Tuesday, July 27, 2010

Miaka 9 baada ya wimbo wake........ JAMII IKO PALE PALE

Ulipotoka kwa mara ya kwanza niliufurahia kwa kuwa ulikuwa ukifurahisha. Kisha nikausikiliza tena na tena na kuangalia hali halisi ya jamii yetu. Na kwa kuwa ilikuwa ni mwaka mmoja tu baada ya uchaguzi, wengi waliuchukulia kama kibwagizo cha kusindikiza kile kilichotokea 2001. LAKINI SI KWELI.
Aliimba kile ambacho kilikuwa, kimekuwa na nategemea kuwa KITAENDELEA KUWA TATIZO katika suala zima la mchakato wa maendeleo yetu waTanzania kwa kuwa tunapuuza ilipo asili ya mchakato huo ambapo ni kwenye uchaguzi. Ikiwa ni miaka 9 sasa tangu msanii Joseph Haule atoe wimbo wake aliouita NDIO MZEE ambao ulipatikana katika albamu ya MACHOZI, JASHO NA DAMU, bado jamii ya Tanzania inaendelea kuishi katika matatizo na kupitia katika hali mbaya ya kimaisha kana kwamba hakuna ambaye ameshaliona, kulionya na kueleza namna ya kutatua jamii.
Wimbo huu ambao umeeleza kwa namna ya USAHIHI maongezi na ahadi nyingi zisizotimilika za wanasiasa na maitikio ya wananchi yasiyojali kusikia kisemwacho na mwanasiasa huyo, unaonekana kupuuzwa hata sasa ambako UONGO huu umeanza kushamiri tunapoelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Wimbo wake huu kwa kiasi kikubwa umezungumzia namna ambavyo waTanzania wengi HAWAJUI KILE WAHITAJICHO na matokeo yake kupokea kila kisemwacho ama kutamkwa na "mzee" ambaye anaaminika kiasi kwamba kila asemacho wao wanakubali. Sina hakika kama mmesikia nililolisoma kwa Dadangu Subi kule fesibuku kuhusu "Mgombea mmoja wa Ubunge kwa tiketi ya CCM huko Iringa anasema akipata Ubunge atawanunulia wananchi nyavu za kuvulia samaki il hali eneo hilo ni la mwinuko na milimani kusikokuwa hata na mto, wachilia mbali ziwa au bahari!" Ninaloweza kufikiria ni namna ambavyo wananchi walivyoshangilia na kuona kama shida zao zimekwisha ilhali wanasahau kuwa hazitakwisha kwani hazipo.
Na sasa ni mwaka mwingine wa UCHAGUZI. Mwaka ambao kila mtu anakuwa muongeaji na kila mmoja ni mzalendo. Kila mtu anaipenda nchi na kuja na sera zake "disposable" na watu bila kujua wataendelea kuimba NDIO MZEE.
Natamani kama wagombea wangekuwa wanasema kile walicho na uwezo.
Natamani kama wananchi wangekuwa wanauliza na kujiuliza yale wapasayo kujiuliza./
Natamani kama waandishi wangetanguliza mbele taaluma na kuhoji kisemwacho kuliko kuripoti
Natamani kama kungekuwa na utaratibu wa kutunza rekodi ya kisemwacho na kuhakikisha mwisho wa muhula waliosema "wanarejesha hesabu"
Natamani tusingekuwa tunachagua viongozi ambao meisho wamuhula ndio wanatuambia kuwa walitumia muhula huo KUJIFUNZA WANACHOHITAJI KUFANYA na bado hakuna anayewawajibisha kwa kuahidi wasichoweza
Natamani kama safari hii wagombeao wangetueleza ambavyo wamefanya katika miaka 5 iliyopita na namna ambavyo wanaamini uwepo wao katika nafasi wanazogombea unavyoweza kuleta mabadiliko endelevu.
NATAMANI KAMA MWAKA HUU, WANANCHI WASINGEKUWA WAITIKIAJI WA KILE KITIKIO CHA NDIO MZEE
Joseph Haule ama Prof Jay akishirikiana na Lady Jay Dee, Babu Ayubu na Juma Nature wameweza kueleza kwa namna ya pekee ambavyo jamii imekuwa "waitikiaji" wasiofikiri.
Albamu hii ya MACHOZI JASHO NA DAMU (ambayo binafsi naamini kuwa moja ya albamu bora zaidi kupata kutoka katika muziki huu nchini Tanzania) imesheheni mengi, imeonesha ujuzi na utambuzi wa Prof Jay na kuiainishia jamii mengi ambayo miaka 9 baadae, hakuna mabadiliko. Ni uwezo huu ulio/ unaomfanya Prof Jay kukubalika ndani na nje ya nchi (kwa jamii zisikiazo kiSwahili) na pia kumuwezesha kupata tuzo nyingi tu.Picha kwa hisani ya Bongo Star Link Blog<>
Naomba USIKILIZE KWA MAKINI kibao hiki NDIO MZEE na tafakari kuleee jamii yetu ielekeako sasa hasa wakati huu wa uchaguzi

TUONANE "Next Ijayo"
Uchaguzi Tanzania ni "label" inayozungumzia namna niionavyo nchi yangu ya Tanzania ijiandaavyo na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010. Kwa maandishi mengine juu ya mada hii katika "label" hii BOFYA HAPA

Uchaguzi Tanzania ni "label" inayozungumzia namna niionavyo nchi yangu ya Tanzania ijiandaavyo na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010. Kwa maandishi mengine juu ya mada hii katika "label" hii BOFYA HAPA

2 comments:

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

na baada ya uchaguzi pengine mambo yatabaki vile vile :-(

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

nikiangalia kuwa wewe unaitwa mzee wa changamoto na nikikubaliana na mengi ya uliyoyasema namimi naugana na kuendelea na kibwagizo au kuitika tu; 'NDIYO MUZEHE'