Wednesday, November 10, 2010

UJUMBE WA Da SUBI KWA WADAU WA WAVUTI.COM......

Da Subi wa www.wavuti.com
Kwa heshima na taadhima ya waungwana na wastaarabu (kwa tafsiri sahihi ya kamusi kwa maneno hayo na si unyambulisho), napenda kufahamisha wasomaji wa wavuti.com kuwa ninayo furaha na nimejawa na wingi wa shukrani kwa michango na changamoto zinazotolewa na watoa maoni. Kupo kuvumiliana kwa hali ya juu.

Walioanza kusoma blogu hii mwanzoni watakumbuka kuwa nilikuwa nikiandika na kuchapisha matoleo binafsi wakati mwingine kama 'mwendawazimu' kutokana na kushindwa kuwa na maneno ya kistaarabu wakati wa kuandika katika matoleo hayo, ili kufikisha ujumbe kusudiwa. Lakini kwa miezi ya hivi karibuni, matoleo hayo yamepungua. Sababu hasa ya kufanya hivi ni kutokana na kutaka kuacha kuandika zaidi habari za “mafumbo” na zenye kutumia tamathali za semi, na kuanza kuziandika peupe.

Nimepokea jumbe tatu tofauti zinazolandana, ndani ya wiki moja:-

- Mosi, unatoka kwa Mabalozi wawili kuniandikia kuwa huwa anasoma wavuti.com
- Pili, unatoka kwa mapadre wawili (mmoja yupo Tanzania, mwingine yupo Roma)
- Tatu, unatoka kwa kijana ambaye amepata “mchumba” kutokana na “mchumba” huyo kupendezwa na maoni aliyokuwa akiyaacha kijana (sikutarajia kuwa maoni yako yanaweza kukupatia mpenzi anayeweza kuwa mwenza wa maisha, so be careful with what you write, people take notes, you could be attracting or scaring away someone. Your words reflects your personality).

Dondoo za barua pepe hizo, mojawapo ikinitaka kusema jambo, ndizo zimenisababisha niandike toleo la leo.

Kwa siku za hivi karibuni, wavuti imekuwa ikipata wasomaji wengi zaidi (kwa mujibu wa takwimu “stats”).

Ni katika ongezeko hilo ninapenda kukufahamisheni kuwa wasomaji wa wavuti si watu wanaoperuzi mitandao tu kama ‘majuha’ la hasha! ni watu ambao husoma na kufuatilia zaidi habari zinazogusa maisha ya jamii ya Mtanzania aliyeko ndani na nje ya nchi.

Wapo watu wa umri na rika kubwa, wanaotimu miaka 70, wanaosoma wavuti.com (uthibitisho ninao, sitauanika)
Wapo vijana wengi wanaofika hapa kujua “kulikoni”, na hawa ni wengi.
Sina uhakika na watoto....

Hivyo basi, ninapenda kuomba samahani kwa mtu yeyote anayeweza kuwa amekwazwa na matumizi ya lugha aidha yangu binafsi au ya watoa maoni. Sina uthibitisho kuwa hili linaweza kuzuiwa kwa asilimia 100, hivyo tuvumiliane pale inapowezekana. Hii ni kutokana na kutokufahamiana kwetu na kutokana na uhuru wa matumizi ya lugha kwa mhusika. Tunafahamu kuwa mtu anapokuwa huru bila kufungwa na woga kuwa niandikapo haya watanifahamu, basi mtu huyo huweza kuandika atakavyo. Lugha na matumizi ya maneno haya yanaweza kuwaudhi baadhi yenu. Nami ninakusihini, tafadhali, kwa heshima yenu, mvumilie kama wazazi/walezi wanavyowavumilia vijana wao wanapokuwa na “frustrations” lakini huwarejeza kwa maneno ya upole na yenye maelezo yanayokidhi haja. Kwa hiyo, ili kuiwekea uwiano (balance) hali hii, ninawasihi pale yanapotolewa maoni yenye maswali, dukuduku na kutaka maelekezo, ili kupunguza jazba na kero, basi walao mchukue muda wenu kutoa maelezo au maelekezo ya wapi maoni hayo yafikishwe (nafahamu ipo tovuti ya wananchi.go.tz lakini ni kama “geresha”, kwamba mlitaka tovuti ya maoni, hiyo hapo! Kwa maana watu wanaandika na kuandika lakini majibu ni "nehi" yaani, hakuna).

Vijana, ni kweli damu zinachemka, lakini badala ya kutumia lugha ya matusi na kejeli ambayo itamzuia hata mwenye jibu kufikiria kutumia muda wake kujibu hoja hizo, basi tujidhili kidogo, andika kero na hasira yako lakini usimtusi mtu (hata ikiwa unadhani kutumia kwake cheo na madaraka vibaya ni tusi kubwa kwako na kwa wananchi, bado kumkosoa mtu huyo si vyema kutumia matusi, hebu mwaibishe kwa kumwekea kasoro zake ili aonekane “kubwa jinga” kwa kutumia lugha nzuri ili kuwathibitishia kuwa vijana si “waruwaru” kama wanavyodhania. Prove them wrong, use a diplomatic language, wenyewe watatia heshima).

Shukrani kwenu, mmewezesha kufikia ONE MILLION PAGE VIEWS in just ONE FREAKING YEAR!!!

This would have not been possible if it were not for YOU guys!

Let’s maintain wavuti.com a blog for sharing SCHOLARSHIPS, OPPORTUNITIES (jobs, grants, trainings, courses, seminars) and NEWS (local and international that affects our nation) and not to forget those “lighter moments”.

KUMBUSHIO NA SISITIZO :
wavuti.com hadi sasa HAIFUNGAMANI na mrengo wowote (siasa, dini, taaluma, rangi ya mtu, jinsia, kabila, rika, nk.)
Ninapokea ujumbe kupitia
subi@wavuti.com na kulingana na maudhui, ninauchapisha kwa wakati muafaka.

8 comments:

Simon Kitururu said...

Mmmh!

Masangu Matondo Nzuzullima said...

Wavuti.com sasa ndiyo tovuti yangu nambari wani kwa kujipatia habari za Tanzania na pimajoto ya hali ya kisiasa.

Ni vigumu sana kuzuia maoni ya watu wenye mihemko na jazba hasa kwa tovuti ambayo haina "kichujio" kama hii ya Da Subi (kwa wengine kule maoni yo yote ambayo yanagusa hata kidogo tu chama fulani basi kamwe hayatoki).

Sijaona matusi (ya kutisha) katika wavuti mbali na jazba za mara moja moja za wadau na sidhani kama kuna haja ya kuweka kichujio..

Hongera Wavuti.Com kwa kufikia wasomaji 1,000,000 ndani ya mwaka mmoja. Ikiendelea hivi basi muda si mrefu Wavuti itakuwa tovuti nambari wani nchini Tanzania. Songeni mbele!

John Mwaipopo said...

chema chajiuza. niungane na profesa matondo katika mawili.

mosi, wavuti.com ni outlet ya habari, elimu,nafasi za kazi na burudani si tu kwa watanzania walioko nje bali hata sisi tulioko tanzania. huwanajiuliza hivi huyu mdada halali usingizi au huwa hafanyi kazi nyingine.

pili, nimnukuu prof matondo tena 'kwa wengine kule maoni yo yote ambayo yanagusa hata kidogo tu chama fulani basi kamwe hayatoki'

hili la tatu ni la kwangu mwenyewe. tofauti na waendeshaji wa zile blogu zinazodhani ndizo za jamii, subi pia hupata wasasa wa kutembelea blogu na wavuti zingine. nina maana kuwa, tofauti na hao wengine, yeye hupitia blogu zingene kuchangia, kujifunza na kuelimisha.


to me wavuti.com's simply the blog of the year.

Subi Nukta said...

Shukrani kwa Mubelwa kwa kuchapisha toleo hili katika blogu yake.
Shukrani kwa Simon, Prof. Masangu na kaka John M. Ushirikiano wenu, changamoto zenu na zaidi sana kusoma muundo na maudhui katika blogu zenu huwa ni changamoto kwangu ya kutaka kufanana nanyi au kufanya tofauti. Nimekuwa nina kiu kubwa ya habari zinazoihusu Tanzania, hii ndiyo siri kubwa ya mimi kuweza kupata habari nyingi za Tanzania na kuzishirikisha wengine katika blogu. Nakiri kuwa kile ninachoweka ni kutokana na kuvutiwa nacho na kupenda wengine wafahamu pia.

Changamoto zinakua na kuongezeka, lakini kamwe sitaki kujisahau wala kubweteka. Ushirikiano wa wanablogu ndiyo unaonipa nguvu kwani bila huo, nitapoteza kiasi kikubwa cha upataji na uhakiki wa habari.

Mwishowe, nimesumbuka na kuona watu wakisumbuka kutafuta nafasi za ufadhili wa masomo na hatimaje ajira, basi nikaona ya nini ikiwa ninayo nafasi ya kuzitafuta, basi mbona nisiwashirikishe wengine kwenye blogu? Uchoyo faida yake ipi? hakuna. Ni hasara tu. Na sipendi hasara.

Potelea mbali huwa ninakesha na wakati mwingine sijui muda wa kulala upi na wa kuamka upi, ila namshukuru Mungu kwa afya na uhai. Nikichoka nitaacha.

Shukrani sana!

Masangu Matondo Nzuzullima said...

@ Mwaipopo: "hili la tatu ni la kwangu mwenyewe. tofauti na waendeshaji wa zile blogu zinazodhani ndizo za jamii, subi pia hupata wasaa wa kutembelea blogu na wavuti zingine. nina maana kuwa, tofauti na hao wengine, yeye hupitia blogu zingene kuchangia, kujifunza na kuelimisha"

Ni kweli. Sijawahi kuona maoni ya "Ankal" au "Mwenyekiti" katika blogu yo yote ile. Pengine wao wamesharidhika na hatua waliyoifikia na hawana kipya cha kujifunza katika blogu zingine - hata ile kutoa ushauri na mwongozo hasa kwa wanablogu wachanga.

Da Subi ndiyo kimbilio letu wanablogu. Na ukimwuliza swali unajibiwa mara moja tena kwa jibu zuri refu lenye kuelimisha. Naye huwa hasiti kupita katika blogu mbalimbali na kutoa mawazo yake huko. Na akiona kwamba blogu yako haijakaa sawa, mara moja anakujulisha na kukupa ushauri. Mchango wake ni mkubwa mno!

Mzee wa Changamoto said...

Amani, Heshima na Upendo kwenu nyooote.
Kwanza hili la Da Subi naamini nimekuwa nikimueleza mwenyewe na kwa kuwa mmegusia hapa mambo mengi, wacha nami niguse jambo.
Kwanza niwaombe radhi nyote kwa ukimya wangu kwani sionekani kwenye utoaji maoni kwenye vibaraza vyenu. Tatizo kubwa ni kuwa nimebanwa saana na ratiba na muda mwingi ninaosoma blogu ni kazini na ama shuleni ambako kote wameweka "machujio" ambayo hayaniruhusu kuweka maoni kwenye blogspot. Ni WORDPRESS pekee inayoruhusu kuweka maoni. Na tovuti kamili kama ya Da Subi.
Lakini naamini siku yaja ambayo nitamaliza shule nikarejea maonini.
Kuhusu maoni yenu kaka Mwaipopo na Kaka Matondo, kwanza nichangie kaka Matondo uliposema "Ni kweli. Sijawahi kuona maoni ya "Ankal" au "Mwenyekiti" katika blogu yo yote ile. Pengine wao wamesharidhika na hatua waliyoifikia na hawana kipya cha kujifunza katika blogu zingine - hata ile kutoa ushauri na mwongozo hasa kwa wanablogu wachanga."
HII SI KWELI..
Ukweli ni kuwa wanatoa maoni na wanajiunga na blogu nyingi. Ila si za kiJAMII kama tujitahidizo kuweka. Kwa hiyo kwao wamesharidhika na kiwango ama hawaoni kama kuna la kujifunza.
TOFAUTI NYINGINE ni kuwa ukiona kitu kiko visivyo ama unahisi huna uhakika nacho, ukimuandikia Dada Subi anakujibu kama atarekebisha ama la na iwavyo vyovyote atakueleza kwanini aliandika alivyoandika na kati ya yeye na wewe ni nani aliye sahihi (kulingana na uchunguzi atakaofanya)
Kuhusu kutembelea blogu za wenzake, hilo sihitaji kueleza, ila nitakaloeleza ni KUTUSAIDIA KATIKA MAMBO MBALIMBALI na kama akikueleza kitu mara kadhaa ukashindwa kuelewa, ANAKUTENGENEZEA VIDEO YA KUFANIKISHA UELEWA.

Mimi sina ninavyoweza kumueleza Da Subi.
Mwacheni yeye aitwe yeye.

Nasi tuendelee kushiriki nafasi yetu kuwezesha kubadili fikra za wananchi kuhusu uelimishaji wa blogu.
NI LAZIMA JAMII IBADILIKE NA IANGALIE BLOGU CHANGAMOTO NA FIKIRISHI KAMA ZA WOTE MNAOCHANGIA NA KUSOMA HIZI "ZETU"

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Mzee wa Changamoto: Pole na hongera kwa kungangarika na shule. Hakuna jambo la muhimu kama hili hasa katika nchi hizi za wenzetu. Kila la heri na baada ya muda si muda utakuta ushakata mzizi wa fitina na kubebeshwa nondo yako. Furaha!

Blogu zetu hizi ni muhimu katika kujenga na kuimarisha "civil society" na kilichoyafanya katika uchaguzi huu ni ushahidi tosha (http://matondo.blogspot.com/2010/11/hongereni-wanablogu-kwa-kazi-nzuri.html). Tuendeleeni kushirikiana na kutiana moyo. Na kila tunapokwama, tunapo mahali pa kumbilia.

chib said...

Kakiri mwenyewe kuwa sometimes huwa anakesha, ni kweli, na nilishamuuliza...

Mimi pia huwa nasoma sana wavuti.com, hata kuna baadhi ya wahesh nilishawapa dokezo na namna ya kuipata wavuti waweze kujichotea habari mpya na mambo mengine kadhaa aka habari zilizovunjikavunjika au breaking news :-)
Cheers Subi, Lakini afya yako muhimu pia