Saturday, September 4, 2010

Tanzania Yangu....Ihamishayo badala ya kutatua matatizo

News and Photo Credit: Beda Masimbe wa Lukwangule Ent. via Da Subi wa www.wavuti.com
Dar leo imezindua usafiri mpya helikopta ambapo vikwangua anga vya mjini hapo vitatumika kama uwanja mdogo wa ndege, kama ilivyo katika nchi zilizoendelea zenye msongamano mkubwa wa usafiri wa ardhini.
Uzinduzi huo umefanyika hoteli ya Holiday Inn saa 5 asubuhi na kushuhudiwa na waandishi wa habari.
Usafiri huo utatolewa na kampuni ya kukodi ndege ya Everett Aviation.

“Huu ni mlango mzuri wa kuboresha biashara. Tutakuwa tukiwatoa wateja hapa na kuwapeleka maeneo kama Zanzibar, Mtwara na hata Uwanja wa Ndege kama mtu au kampuni itataka kupatiwa huduma hiyo. Wageni watakapokuwa wakiwasili kutakuwa na mawasiliano na mamlaka ya anga hapa nchini, lakini pia hata hapa kwenye hoteli ghorofa ya 11 kutakuwepo na waongoza ndege kutoka kampuni binafsi na wale ambao watakuwa tayari kukabilina na dharura yoyote itakayojitokeza kama ajari au moto, ingawa hilo hatutegemei kutokea,” alisema Meneja Masoko na Mauzo wa hoteli hiyo, Ruan Schreuder.

Schreuder alisema kuwa bado wanafanya mazungumzo na Malaka ya Anga Tanzania ili kupewa kibali cha kutoa huduma hiyo katika paa la hoteli yao na kuwa wanatarajia kuanza kutoa huduma hiyo mwezi Desemba mwaka huu.

YATOKANAYO:
Kuna maswali mengi zaidi ya majibu niwazayo.
Binafsi nawaza kama kuna maandalizi ya kutosha ambayo yamefanywa kabla ya kutangaza na kuzindua hili. Na kama yapo, je yamewashirikisha vipi wananchi ambao iwapo kuna jambo lolote baya litatokea (Mungu aepushe) ndio watakaoathirika na pengine kubaki bila msaada wala kukumbukwa na yeyote?
Najiuliza........
1: Watakaotumia usafiri huu ni kina nani? Labda jibu ni wale wenye uwezo, ambao ndio wenye maamuzi na ambao tumezoea kuona wakipuuzia matatizo mpaka yampate mmoja wao. Si twakumbuka alipouawa askari ama walipopata ajali mawaziri? Tatizo likazungumzwa as if ndio limeanza. Pengine haya "maendeleo" yanatupunguzia nafasi ya kupata suluhisho kwa kuwa wakiwa juu hawatajisumbua kuangalia mchakato ulio chini. Hwatahangaika kujua kinamama wajawazito na walio mahututi wanaopoteza maisha wakiwa kwenye foleni ambazo hazikustahili kuwepo.
2: Hivi hili ni suluhisho la tatizo la barabarani? Kwani zitakuwepo ngapi na "nauli" yake itakuwa kiasi gani? Na zitakuwa zikianzia safari wapi? Mbagala, Gongo a Mboto, Mwenge, Manzese ama?
3: Ni kweli kuwa nusu ama wengi ya wake wanaokwama kwenye daladala wataweza kutumia haya ili kuweka uhuru kwa barabara zetu? Labda wangeleta "version" ya kumbakumba ya helikopta. Na kituo kitakuwa kimoja? Wapi? Mbona maelfu wahangaikao ni wale wa Kariakoo na Kigamboni?
4: Nimekuwa "nikilia" na ajali za barabarani. Wameshindwa kudhibiti za chini, vipi za angani? Wamejizatiti vipi kuhakikisha kila kiendacho angani kiko salama na hakiingiliani na nyingine zilizo juu?
5: Majengo yetu twasikia hali zayo kiujenzi. Je! Yalijengwa kuhimili hizi kashikashi za ziada ama kwa kuwa kuna "access" huko juu basi "twapandishia? Kuna ushahidi wa kitaalamu kuwa majengo husika yataweza kuhimili pilika hizi?
6: Helikopta hizi zitaongozewa wapi? Yaani uongozaji wa helikopta utafanywa na mnara wa Uwanja wa ndege ama la? Na kama sivyo, usalama ukoje kwa helikopta nyingine, ndege na mengine?
7: Bima je? Binafsi tangu nipate ajali mpaka leo miaka 11 iliyopita sikusikia yeyote aliyelipwa japo gharama za matibabu na bima. Tulifuatilia mpaka tukachoka. Na tunajua kinachoendelea watu wanapopata ajali. HAWALIPWI.
Bima za huduma hii zikoje? Tunaweza kuona hatari yake ilivyo.
8: Wahusika wanaweza kuweka bayana namna ambavyo walifikia maamuzi haya? Kuna nyakati nadhani maamuzi makubwa yanayoweza athiri mazingira, afya na hata uhai wa watu yawe yanapita baada ya mjadala bungeni. Hili limetoka wapi na limefikiwa vipi?
Lakini hii ndio Tanzania yangu. Iliyoshindwa kuzuia ajali za barabarani inazoziona na kuzifikia kwa urahisi na sasa inahamisha matatizo angani.
Kumbuka....NAWAZA KWA SAUTI TUUU!!!!!!!!!!!!
Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA

Tuonane "Next Ijayo"

3 comments:

chrischals said...

kaka hapo umenena ipasavyo bt kama ulivyosema itagundulika kuwa wapo wrong ktk hayo maamuz pale mmoja wa anayeandaliwa huo usafiri[watu wenye fweza]atapopata tatizo{siombei hivyo}. Ama kweli nchi yetu haijui kutatua tatizo!

born city said...

Dar ni kweli ina tatizo la msongamano. Ninalolijua ni kuwa master plan ya transport for Dar imeshaandaliwa. Kinachotafutwa ni fedha ili serikali waanze kujenga kwa awamu. Of course itabidi tusubiri ndani ya miaka 2 au 3 hivi.

In the meantime sioni ubaya kuwa na usafiri kama wa chopper. Kumbuka tulikotokea. Enzi za UDA zilikuwa na kero zake baadaye daladala zikaruhusiwa kero haikuisha maana magari yaliongezeka na watu waliongezeka na jiji likawa linakuwa kwa ukubwa. Haya taxi zilikuwepo na polepole taxi bubu. Bado tatizo likawepo. Sasa tumeruhsu bajaj na pikipiki. Swali kuna tatizo gani kuwa na Chopper kama itanifikisha airpot ndani ya dakika 5 mradi niwe tayari kulipia?

Mzee wa Changamoto said...

Kaka Chris, karibu saana Barazani. Naona nawe umejikita kwenye kuangalia na kuchangia. SHUKRANI KAKA NA KARIBU

Ndg yangu BORN CITY.
Unless umebadili jina, hii itakuwa mara ya kwanza kukuona hapa barazani kwenye upande wa maoni. KARIBU SAAANA.
NASHUKURU NA KUHESHIMU mawazo na mchango wako na nafurahia ulivyokubali kutokukubaliana na mtazamo wangu kwa namna ya heshima zaidi.
ASANTE
Kuhusu ninalowaza hapa, kwangu tatizo ni kuwa NI KIPI KINACHOSABABISHA MSONGAMANO WA MAGARI DAR?
Kaa ulivyosema waliweka daladala hazikukidhi, zikaja taxi na taxi bubu, bado yaleyale, kukaja bajaji na bado msongamano uko palepale.
Unadhani tatizo liko wapi?
Kwanza nahisi haya yote si suluhisho. Kuongeza vitembea barabarani wakati hupanui barabara si suluhisho hata. Labda kama ulivyosema kuwa kuna mpango utakaochukua awamu mbili ama tatu. LAKINI NI WANGAPI WANAJUA HILI?
Tuna tatizo kuubwa la uhabarishanaji Tanzania yetu.
Watawala hawaamini kuwa ni haki ya mwananchi kujua habari kama hizi. NAFURAHI KUWA UMELIWEKA HILO BAYANA.
Lakini unadhani helikopta zitasafirisha watu wangapi kwa siku? Na hiyo ni asilimia ngapi ya wakazi wanaohangaika kwenye trafiki ya Dar?
Kama nilivyosema awali. SERIKALI YETU IKO BUSY KUMWAGILIA MAJANI BADALA YA MIZIZI. Hata kama dalili ya ukame yaweza onekana kwenye majani na si mizizi, tiba yake iko kwenye mizizi na si majani
Blessings mankind