Tuesday, August 10, 2010

Miongo 3 ya uhai....Kila mtu na kitu ni shule

"you gotta live to learn, you gotta crash and burn,
you gotta make some stances and take some chances,
you gotta live and love and take all life has to give
you gotta live and learn so you can learn to live"
Darius Rucker


Nilipozaliwa tu nikaanza kuwaza. Na mpaka sasa ninawaza. Nawaza kwa sauti.
Ni kweli kuwa leo ni mwaka mpya kwangu. Tarehe kama hii miongo 3 iliyopita katika hospitali ya Brackenridge, Austin TX, ndiyo nilizaliwa. Nikiwa mtoto wa tatu wa familia ya watano wa Mr na Mrs S. Bandio.
Maishani nimebarikiwa kupitia ngazi nyingi. Za kulazimika na hiari. Zenye kuona mambo na kuoneshwa na namshukuru Mungu kuwa katika hayo yote, bado kulikuwa na nafasi ya pili ya kuweza kuyarejea yale niliyokosea na pia kurekebisha na kuboresha niliyotenda vema.
Nikiwa "bwa'mdogo", nilikuwa napenda vitu vingi na nilikuwa na ndoto nyingi. Lakini kama wengi tujuavyo, mazingira ya maisha ya nyumbani (na hasa zaidi ya miaka 10 ama 15 nyuma) hayakutoa nafasi kubwa kwa wengi wetu kutambua na kuendeleza kile tulichopenda. Ilikuwa ni kusoma na kusomeshwa (labda niseme kukaririshwa) kisha utaambiwa ni nini kinakufaa kulingana na matokeo yanayotokana na mitihani ambayo ufaulu wake ungetokana na ufundishaji uliopata na pengine mazingira uliyokulia.
Hivi hujajiuliza kuwa "kama kweli uhandisi ama udaktari ama fani yoyote ya 'kisasa' si kitu cha kuzaliwa nacho, kwanini ndugu zangu wa Rubafu ama Nangurukulu ama Kasulu ya ndani ama Nanjilinji hawafiki huko?"
MAZINGIRA.
Anyway!!!!!!!
Ina maana kuna wengi walioangukia ualimu kwa kuwa "combi" za O-level ziligoma nawengine kuelekea "A-Level" kwa kufuata uchaguzi waliofanyiwa kutokana na walivyofunzwa.
Well!! Wacha nirejee kwenye "topiki"
Nilijikuta nikiwa mpeenzi sana wa kazi mbili zisizokuwa na uhusiano (kwa mtazamo wa wakati huo) ambazo ni UFUNDI na UTANGAZAJI. Nikiwa mdogo nilikuwa sikosi kusikiliza na kuchanganua walichosema watangazaji. Na bado nakumbuka kuwa shabiki mkubwa (mpaka sasa) wa Uncle Charles Hilary. Nilipenda kusikiliza alichosema na alivyosema. Matumizi ya lugha na mengine mengi. Pia kulikuwa na Uncle J Nyaisangah ambaye alikuwa akinifanya nihisi jengo la utangazaji ni kuuubwa kiasi kwamba bendi zoote zinakaa pale na akiita bendi fulani huanza kupiga muziki. Nilipenda kazi ya kuwa na uwezo wa kuziona bendi zote na kisha ukaamua ni ipi itumbuize wimbo gani na pengine kwa muda gani (kulingana na uamuzo wako na fundi mitambo). Hahahahaaaaaaaaaaaaaaaaa
Lakini pia nilipenda "kuchokonoa". Nilipenda saana kuona kitu kikitengenezwa na kutoka katika ubovu mpaka utendaji kazi. Ni hali hii hii niliyoiona kwa madaktari wanapotibu lakini utabibu haukuwahi kutekenya mfumo wa maamuzi ya tamaa za kazi.
Nikirejea nyumbani, nili/ nimebahatika ama NIMEBARIKIWA kuwa na familia tengefu. IMETENGEMAA kiasi ambacho kwa namna nyingine iliniathiri na kuamini kuwa HAKUNA MIGONGANO KWENYE FAMILIA. Niliamini kilicho kigumu kwenye familia ni kulea maana niliona namna nilivyokuwa "changamoto" kwa wazazi na walezi wangu.
Lakini mara zote walionesha na kuwa mfano wa nini familia yaweza kufanya na kurekebisha mtu kwa upendo hata kama uliambatana na bakora.
NAWASHUKURU KWA HILO.
Maisha yangu ya shule yalianza mapema saana. Nilipojitambua kuwa ni kiumbe, nilikuwa naenda shule. Wazazi wangu walinizoesha ama kunianzisha shule nikiwa mdogo na nilikua nikitambua mfumo wa kuamka kwenda shule na kurejea nyumbani kuendelea na kazi za nyumbani
Malezi ya nyumbani nayo. Hahahahahaaaaaaaaaa. Kwa akili za wakati huo sikuona kama yanafaa. Sasa hivi wala siwezi kubadilisha kwa lolote. Nyumbani tulifunzwa kila kazi iendanayo na umri wako. Ungejua kufua muda ukifika, kupika na kusafisha, kupanga na kupangua. Yaani tulijikuta tukitambua namna ambavyo vitu vyawa vilivyo na hilo lilinifanya kuthamini kila "kidogo" kitendwacho" maana nilijua "shughuli yake".
Baada ya miaka 18 na wazazi, nikaachana nao na kuanza maisha ya ndugu, jamaa na marafiki. Nikiwa na Dada zangu na walezi kama Mama na Baba wadogo, Shangazi na Wajomba, Shemeji na Kaka na Dada na wengineo.
Hapa napo si padogo. Niliendelea KUJIFUNZA maisha ya kuwa mbali na wazazi (ambao kwa namna fulani wana wajibu wa lazima wa malezi kwako) na kuanza kukua na kutambua kuwa naishi na walio na wajibu wab hiari maishani mwangu
Nikaenda chuo ambako nako nikakutana na wenzangu ambao nao wakajenga sehemu kuu ya maisha. Na baada ya chuo nikarejea kusaka maisha na kisha KAZI.
Huko nako nikakutana na watu wa tofauti, wenye makuzi, mila, desturi na mitazamo tofauti.Nako nikafunzwa.
Lakini maisha hayajawahi kuwa na mwisho na wala hayaonekani kuwa na mwisho wa kujifunza. Nimekuwa nikikutana na watu wa aina mbalimbali, katika mazingira mbalimbali na kwa namna mbalimbali. Nimeonana na kuwasiliana na watu na pia nimetambulishwa na kutambulisha watu. JAMBO MOJA NINALOMSHUKURU MUNGU ni kuwa katika kila nikutanaye naye, NAJIFUNZA
Kila mtu kwa namna ambavyo amekuwa mbele yangu amekuwa DARASA tosha kutambua ambalo sikulijua.
Kila kitu ambacho nimetenda ama kutendewa kimekuwa darasa tosha kwa maisha niliyopo na yajayo.
Nikisema nianze kutaja kila aliyenibariki katika miongo hii mitatu iliyopita, sitaweza lakini hii haimaanishi kuwa sitataja wachache kwa majina na wengi kwa mjumuisho.
Wazazi wangu wapendwa, Kaka na Dada zangu. Natambua kuwa ninyi ndio mliojenga MSINGI wa maisha yangu.
Walezi wangu ambao niliachwa nao wazazi walipokuwa kazini na wale walionilea nilipotoka kwa wazazi, ninyi mlipalilia pando la wazazi.
Marafiki na wale wajihesabio kuwa maadui. Ninyi mmenifunza kwa njia iliyonifaa na nawashukuru mno.
Kipekee napenda kumshukuru Da mdogo RENATHA BENEDICTO ambaye bado namtafuta na naendelea kuomba msaada wa waungwana kuniwezesha kuniunganisha naye.
Kwa sasa sina budi kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mke wangu mpeeenzi Esther na binti yetu Paulina. Ninyi mmekuwa kama STRESS-BUSTERS wa maisha haya magumu. Mmekuwa yeyusho la kero na hasira za wengine juu yangu na kuwa msingi na mhimili wa pale nitelezapo.
NAWAPENDA NA KUWAHESHIMU MNO
Kwa yeyote na chochote nilichokutana nacho maishani kwangu, na ambacho kimekuwa shule na makuzo yangu.
NAWAPENDA SAAAANA
Ni mwaka mpya kwangu, ni muongo mwingine maishani mwangu, na kila mtu niliyekutana naye na kila kitu nilichokutana nacho NIMEJIFUNZA, na kwa kila nitakayekutana naye na kila nitakachokutana nacho, NITAENDELEA KUJIFUNZA.
Baraka kwenu nyote

17 comments:

emu-three said...

Happy birthday mkuu, na historia yakoo imenivutia sana.Mungu akujalia afya na uzima

Fadhy Mtanga said...

Heri ya siku ya kuzaliwa kaka. Nakutakia baraka tele wewe na familia yako kwa ujumla.

Fadhy Mtanga said...

Heri ya siku ya kuzaliwa kaka. Nakutakia baraka tele wewe na familia yako kwa ujumla.

Baraka Mfunguo said...

Did not think it was your birthday. Is what? Oh Happy Birthday Man and congratulations. Tuko Pamoja sana Mkuu.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

hongera, yangu ilipita kimya kimya mwaka huu niliona nisherehekeee ya bwana mdogo pekee

malkiory said...

Ndugu Mubelwa, nakutakia heri, afya na fanaka tele katika siku yako hii ya kuzaliwa. Nakuombea kwa mola ili akujaza nguvu ya kuweza kuielimisha jamii yetu hasa katika kipindi hiki kigumu cha uchaguzi mkuu. Cheers!

Faith S Hilary said...

Happy Birthday dear!!! Make this day count out of all days of the year! God Bless youuuuuu! Mch luv! xx

PS: Dad says happy birthday ;)

Egidio Ndabagoye said...

Heri siku yako ya kuzaliwa

EDWIN NDAKI (EDO) said...

Nakutakia kila jema ktk mchakato wa maisha..happy birthday

mumyhery said...

happy birthday Mubelwa, Munugu akujalie maisha marefu yenye furaha na afya tele

EDNA said...

Heri ya siku ya kuzaliwa kaka,nakutakia kila lililo jema katika maisha yako pamoja na familia yako,najivunia kukufahamu May god Bless you.

Yasinta Ngonyani said...

Siku bado hajaisha nami ngoja nivunje sheria ya likizo na kukutakia siku hii tukufu. Hri sana kwa siku hii ya kuzaliwa na Mwenyezi Mungu awe nawe pia familia yako akupe nguvu mpya za kuitunza familia yako.

PS: Familia yangu inakupa pia HERI NYINGI SANA. HONGERA.

Mija Shija Sayi said...

Hongera mwanakwetu. Miaka 30 si michache. Hongera sana kaka Bandio.

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Mwanablogu makini, mchambuzi yakinifu, mtoa hoja thabiti......

Mubelwa;

Wewe ni uthibitisho halisi wa ile methali ya Kinaijeria isemayo kwamba "hekima haipatikani katika mvi tu"

Nakutakia miongo mingine mingi mizuri huko mbeleni. Hongera kwako pamoja na familia yako.

HAPPY BIRTHDAY!!!

PASSION4FASHION.TZ said...

Happy birthday kaka Bandio,hongera sana kwakuweza kuifikia tena siku kama hii ya leo,mungu azidi kukupa afya njema na busara zaidi uzidi kutuelimisha.

Christian Bwaya said...

Heri ya kuzaliwa! Nina hakika kama usingezaliwa, yapo mengi tu nisingeyajua!

Jeff Msangi said...

Happy Birthday kaka.As a friend,fellow blogger,I feel blessed to have you around.I admire your thoughts,understand and share your frustrations and walk in the same path with you in believing tomorrow can and will be better.We can make it better.We just need to Keep On Moving just as Legend Bob Marley told The Wailers just a day before he passed away.We have to.