Monday, May 3, 2010

Za Kale vs Maisha ya Sasa.......SOPHIA

Moja ya "jumuiko" la bendi ya Marquis (sina hakika ni wangapi walioshiriki katika muziki huu) lakini kwa mujibu wa Blogu ya WANAMUZIKI TANZANIA, "mwenye nyeusi tupu akiwa na gitaa ni Dekula Kahanga Vumbi, wa pili toka kushoto na suruali nyeusi ni Issa Nundu" Picha@ Wanamuziki Tanzania Blog
Ni wiki iliyopita niliposhiriki mjadala kuhusu KUONGEZEKA KWA TALAKA NCHINI KENYA NA KATIKA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI (dodosa hapa) na katika mjadala huo kuna mengi yalijadiliwa. Na licha ya kuonekana kuwepo kwa sababu nyingi, kilichokuja kuonekana kuwa sababu ya tatizo hilo ni MFUMO MZIMA WA MALEZI.
Na tatizo la talaka kwa nchi zetu za Afrika lazidi kuongezeka kila uchao kwa kuwa wale wanaooa na kuolewa hivi sasa, ni wale ambao HAWAKUANDALIWA kutafuta watu walio makini na sahihi katika mahusiano na pia hawapati msaada wa kukabiliana na misukosuko ya kimahusiano.
Tatizo kuu tulilonalo kwenye suala zima la ndoa ni
1: Hatuelimishw kuhusu changamoto za ndoa, ama
2: Tunaelimishwa kidooogo sana kuhusu changamoto za ndoa, ama / au
3: Tunaelimishwa visivyo kuhusu suala zima la ndoa
Lakini kuna wale wanaopata mafunzo ya ndoa, ila kama nilivyosema, mafunzo haya (ambayo siku hizi ni kwa kina mama zaidi) mara nyingi hutolewa na watu ambao wameachika. Jaribu kufikiri mafunzo kuhusu ndoa toka kwa mtu ambaye ndoa imemshinda.
Lakini hivi sivyo ilivyokuwa miongo kadhaa iliyopita. Licha ya ile tabia ya wazazi kuwachagulia watoto wao mwanamke ama mwanaume wa kuoana naye (tabia ambayo sijawahi kuiunga mkono), lakini pia wazazi walikuwa wakiwafunza watoto ama kuwaasa wale wakaribiao kuingia maisha ya kinyumba kuhusu dunia na suala zima la ndoa. Na hili lilikuwa msaada kwa ndoa nyingi kwani kukumbana na magumu hakukumfanya mhusika kujiona aliye ama mkosi ama mwenye matatizo kuliko wengine.
Na kama tujuavyo, kilichotokea kwenye JAMII zetu, kilielezwa ama kuoneshwa ama kutunziwa kumbukumbu na wanamuziki wetu. Hakukuwa na tofauti katika hili la USIA WA NDOA NA MAISHA KWA UJUMLA.
Sikia wasanii katika wimbo ufuatao wakiasa kuwa hata ukiwa na cheo YAKUPASA KUHESHIMU maoni ya wazazi wako kwani kwa kuwabishia kuna uwezekano wa mambo kutokukuendea vema. Na hapa simaanishi LAANA, bali kwa kuwa wazazi wanaokupenda watakueleza kila wajualo kuhusu maisha, na kwa wewe kutotenga muda wa kuwasikiliza, kuna uwezekano wa kukosa yale ambayo unaweza kuyaepuka kutokana na makosa ama ujasiri wao.
Ni katika kuoanisha nyimbo hizi na maisha haya ya sasa na hasa suala hili la Maisha, Ndoa na Talaka, tunakutana na Marquiz du Zaire wana Zembwela katika wimbo SOPHIA. Kwa mujibu wa Uncle Dekula "Vumbi" Kahanga (msome hapa) (niliyemuomba orodha ya walioshiriki katika wimbo huu) "wimbo wa Sophia ulitungwa na Nguza Viking na yeye ndiye alipiga Gitaa la Solo,waimbaji walikua,Kasaloo Kyanga,Mutombo Audax,trombone ilipulizwa na Berry Kankonde,tarumbeta zilipulizwa na Kaumba na Bizos,Sax ni King Maluu"
Burudika ukielimika.

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mitandao shirika hapa** . Ama ili kuweza kujua tasnia nzima ya muziki na wanamuziki wa Tanzania BOFYA HAPA

4 comments:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

kuhusu ndoa kufunzwa na walioachika, kuna msemo wa kihaya usemao "otalishwera muala wa kyelimiile""

mtwiba utatafisiri zaidi

Masangu Matondo Nzuzullima said...

Msemo wangu wa Kihaya niupendao sana (nilifundishwa na mwisiki mmoja kule Kahororo) miaka ile ya neema ni huu:

"Ebigambo bingi bikatanga enkoko okwikukusa"

Mtwiba pia atatafsiri zaidi; na samahani kwa kutoka nje ya mada!

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

@matondo, DUH, labda kazi kwa mtwiba

Anonymous said...

Naona Mtwiba amewaignoa. Duh, inauma eeh???