Wednesday, September 22, 2010

Tanzania yangu....Inayopuuza HALL OF FAME kutukuza "HALL OF SHAME"

Kama kuna kitu ambacho sisi kama waTanzania tumeweza kudhihirisha ni KUTOTHAMINI WALIOWEKEZA MUDA NA VIPAJI VYAO KATIKA YALE YALIYO MEMA.
Niliwahi andika kuwa Tunawapenda, Hatuwathamini.....Kwa kuwa hatuwajui (irejee hapa). Humu niliandika kuhusu makala niliyoipata na kuisoma kwa Da Subi kuhusu watangazaji wa Radio Tanzania ambao sio tu walitufunza, kutuburudisha na kutuhabarisha, bali pia walikuwa chachu ya watangazaji wengi wachanga ambao sasa hivi wanachukua heshima na "matumizi" yote toka kwa wenye nacho ambao wanawafanya (hawa wachanga na ambao wengi wao hawakidhi viwango vya kazi kimaadili) wawe kama wenye kustahili sifa na heshima zote.
Lakini tukiweka mbali watangazaji, kuna ndugu wengine katika fani kama MUZIKI ambao nao licha ya kutumika kama chombo cha starehe cha serikali (irejee hapa), hawapati heshima yoyote wastahiliyo na huishia katika maisha ambayo ni wenye mamlaka wachache ambao hutumbuizwa nao, huwakumbuka. Niliandika nikiuliza Ni lini tutawaenze watu hawa? (irejee hapa).
Mambo hayajabadilika hata sasa. Na sijajua kama wa kuyabadilisha ni WALIOKO KWENYE "VILELE" VYA FANI ZAO ama SERIKALI?
Ninaloona likisahaulika hapa ni kuwa hata hawa ndugu waigizaji, watangazaji, waimbaji na wasanii wengine ambao sasa wanaelekea "kufaidi" matunda ya kazi zao, hawakumbuki kuwa wakati watakapostaafu, wakati ambao hawatakuwa wakiingiza kipato ka namna waingizayo sasa, wakati ambao wale "wanaowatumia" hawatawahitaji tena, watarejea kwenye KILIO ambacho waliowatangulia wamekuwa wakilia na KUPUUZWA.
Mzee Kipara.
Nyota "aliyezalisha" wasanii wengi maarufu, kuelimisha na kuburudisha watu (na hata vongozi) wengi lakini sasa hivi anahaha kusaka pesa ya matibabu
Photo Credit:
Kanumba the Great
Marehemu Hamis Kitambi
Mmoja ya waliofanya vema kwenye tasnia ya muziki hapa nchini ambaye mpaka mauti inamkuta alikuwa kwenye hali isiyoendana na aliyofanya
Photo Credit:
Wanamuziki Tanzania blog
Unadhani ni hawa tu? Unakumbuka nyimbo kama Mwanameka, Georgina, Masudi, Dunia Imani Imekwisha, Sunia Uwanja wa fujo, Siwema, Zuwena na nyingine ambazo hata sasa "zinafunika" zile zilizoko studioni zikiandaliwa "kupakuliwa"?
Umebahatika kusoma maisha yake na HESHIMA aliyopata kwa MCHANGO WAKE KWA JAMII? Jikumbushe hapa kwa Uncle Kitime
Kwa ujumla, ukiacha wanasiasa wakongwe kama Hayati Baba wa Taifa, Mzee Kawawa na kizazi chao, mtu anayeheshimika na kuthaminika Tanzania yetu si yule ALIYEJITOA KWA DHATI kutenda yaifaayo jamii.
Si unakumbuka habari kuhusu baadhi ya waliokuwa viongozi wa utawala wa Mwl Nyerere ambao hawakujiwekea mali na sasa wanaishi kwa msaada wa wanandugu kwa kuwa "hawakujiwekea cha juu" kwa namna iiumizayo jamii sasa?
Labda (na najua kuwa) tulistahili kuwaenzi waliotuonesha njia.
Najua kuwa tulistahili kuwaheshimu na kuwatunza.
Najua kuwa tulistahili kuwathamini.
LAKINI SICHO KINACHOFANYIKA.

Tumeshindwa kuwaenzi, kuwathamini na hata kuwatunza na kuwatuza kwa waliyofanya.

Lakini hapa naizungumzia Tanzania Yangu.....Inayopuuza HALL OF FAME na kuendelea kutukuza HALL OF SHAME

Ni aibu..............

"Nawaza kwa sauti tuuu!!!!!"


Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA

Tuonane "Next Ijayo"

1 comment:

Simon Kitururu said...

Si utani ulichosema Mkuu!