Kundi zima la Morgan Heritage liundwalo na ndugu watano.
Ni siku 5 tu zimepita tangu kumalizika kwa michuano ya soka ya Kombe la Dunia ambayo ilifanyika na kufana huko nchini Afrika ya Kusini. Na kumalizika kwa michuano hiyo kwa baadhi ya "wafaidi kuangalia" kunamaanisha kuwa ni mwisho wa mchakato mzima na sasa wanasubiri "kufaidi" mwaka 2014. Lakini kwa waliokuwa wamewekeza na kuhitaji matokeo yaliyo sahihi, WAMEFANYIA KAZI MATOKEO YOTE.
Kwa waliopoteza mechi kizembe ama kijinga wamewajibishwa. Ina maana Makocha, Wachezaji ama Viongozi vya vyama ama mashirikisho ya soka nchini mwao wamewajibishwa kwa adhabu mbalimbali. Wengine kwa hiari yao wenyewe wakaamua kumwaga manyanga.
Lengo hapa ni KUJIPANGA KWA AJILI YA MICHUANO IJAYO NA KUANGALIA UWEZEKANO WA KUKAMILISHA DHAMIRA NA MALENGO YA NCHI KULITWAA KOMBE HILO
Ninatamani saana kama uwajibishaji wa namna hii ungekuwa unatokea kwenye maisha yetu ya kila siku. Maisha ya kisiasa na kitawala nchini Tanzania. Yaani tunapoelekea mwisho wa "kombe la urais na ubunge", tuangalie ni nani na nani wamefanya nini. Kisha tuangalie kama kuna anayestahili kuwajibishwa. Tuangalie ni "timu gani" tunayohitaji kuwa nayo ili kutuwezesha kulitwaa KOMBE LA MAENDELEO kwa wananchi katika fainali zianzazo mwishoni mwa mwaka huu mpaka mwaka 2015.
Kwa wale ambao hawakuwa na msaada kwetu, walioshindwa kutumia rasilimali zilizopo, walioshindwa kuhimiza nguvukazi kuendeleza maeneo watokako, waliohamia nje ya majimbo yao na kuendekeza biashara na kujirundikia pesa, wasiotetea wananchi wao na ambao kwa namna moja ama nyingine wameshindwa kutekeleza kile walichoahidi kukifanya mwaka 2005, TUWAENGUE.
Lakini pia tukumbuke kuwa kumekuwa na mengi ya kukwamisha mambo kutimia, lakini cha kuangalia ni namna gani wamejitahidi kutimiza malengo na ni kwa kiasi gani mambo yaliyo nje ya uwezo wao (kama mtikisiko wa uchumi uliokumba dunia) vimechangia kuwakwamisha.
Kwa ujumla tuwe makini katika kuchagua. Tujiulize waliyojiuliza MORGAN HERITAGE katika wimbo wao POLITICIAN waliposema "why should we trust in politicians, and why should we vote every elections. When there's no place for we (you and me) in their secret society. They call us minorities".
Hakuna haja ya kuendelea kuchagua uozo ambao unaendelea kututafuna na kutumalizia maliasili. Wenye kuongeza gharama za malipo na posho ilhali hawana suluhisho lolote katika kutatua matatizo ambayo WAMEYAONA, WAMEYAKIRI, WAMEYATANABAISHA KUWA YANATATULIKA NA KIKUBWA ZAIDI WAMEAHIDI KUYATATUA
Nikiwa na kiongozi wa uimbaji (lead singer) wa kundi hilo Peter Morgan (2008)
Sikiliza kibao chao hiki POLITICIAN kilichomo kwenye albamu yao MISSION IN PROGRESS uburudike na kujifunza pia.
**Them, I & Them ni kipengele kikujiacho kila Ijumaa kinachoelezea kazi za wasanii (Them) kulingana na maono yangu (I) kwa ajili na manufaa ya hadhira (Them)**
Kwa nyimbo zaidi ndani ya kipengele hiki bofya hapa.
IJUMAA NJEMA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
2 comments:
Baadhi yaTanzania tunachukulia uchaguzi ni sehemu ya ulaji, wengi wetu hatuweki umakini kwenye kumchagua kiongozi bora, tunachukulia ni utaratibu tu,tunapiga kura kwa ushabiki, tunafuata mkumbo, na kingine, uelewa wa siasa hatuna.
Watanzania tunavyo vigezo vitakavyotusaidia kumjua kiongozi bora na asiye bora?tunajua undani wa vigezo hivyo ili tusidanganywe?
Naamini kwa sisi kujua siasa ya nchi, historia ya nchi, taifa limepitia wapi hadi kufika hapa lilipo ni miangoni mwa vigezo, je, ni wananchi wangapi tuijuayo historia ya nchi ipasavyo? Mgombea akija na kuanza kueleza kuhusu nchi, ilikotoka hadi ilipo na anataka kuipeleka wapi, hatutabaki kushabikia tu?
Kwa kweli elimu yetu haituandai ipasavyo ktk siasa, tunabaki kuwa washabiki tu. Uwekezaji ktk elimu ya uraia ni muhimu sana kama msingi wa kuchagua viongozi bora. Mwanafunzi wa chuo kikuu, anashangaa anapoambiwa kuwa jeshi la Tanzania liliwahi kuasi mara mbili, ajabu mtu huyo kasoma Historia kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu.
Mzee wa changamoto, ninafarijika sana kusoma hii michango yako hapa inayoelezea machungu uliyonayo juu ya siasa chafu ya chama tawala, siasa ambayo imeshindwa kukwamu wananchi walio wengi kwenye wimbi la umasikini.
Kilichoniacha mdomo wazi ni kitendo cha TBC kutangaza live hadi kwenye mitandao mkutano wa CCM uliofanya Dodoma hivi karibuni, ambapo Rais aliwateka kwa njaa zao wasomi wetu wa chuo kikuu, wanamziki wa kizazi kipya na hao wanafiki wanaofungua matawi ya CCM Uingereza, Italy, India n.k
Nilijaribu kuchangia kwenye blog ya Michuzi kupinga vitendo wa chama tawala kumwaga hela nyingi kuyateka makundi niliyoyataja hapo juu kwa maslahi ya kujitafutia kura na kula chakushangaza hizo posti zilitupwa kapuni. Roho iliniuma sana. Nasema ipo siku, tusikate tamaa kwani ni mimi na wewe ndio tutakaoleta mapinduzi ya kweli Tanzania.
Post a Comment