Monday, September 20, 2010

Kabla hatujapata Rais wa upinzani, .............

Photo Credit: Matondo Blog
"why should we trust in politicians, and why should we vote every elections. When there's no place for we (you and me) in their secret society. They call us minorities".Morgan Heritage
Najua kuwa "MAENDELEO NI LAZIMA YAENDANE NA MABADILIKO" lakini pia najua kuwa "MABADILIKO SI LAZIMA YAMAANISHE MAENDELEO". Na hili ni kati ya yale ambayo ningependa wengi wayatambue na kuyajadili.
Kwani tunalotaka hasa nchini Tanzania ni nini? MAENDELEO ama MABADILIKO?
Labda twataka YOTE lakini ni lazima kuangalia kile ambacho kwa kuwa nacho, kitamaanisha kingine. Nacho ni MAENDELEO.
Sasa ni wakati wa kampeni za UCHAGUZI MKUU nchini mwetu na kwa bahati mbaya, naona kashfa na habari za maisha binafsi ya wagombea yakichukua nafasi ya MIPANGO, MALENGO NA MIKAKATI ya kuikomboa jamii yetu ambayo ikingali nyuma saana katika maendeleo.
Labda si tatizo la wagombea bali ni "waripoti" wajiitao waandishi ambao wananogewa na kashfa na udaku hata kwenye kampeni. Lakini pia, kwani wanaopiga kampeni na ambao ndio "wanaowakaribisha" waripoti hao, si wana kamati mbalimbali zikiwemo zile zinazoshughulikia UHABARISHAJI? Nao hawaoni kuwa kampeni zao zinajazwa udaku kuliko mahitaji ya waTanzania?.
Lakini pia naona HARAKATI kuu za watu wengi (hasa vijana) kushiriki katika kugombea nafasi mpya.
Labda ni mchakato wa kijamii kuliko wa kisiasa ambao unaamini kuwa "ili kubadili maisha na jamii yetu, ni lazima kubadili wale wanaofanya maamuzi katika vyombo vya kimaamuzi ambavyo ni vya kisiasa". Tatizo ninaloona hapa ni kuwa TUNATAKA KUBADILI WATU WASIOFANYA KAZI KWA UFANISI NA KUWEKA WATU WALIOLELEWA NA KUAMINI KATIKA MFUMO HUOHUO WA KUTOFANYA KAZI KWA UFANISI"
Binafsi naamini TWAHITAJI MABADILIKO ambayo ni pamoja na kuwa na viongozi tofauti toka vyama tofauti kwa ajili ya kutupa HARAKATI TOFAUTI za kusaka maendeleo ya nchi yetu. Kwa ufupi, ningependa kuona nchi yangu ikipata UONGOZI WA UPINZANI, lakini kabla hatujapata Rais / kiongozi wa upinzani......
1: Ningependa kujua wamejipanga vipi kuboresha utendaji wa haki na usawa kuanzia ngazi za kaya? Narejea msemo niliowahi andika mara kadhaa na nitauunganisha na maandishi yangu nitakapokuwa nakamilisha hili, kwamba, "japo moja ya dalili za upungufu wa maji ni majani kunyauka, lakini kutatua tatizo hilo hatuhitaji kumwagilia majani, bali mizizi."
2: Ningependa kujua wana msingi gani wa UAMINI na UTEKELEZAJI wa ilani mbalimbali kuanzia ngazi za kaya?
Hapa wacha niwarejeshe kwa Kaka Kenedy Kimaro wa Habari ni Habari Blog atuunganishaye saana na video za nyumbani kisha ujiulize kuwa ni "wabunge" wangapi wanajua nini cha kufanya kuwezesha maendeleo ya mahala watakapoongoza iwapo wao na mgombea wao wa urais watashinda?
Tazama na sikiliza mdahalo huu mfupi hapa chini kuangalia kama wote (maana naona mmoja yuko makini) wanaendana na kampeni za "wakubwa" wao

3: Bado sijajua ni vipi wagombea wa UPINZANI walifikia maamuzi ya kuwepo katika nafasi ya u-rais. Bado naamini kuwa wangezunguka nchi nzima wakipiga kampezi za watu kuchagua wabunge wa upinzani ambao wangeingia bungeni kwa idadi kubwa zaidi na kuwa "mchachafyo" wa kuondoa KUBEBANA tunakoona kunafanywa na hawa wana-CCM ambao wanaogopa hata kusema kile kiwakeracho..
MASWALI YANIFANYAYO KUWAZA NIVI NI KUWA
(i): kwani hata mmoja wa wagombea wa upinzani AKISHINDA LEO WAKATI 90% YA WABUNGE NI WANA-CCM, UNADHANI ATAMUADHIBU NANI? ATATUMIA KURA GANI AMA SHERIA GANI ISIYOPITA BUNGENI KUWAADHIBU ALIOSEMA WANAIIBIA SERIKALI NA WANANCHI?
Pengine ni wakati wa sasa watu kutambua kuwa tunahitaji miaka 5 ijayo kujijenga katika ngazi muhimu za chini kabla ya kuanza omba ngazi za juu.
*Hivi nchi hata iongozwe na MASIA anayetawala ki-demokrasia, unadhani itafanikiwa kama asilimia 98 ya watendaji ni WAPINZANI WAKE tena wasiopenda kuona anafanikiwa?
Nadhani wanachotakiwa kufanya (wagombea wa urais kwa tiketi ya upinzani) ni kuachana na nafasi ya uRais japo kwa msimu mmoja, kisha kutumia misingi waliyonayo, rasilimali na hata ilani zao kuzunguka nchini bila kuchoka kujenga ubora wa vyama katika ngazi za chini (kaya, kijiji, tarafa, wilaya mpaka mkoa).

LAKINI huyu ni mimi awazaye. Mwananchi tuu muwaza kwa ndani na ambaye NINATUNZA HAKI YA KUKOSEA NA KUKOSOLEWA.
Ni kwa mtazamo huu, ninaamini bado hatujawa tayari kumpokea rais toka chama cha upinzani, kama kama ambavyo nimekuwa nikisema, "japo moja ya dalili za upungufu wa maji ni majani kunyauka, lakini kutatua tatizo hilo hatuhitaji kumwagilia majani, bali mizizi." Na mizizi ya utawala wa kisiasa ni ngazi za kaya, kijiji, kata, tarafa, wilaya mpaka mkoa.
Kwa maana nyingine, japo naamini serikali ya Rais Kikwete haijafanya ambayo ingeweza kufanya (kwa kutumia rasilimali zilizopo na kwa kuwa mamini na wanaozisimamia, bado wa kumuondoa si Kikwete, bali wale wanaomfanya awe alivyo.
NAWAZA KWA SAUTI TUUUU!!!!!!!

Uchaguzi Tanzania ni "label" inayozungumzia namna niionavyo nchi yangu ya Tanzania ijiandaavyo na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010. Kwa maandishi mengine juu ya mada hii katika "label" hii BOFYA HAPA

5 comments:

Fadhy Mtanga said...

Kaka nami unanifanya niwaze kwa sauti kuu alfajiri yote hii. Unaweza ukajiapiza kabisa kuwa wewe na siasa ni mbali mbali kabisa. Lakini si punde, unagundua huwezi kwepa kujadili mfumo unaogusa mustakabali wa maisha yako.

Mwaka 1997, wakati wa ziara yake hapa nchini, Lucky Dube akihojiwa na bi Rahma Aziz wa DTV (ama CTN sikumbuki vema) alisema anachukia siasa kwa kuwa inawagawa watu.

Kipindi hiki cha kampeni tunaona mambo mengi. Lakini lipo la msingi zaidi. Nalo ni maisha yetu kwa ujumla wetu.

Kwa upande wangu, mie sikishabikii chama chochote mwaka huu. Ila nashabikia mabadiliko. Mabadiliko sidhani ni lazima CCM kuondoka na Chadema kuingia. Lakini mabadiliko si kwa CCM kubaki madarakani. Kwa mtazamo wangu, mabadiliko ni namna ya kuwaongoza watu na kusimamia vema rasilimali za taifa.

Nilichojifunza, wengi tunayaogopa mabadiliko si kwa kuwa hatuyahitaji. La hasha. Ila kwa kuwa tunazijua vema gharama za mabadiliko. Mabadiliko yana gharama kubwa sana. Ukiitazama Zambia ilivyoporomoka kiuchumi kwa kasi ya ajabu toka 1992, utaelewa nasema nini.

Tunaogopa gharama za mabadiliko. Hatupo tayari kuzibeba sisi. Ngoja tuwaachie kizazi kingine waje wazibebe wao ili sisi tukwepe lawama tuliiharibu Tanzania.

Lakini tusipofanya mabadiliko, haimaanishi tupo salama. Tukiitazama Zimbabwe ambayo haijawahi kubadili chama kinachotawala, tunaweza kufahamu nini maana yake.

Mabadiliko.

Mabadiliko si jambo linalokwepeka. Kama si leo, basi kesho. Kesho kutwa. Mtondo na mtondogoo. Ila lazima yatakuja tu. Yatakuwa na gharama gani? Watakao yaleta watazijua gharama zake.

Jana mtu aliniandikia sms, akaniambia nani alifahamu kuwa utumwa ungefikia mwisho? Akanifikirisha sana kuhusu mambo mengi ambayo awali ilidhaniwa yasingewezekana.

Nimekwenda nje ya mada yako kaka Mubelwa. Lakini sote tunajadili mustakabali wa taifa kwa kupitia uchaguzi.

Kwangu sijali nani ama chama gani kinatawala Tanzania. Ninachokijali, aliye madarakani anafanya nini.

Lakini sijui kama nami ni mmoja wa wanaogopa gharama za mabadiliko ama lah. Nipo kama sipo. Ila kuna jambo nitalifanya. Nitapiga kura.

Ni hayo tu.

emu-three said...

Huenda `mazoea yana taabu' ndio maana lazima tuone kuwa ili chama kingine kishinde ni lazima kiwe na a to z. Lakini najiuliza je chama ndicho kinatawala serikali au serikali ndio inatawala chama?
Mimi naona kuwa kwa vyovyote ili tuweze ni lazima tujaribu, na tusipojaribu tutajua lini? Kwa mfano wengine wanadai vyama vingine vimefanya nini ili vionekane vinaweza, najiuliza kwa vipi na wakati havipo madarakani?
Sijui labda na mimi ni limbukeni wa siasa, lakini mtizamo wngu upo pale pale kuwa ili kuwe na maendeleo ya dhati lazima kuwe na ushindani, ili kila mmoja akione kile `kiti' cha ikulu, cha ubunge cha udiwani ni `kiti cha moto' kukikalia si rahisi!

John Mwaipopo said...

fadhy you have said it all WITH A LIGHT TOUCH

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

faith umenena na mimi namwambia kijana wa changamoto kuwa haijui siasa ya bongo ya sasa. bado anaaminiCCM iko juu wakati kuna vijana kibao