Saturday, January 1, 2011

Mhe Rais, kabla hatujazungumzia katiba mpya, tufafanulie hili...

"NI VIPI WIZARA YA KATIBA IMETUMIA PESA ZA WANANCHI BILA KUTIMIZA HILI NA SASA UNAHITAJI KULIWEKEA TUME MAALUM?
Ni kweli tume hii itafanya kazi nzuri kuliko WIZARA? Na kama ndivyo, utaendelea kuwa na Wizara ya Katiba isiyojishughulisha na katiba kwa kuwa suala la katiba litashughulikiwa na tume utakayounda? Na pesa je? Kutakuwa na peza za WIZARA YA KATIBA na TUME YA KATIBA? "
Photo Credits: Dimitrios Kambouris via
Josephat Lukaza Blog
Usiku wa kuamkia leo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Jakaya Mrisho Kikwete amehutubia Taifa katika salamu zake za mwaka mpya. Hotuba yake hiyo ya karibu robo tatu ya saa iligusia mambo mengi sana ikiwemo Hali ya Usalama nchini, Demokrasia, Uwajibikaji wa mawaziri, Nidhamu katika matumizi ya mali za serikali, Hali ya Uchumi, Hifadhi za chakula, Kilimo, Matatizo ya Umeme, Mahusiano ya kimataifa, Michezo na kisha akagusia MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA UHURU wa Tanganyika (ameita Tanzania Bara).
Na katika kugusia hilo, Mheshimiwa Rais wangu amezungumzia mambo makuu manne ambayo yanapangwa kufanyika mwakani. "Kwanza, nautangaza mwaka 2011 kuwa ni Mwaka wa Maadhimisho ya Miaka Hamsini ya Uhuru wa Tanzania Bara....Pili, tufanye tathmini ya kina ya mafanikio tuliyoyapata, katika juhudi zetu za kujiletea maendeleo katika miaka hamsini hii. Kila Wizara, idara na taasisi za Serikali na hata sekta binafsi zifanye tathmini ya eneo lake. Tathmini hizo ziandikwe katika vitabu ili kuhifadhi kumbukumbu hizo muhimu kwetu na kwa vizazi vijavyo. Vitabu na nyaraka hizo vitakuwa kumbukumbu zenye manufaa makubwa kwa wenzetu watakaokuwepo mwaka 2061 wakati wa kusherehekea miaka 100 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Itarahisisha kazi yao ya kufanya tathmini wakati huo......Tatu, kwamba yafanyike maonyesho maalum katika Uwanja wa Maonyesho wa Julius Nyerere hapa Dar es Salaam na kote mikoani kwenye viwanja vya maonyesho, kuelezea mafanikio yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali katika miaka 50 tangu Uhuru wa Tanzania Bara..." Hili nilishaligusia HAPA na nitalizungumzia kadri muda utakavyoruhusu. Kwa leo niendelee na mada kuu ambayo jambo la nne ambapo Mhe Rais amesema...
"Ndugu wananchi.
Jambo la nne ambalo tulilokubaliana kufanya ni kuanzisha mchakato wa kuitazama upya Katiba ya Nchi yetu kwa lengo la kuihuisha ili hatimaye tuwe na Katiba inayoendana na taifa lenye umri wa nusu karne. Katiba yetu ya sasa tuliyoachiwa na waasisi wa taifa letu, imeifanyia nchi yetu mambo mengi mazuri na kuifikisha Tanzania na Watanzania hapa tulipo. Tunayo nchi moja huru, ya kidemokrasia na inayoendesha mambo yake kwa kuzingatia utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na mgawanyo wa madaraka miongoni mwa mihimili mikuu ya dola. Nchi yenye amani, utulivu na watu wake ni wamoja, wanaopendana na kushirikiana na maendeleo yanazidi kupatikana.
Pamoja na hayo, mwaka 2011, nchi yetu inatimiza miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, miaka 47 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar na miaka 47 ya Muungano wa nchi zetu mbili. Yapo mabadiliko mengi yaliyotokea katika nyanja mbalimbali za maisha ya nchi yetu na watu wake katika kipindi hiki. Kwa ajili hiyo ni vyema kuwa na Katiba inayoendana na mabadiliko na matakwa na hali ya sasa. Katiba ambayo italipeleka taifa letu miaka 50 ijayo kwa salama, amani, umoja na kuwepo maendeleo makubwa zaidi.
Ndugu Wananchi;
Ndiyo maana tukaamua kuanzisha mchakato huu na kwa ajili hiyo, nimeamua kuunda Tume maalum ya Katiba, yaani Constitutional Review Commission. Tume hiyo itakayoongozwa na Mwanasheria aliyebobea, itakuwa na wajumbe wanaowakilisha makundi mbalimbali katika jamii yetu kutoka pande zetu mbili za Muungano. Jukumu la msingi la Tume hiyo litakuwa ni kuongoza na kuratibu mchakato utakaowashirikisha wananchi wote bila kubagua, vyama vya siasa, wanasiasa, wafanyabiashara, asasi za kiraia, mashirika ya dini, wanataaluma na makundi mbalimbali ya watu wa nchi yetu kote nchini, katika kutoa maoni yao juu ya wayatakayo kuhusu Katiba ya nchi yao.
Baada ya kukamilisha kukusanya maoni,Tume itatoa mapendekezo yake yatakayofikishwa kwenye vyombo stahiki vya Kikatiba kwa kufanyiwa maamuzi.Baada ya makubaliano kufikiwa, taifa letu litapata Katiba mpya kwa siku itakayoamuliwa ianze kutumika.
Ndugu Wananchi;
Ni matumaini yangu kuwa mchakato huo utaendeshwa vizuri, kwa amani na utulivu kama ilivyo sifa ya nchi yetu na mazoea yetu ya kujadiliana bila kugombana. Wananchi watapewa fursa ya kutosha ya kutoa maoni yao kwa uhuru na pawepo kuvumiliana kwa hali ya juu pale watu wanapotufautiana kwa mawazo. Pasiwepo kutukanana, kudharauliana, kushutumiana, kubezana, kuzomeana wala kushinikizana. Naomba washiriki waongozwe kwa hoja badala ya jazba. Tukiwa na jazba, hasira na kushinikizana kamwe hatutaweza kutengeneza jambo jema. Na inapohusu Katiba ya Nchi itakuwa hasara tupu. Haitakuwa endelevu na kulazimika kufanyiwa marekebisho mengi mwanzoni tu baada ya kutungwa.
Nawaomba Watanzania wenzangu wenye maoni yao wajiandae kushiriki kwa ukamilifu katika mchakato huu. Katoeni maoni yenu mazuri yatakayowezesha nchi yetu kuwa na Katiba itakayokidhi matakwa yetu ya sasa na ya miaka 50 ijayo."

Mheshimwa Rais. Kwanza nikupongeze kwa mikakati yote uliyoieleza. Umeonekana kutoa ufafanuzi katika mambo mengi. Lakini kuna moja ambalo NINAOMBA UTUFAFANULIE (hata kupitia msaidizi wako) KABLA HATUJAANZA MCHAKATO WA KATIBA MPYA. Katika Baraza lako la mawaziri ulilotangaza Nov 24 mwaka jana ulitaja WIZARA YA KATIBA NA SHERIA ambayo sasa ipo chini ya Mhe Selina Kombani. Waziri wa Sheria na Katiba Mhe Celina Kombani
Ninalowaza ni kuwa Wizara hii kamili yenye bajeti na watendakazi kamili ilikuwa ikifanya nini katika awamu yako ya kwanza? Natambua uwepo wake kama ilivyoonekana HAPA kwenye baraza lako la kwana ambapo ilikuwa chini ya Mhe Mary Nagu. Je! Kuna loloe ambalo tunaweza kuelezwa kuwa Wizara hiyo ilifanya katika miaka mitano ya awali katika suala la Katiba?
Ni kweli kuwa kuna UELIMISHAJI WOWOTE KUHUSU KATIBA uliofanywa na Wizara hii? Ama (kama mlijua kuwa Tanganyika itatimiza miaka 50 ya uhuru na 47 ya Tanzania) hamkukumbuka kutumia Wizara hii kuanza kufanya tathmini ya kujua nini kingehitajika mwaka 2011? Je!! Tutakosea kusema kuwa HUU NI MCHAKATO WA ZIMAMOTO?
Umesema (na hapa nakunukuu) "Baada ya kukamilisha kukusanya maoni,Tume itatoa mapendekezo yake yatakayofikishwa kwenye vyombo stahiki vya Kikatiba kwa kufanyiwa maamuzi.Baada ya makubaliano kufikiwa, taifa letu litapata Katiba mpya kwa siku itakayoamuliwa ianze kutumika."
SWALI LANGU NINALOOMBA UFAFANUZI ni kuwa, NI VIPI WIZARA IMETUMIA PESA ZA WANANCHI (na umenukuliwa ukisema matumizi ya serikali yameongezeka) BILA KUTIMIZA HILI NA SASA UNAHITAJI KULIWEKEA TUME MAALUM?
Ni kweli kuwa tume hii itafanya kazi nzuri kuliko ambayo ingefanywa na WIZARA? Na kama ndivyo, utaendelea kuwa na Wizara ya Katiba isiyojishughulisha na katiba kwa kuwa suala la katiba litashughulikiwa na tume utakayounda? Na pesa je? Kutakuwa na peza za WIZARA YA KATIBA na TUME YA KATIBA?
Ama watendaji wa Tume ya utakayounda watakuwa ni wafanyakazi wa Wizara ya Katiba? Kama ndivyo, natumai TUME HII HAITAKUWA MATUMIZI YA ZIADA bali sehemu ya shughuli za WIZARA ambao kwa kuwa zilistahili kuwa zimefanyika ama zifanyike kama wajibu wa kawaida na si "ofa" kwa waTanzania.
MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI AFRIKA.

6 comments:

Mbele said...

Shukrani kwa changamoto yako. Napenda tu kugusia kuwa kule kwenye ukumbi wa Facebook m-Swahili mwenzetu mmoja alipendekeza kuwa wimbo wetu wa Taifa tuubadili. Badala ya kusema "Mungu Ibariki Tanzania, wabariki viongozi wake," iwe "Mungu Ibadili Tanzania, wabadili viongozi wake..."

Lilikuwa ni pendekezo. Nami napendekeza tutenge kafungu, tuunde tume kuangalia pendekezo hili :-)

emu-three said...

Mhh, kweli hilo swali nalo...wasemaje mhe wa nchi...mmh, Mzee Mbele, kweli hata huo wimbo unahitai marekebisho, hebu niuuimbe kwanza.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

duhu wabadili viongozi\
kali hiyo

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Hii changamoto kweli kweli. Je anao ubavu wa kufafanua hii changamoto au tumemwonea mtu mwenyewe?
Tufurahi japo tusibweteke kuwa amejifunga akidhani hii itaishia kuwa kama safari ya Kanani ambayo imegeuka kuwa ya mafisadi na mafisidunia.

Christian Bwaya said...

Kuna tofauti ya kuwa Rais wa Tanzania na Rais wa Watanzania. Unaweza kuwa Rais kwa mujibu wa sheria na usiweze kuwa Rais mioyoni mwa unaodhani unawaongoza.

Anonymous said...

Katiba yetu ina mapungufu mengi ambayo kwa sasa ayaendani na hali halisi ya mazingira,kuna mtu anaweza nipa sababu mbili za kuwa na wakuu wa wilaya na mikoa na hapo hapo kuna RDD sijui bado wanahitwa hivyo na wako wa wilaya pia.kuna shule ngapi zinahitaji vitabu na madarasa safi,hiyo high life ya mkuu wa wilaya na mkoa wangepewa wananchi sio mtu mmoja,kuna mikoa 26 sasa na wilaya tele tukiweza kuchukua hizo shangingi na nyumba zao tukawekeza ktk afya na elimu sisi tutakuwa wpi?tunaishia kusema nchi maskini kumbe wachache wanashiba pembeni na ndio maswaiba wa................