahili.

Hata filamu zetu tunataka tuzungumze Kizungu kwa kuwa tunaona Kiswahili 'haukamu'

Ahsante kaka kwa kuniambia umepata muda wa kusikiliza muziki wa Kiswahili.

Titi la mama li tamu, chambilecho Shaaban Robert.

Albert Kissima said...

Tungo kuwa tata nionavyo mimi, hutegemea na mtu mwenyewe, kwamba tungo husika anaifahamu kwa namna ngapi tofauti.

Kwa mfano, tungo ulizoziweka bayana ambazo zinahisiwa kuwa na utata wa tafsiri, wapo ambao wanafahamu maana moja tu kwa kila tungo kutegemea na mazingira waliyokulia kwani ni lazima tafsiri itokane na kitu ambacho tayari kipo/kimeshajengeka akilini (yani uhusishaji wa mambo). Kijana wa mtaani aliyezoea maneno ya mtaani yasiyo rasmi mathalani, ana nafasi kubwa sana ya kutafsiri tungo hizi kwa uhalisia wake kama maneno ya kawaida ya kiswahili na pia kwa tafsiri nyingine ya maneno ya mtaani.


Tungo kama hizi binafsi naona ni kipimo kizuri cha namna ya kugundua upotoshaji wa maneno ya kiswahili au niseme inapima kiwango ambacho lugha imeathiriwa na baadhi ya watumiaji na pia tungo hizi zinatoa picha ya tabia, mienendo, mitizamo na uhalisia wa maisha ya watumiaji wa lugha husika.

Bila shaka watunzi wa tungo ulizozitolea mfano, nao kwa namna moja ama nyingine hawakuzitumia tungo hizi accidentally, walikuwa na sababu. Pengine kwa tafsiri zao waligundua kuwa zilikuwa na maana tofauti, au walitaka kuonyesha namna nzuri ya utumiaji wa tungo hizi baada ya kusikia baadhi ya watu wakizitumia vibaya n.k Lengo hasa wanalijua wao wenyewe.

nyahbingi worrior. said...

amani iwe nawe kaka.

mdoti Com-kom said...

Kaka nimerudi. Tafadhali pitia kijiwe changu ninujumbe mzito. Uwezo wa kufikiri huonekana katika mawazo uyatoayo, kufikiri vizuri kunategemea lugha uitumiayo, na kuelewa vizuri kunategemea mtazamo wako. wkibezao kiswahili ni wale waliowatumwa wa ugeni (uingereza) wasiokubali kuwa huru, hata baada ya desemba 9, 1961. na ndio maana wanashindwa kujitambua kwa kuwa wanfikiri kwa lugha isiyoyao.
uswahili umeunganishwa na mabo yasiyomema siku hizi, mtu akifanya jambo lisilo kubalika sana huitwa mswahili, akidanaganya huitwa mswahili na pia watu husewa " acha uswahili. waswahili ni watu wanaodhaniwa kuwa sio wastaarabu je twawezaje kuondoa dhana hii!

Maisara Wastara said...

mie ni mgeni hapa..........

chib said...

Jumapili hii imekuwa nzuri sana kwangu kwa kusoma na kupata burudani humu ndani ya PROBLEMEEEE

Mzee wa Changamoto said...

Duh!! Sijui nisingewaza ningefunzwa nini? Kaka Fadhy UMENENA tunavyojikimbia wenyewe. Nimekuwa nikisema mara kwa mara kuwa tunakimbia ambako hatuwezi kufika kirahisi ilhali tunavunja kila daraja tuvukalo. Matokeo yake ni kuwa HATUJAFIKA NA PENGINE HATUTAFIKA na HATUWEZI KURUDI.
Twawa kama mihogo iliyopikwa na isiive.
INASIKITISHA.
Kaka ALBERT.
Heshima kwako Kaka. Ni zaidi ya elimu uliyoitoa hapo. Mchanganuo wako umenielimisha zaidi ya nilivyokuwa naelewa na nashukuru kuwa kila ujapo, waja na uelimishaji wa haja.
BARAKA KWAKO KAKA NA NAJIVUNIA FIKRA ZAKO.
Kaka NYABHINGI. Karibu tena na tunafurahi kukuona hapa barazani. BARAKA KWAKO
Kaka wa Mdoti, karibu tena. Naelekea kwako kujumuika nawe kama ilivyo ada.
Da Maisara, wewe ni mgeni mwema mwenye kujitambulisha. Karibu saana na twaja kwako.
Ndugu Chib. Burudika saana Kaka. Ni vema na mema kukuona hapa.
BARAKA KWENU NYOTE

Bennet said...

Sina cha kuongezea ila mmenikumbusha nyimbo ya solo thang aliita vina utata, sasa haikujulikana ni vina vya mashairi vyenye utata au vitu anavyoongelea ndio vina utata, ingawa kiukweli vyote vilikuwa na utata

Yasinta Ngonyani said...

Sina la nyongeza kwani waliotanmgulia wamesema yote. Ahsante kwa miziki na misomo hiyo. SITAACHA KUONGEA KISWAHILIB NA PIA KUWAFUNZA WANANGU. naipenda naipenda lugha ya kiswsahili eeehhh. Ama kweli kiswahili kitamu.

Maisara Wastara said...

Jana nilikuwa na haraka yakujitambulisha na sikuwa na nafasi ya kutoa maoni.

Mie ni mpenzi sana wa mduara, Taarab, Vanga, Mdundiko na Mnanda, ingawa huwa na bip nyimbo tofauti tofauti, lakini kwangu mie mduara ndio wenyewe.

Hebu msikilie Omari mkali, huyu kijana anajua kucheza na lugha utadhani Mtu wa Pwani we acha tu>

katika wimbo wa shanuo kuna mahali anasema:

'usigeuke shanuo, kazi zake ni mbli tu, kuchana nywele na kusuka nywele.

Kuna kijana Omari Omari anakuja juu katika fani ya mnanda, naye kuna wimbo wake anasema,

'mbona ng'ombe kanyimwa ndevu lakini mbuzi kapewa'

Kwa kweli hii nayo ni changamoto...