Saturday, January 22, 2011

Uswahili, Mswahili na Kiswahili...Ni nini nani na kipi?

Tunatambulishana na kutambulisha vitu kwa namna ama mitindo mbalimbali (japo si lazima utambulishanaji huo uwe sahihi ama makini)
Mfano: Kuna mchekeshaji mmoja mwenye asili ya Amerika ya Kusini, aliwahi kusema kuwa si lazima uwe umezaliwa kwenye ukanda atokao yeye ili utambulike kuwa ni m-Latino, bali ukishafanya / kupata huduma za ki-benki (kama ku-cash check nk) kwenye liquor store, basi wewe ni m-Latino.
Nilifurahia tu sentensi yake kwa kuwa najua kinachowafanya ndiugu zetu hao wafanye hivyo, lakini jana nilipokuwa nasikiliza nyimbo kwenye mp3 yangu, nikakumbuka nilivyokuwa naitwa MSWAHILI.
Basi kama wako sahihi, hapa chini paonesha maisha na harakazi za kwetu

Na siwezi kupinga kilichonifanya kuitwa hivyo kwa kuwa nilijua fikra za walioniita MSWAHILI. Kwao waliamini kuwa kuongea kwa namna fulani ama hata kusikiliza miziki yenye mafumbo ama lugha fulani ni uswahili. Na mimi nilikuwa natimia kwenye tafsiri yao. Nilipenda na bado napenda maongezi yenye kueleza kitu kwa namna ya kibunifu. Nilipenda na bado napenda maongezi ambayo yana mifano na kuchangamsha akili. Nilipenda na bado napenda maongezi ambayo yana TUNGO TATA.
Yaani kwangu ningependa kusema "chupi ya maziwa" badala ya sidiria. Chumba cha bwenini ungesikia mtu akiulizwa kama fulani ni "bubu wa masikio" badala ya kiziwi kwa kuwa tu hakusikia ulichomueleza. Ni misemo miingi sana ya kueleza kitu kwa namna yake. "Mtoto' ingekuwa na maana nyingi kulingana na sentensi na sasa ukiongezea "mtoto si riz'ki" nayo ingemaanisha vingine. Ilikuwa raha.
Lakini pia nilipenda kusikiliza nyimbo zilizokuwa na MAFUMBO na hata TUNGO TATA. Sasa nikaambiwa hiz ni nyimbo za kiSwahili kwa kuwa zilikuwa zikisema vibaya na wengine kusema ati zilikuwa zikitusi. Lakini nililogundua ni kuwa nyimbo hasa MDUARA ni nyimbo za kufikirisha na pengine badala ya kuziita za kiSwahili, tujifunze kuuliza kisemwacho na kama kina utata basi tusiwe wepesi kuamua alichowaza muimbaji bali tuwaulize waimbaji.
Leo nimekumbuka haya baada ya kusikiliza albamu yangu yenye mkusanyiko wa nyimbo za mduara na nimeona nishirikiane nanyi mawazo haya. Nikisikiliza nyimbo SHANUO na SITISHIKI zao Chuchu Sound nafurahishwa na upangiliaji wa vina na matumizi ya kiswahili fasaha. Mfano wanaposema "maisha si mashindano japo kipato kikubwa unacho wewe". Lakini pia kuna tungo chache Tata ambazo waweza zisikiliza hapa

Pia maumbo yaoneshayo uhalisia wa maisha kama "ni rahisi kuteka maji kwa pakacha kuliko yeye kuniacha" ambalo ni funzo kuwa kuna sehemu nyingine si za kujisumbua "kuharibu"
Lakini kuna mengi ya kujifunza katika "kauli" zao mwishoni. Labda tusikilize ili kujua tujifunzalo na pengine uwaze NINA WAZA NINI nisikilizapo hizi na pia waweza KUWAZA kama wawazao akili zangu kuwa za "kiswahili" wako sahihi

Na sasa tuhamie kwenye SWEET BABY ya TOT-Plus. Kuna kauli ambazo zilikuza mashaka lakini moja ya ambayo nilibahatika kuwa na mdahalo ni ile ya "Anti" ambayo wamezungumzia ku"gonga hodi mara 2 mbele, kama kimya gonga kimya mara 3. Kama kimya mwaga mzigo wako hapohapo nje. Ataupata". Tofauti pekee niionayo kati ya kilichoimbwa hapa na kwetu uHayani ni kuwa sisi kama umegonga mbele na nyuma hujamuona mtu, waacha ka-jani ka mgomba ili wakirejea wajue kuwa kuna aliyekuja akawakosa. Hatumwagi mzigo wao (labda kama umeambiwa ama kukubaliana hivyo). Sikiliza mwenyewe na uwaze.

Katika nyimbo hizi, kuna misemo miiingi sana ambayo inaweza kwenda na maana halisi lakini ikanyambulishwa visivyo. Kama nilivyosema HAPA kwa Binti Mkundi, "Mfano wimbo wa Aungurumapo Simba RMX ambayo Banza aliweka uhalisia wa maisha yetu japo wapo waliotafsiri kama matusi. Alisema "RAHA YA CHUNGWA, UMENYEWE, KISHA UKATIWE". Mimi ni kati ya walaji wazuri wa chungwa, lakini kila ninapofikiria kulimenya na kubaki na harifu ya maganda baada ya kula najiuliza mara mbili kama "kweli nahitaji kula chngwa wakati huo ama la?'" Na nikimpata wa kulimenya na kukata, NAWEZA KULILA WAKATI WOWOTE. Katika wimbo huo huo, Banza akasema "RAHA YA DAFU, UKISHAKUNYWA YALE MAJI, SHARTI DAU LICHOKOLEWE". Sijui atakayepinga kuwa hu ni ULAJI wa asili wa dafu ni nani? Kama huna kichokoleo kizuri basi ndio ungehitaji "njia m'badala" kama kulivunja kisha ukatumia kichokoleo chako hafifu kulila. Na sehemu nyingine akasema "RAHA YA NANGA BAHARINI, MTONI ITASHIKWA NA TOPE." Kwa sisi tuliokulia kwenye misafara ya majini wajua nanga. Na kwa wavuvi wanajua karaha ya nanga yenye matope. Haimaanishi kuwahuwezi kushusha nanga mtoni (maana waliozoea kuvua mtoni wanafanya hivyo) ila SI KWA RAHA KAMA BAHARINI. Na huo ni ukweli ulio wazi. Sasa kutafsiri vingine na wanavyouliza watu nadhani si tatizo la muulizaji, bali la mtafsiri.
UKWELI NI KUWA NAWAZA SIJUI NINAWAZA NINI?

***"Waliwaza nini ni kipengele cha kuelimishana tukifurahia. Hiki kitakuwa kikikuletea habari za kweli na kushangaza kuhusu watu ambao wamefanya yale ambayo unaweza kujiuliza kuwa WALIWAZA NINI? wakati wanatenda haya.
Kitakuwa na habari fupifupi kutoka ulimwenguni kote. Kwa habari zaidi kuhusu kipengele hiki
BOFYA HAPA"***

7 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Watu wameshawahi kuandika tasnifu za shahada za uzamivu kabisa kuhusu maswali haya. Si maswali rahisi kuyajibu hasa kwa wakati huu ambapo Kiswahili kimejitandaza duniani kote.

Hata tukiachana na Mswahili, pengine tujiulize tu Mhaya ni nani? Ni yule anayezungumza lugha ya Kihaya kwa ufasaha kama Kamala? Au ni mtu anayeujali na kuuthamini Uhaya - hata kama hafahamu Kihaya na utamaduni wa Kihaya? Vipi kuhusu kijana wa kizazi cha dot.com ambaye hafahamu Kihaya wala mila na desturi za Wahaya (mf. umuhimu wa senene). Bado tunaweza kumwita kuwa ni Mhaya? Ni nini kinachomfanya mtu aitwe Mhaya. Wewe Muberwa ni Mhaya? Kwa nini?

Kuna makala moja nzuri sana kuhusu jambo hili imeandikwa na Profesa John Mugane wa Chuo Kikuu cha Harvard ambayo inaongelea kwa ufasaha kuhusu suala hili. Na kwa watu kama Ngugi wa Thiong'o, wewe kama huwezi kuongea lugha ya kabila lako basi huna haki ya kusema ni memba wa kabila hilo!

Sehemu iliyobakia ya swali lako ni ya kifalsafa na inahusisha mambo mengi yakiwemo mfumo wa kinyonyaji na mahusiano ya kihasama kati ya makampuni ya Kimagharibi ambayo yanafaidika na biashara ya kondomu na vyandarua kwa kusaidiana na viongozi wetu wachache wenye njaa. Hili naliachia wachambuzi wengine walijadili kwa kina na pengine nami nitapata mawili matatu ya kujifunza na hatimaye kuongezea. Leo tunazugwa kwa kuletewa vyandarua na kondomu za "bure", na kama ulivyosema msisitizo hasa siyo katika kiini cha tatizo bali ni katika dalili tu. Na hili ni mojawapo ya matatizo makubwa ya Afrika. Na kwa jinsi tulivyotawaliwa kifikra, yaani tumekuwa kama vile hatuwezi kufikiri na kuja na masuluhisho yetu wenyewe - au kupendekeza masuluhisho tunayodhani kwamba yatagusa kiini cha matatizo yetu...Tumezoea vya bure na kuamuliwa mambo kama watoto wadogo na baada ya muda cha moto tunakiona. Hata huu upuuzi wa Dowans na Richmond tunaohangaika nao unaingia katika mkumbo huu huu.

Unakumbuka pia kuna kipindi fulani kulikuwa na ukame sana na maji katika bwawa la Mtera yalishuka sana. Baadhi ya wanasiasa walipendekeza eti kuleta wataalamu wa kuleta mvua kutoka Vietnam kuja kufanya "cloud seeding" ili mvua inyeshe karibu na bwana hilo ili lijae na mgao wa umeme hatimaye uwe historia. Kwa masuluhisho kama haya ni wazi kwamba tunavyoyaona matatizo yetu pengine ndiyo tatizo.

Nimebwabwaja vya kutosha. Ngoja niachie na wengine.

emu-three said...

Mmmh, mimi nirudia usemi usemao `mkataa utamaduni wake ni mtumwa' kwanini nimeanza hivi, kwasababu katika jamii zetu watu wamekuwa wakitumia neno `uswahili' kwa tafsiri mbaya, na hili chimbukolake ni `kiswahili'.
Najua wanamaanisha watu wa pwani, na zile tabia zo ambazo ni kinyume na maadili zikautwa `uswahili' ...lakini je tabia mbaya za makabila yetu zinaitwa `kabila letu...' ni nadra sana, ...
Sasa kwanini watu wakafikia hatua ya kukinasibisha kiswahili , au uswahili kwenye matendo mabaya. Upo usemi usemao, `ukitaka kumuua mbwa muite kwanza maneno mabaya. Hawa walioanzisika tala-lala hizi za uswahili ni wapinzani wa lugha ya kiswahili...!
LAKINI Wahenga husema chema chajiuza kibaya chajitembeza, leo hii kiswahili kinapanuka, hawa jamaa wanaima chini kwa aibu...kwasababu huu ni utamaduni wetu, sehmu hizi za Africa masharaki, tena na kati, na sasa ...ipo siku mtasikia ni miongoni mwa lugha za kimataifa!
Mengine kutokana na hoja hii yapo wazi, kiswahili ni lugha, mswahili ni mtumiai wa lugha hii, na uswahili ni yale matendo ya wanaoutumia lugha hii, lakini je ndio maana yake inavyotafsiriwa...hapana kwani wanasema `ukutukanaye hakuchagulii tusi..' AU NIMEKOSEA JAMANI...NI hayo tu mkuu!

Simon Kitururu said...

Mmmh!

Fadhy Mtanga said...

mimi ni shabiki mkubwa wa Kiswahili....huwa nasuuzika sana nizisikilizapo tungo kama hizo.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kwangu Mswahili hutegemea na msemaji. Kwanza hakuna kabila la waswahili. Maana tunaambiwa kiswahili ni lugha itokanayo na mchanganyiko na muingiliano wa watu mbali mbali kwenye ukanda wa pwani. Hivyo nukta ya kwanza ni kwamba hakuna kabila la waswahili.
Mie hujiita mswahili hasa ninapokuwa na hawa wazungu nikimaanisha muafrika. Nilipokuwa naishi Kenya niliwahi kuwaita wenyeji wangu waswahli wakachukia. Maana kwao mswahili ni mtu asiyestaarabika.
Baada ya kuwaelimisha nini maana ya kuwa mswahili, sikuona tena wakichukia pale nilipowaita waswahili.
Kwa mfano, niliwaambia kuwa adui mkubwa wa mswahili ni mtu anayemnyemelea mkewe au binti yake.
Niligundua kuwa kwao mke au mume kwa baadhi ya makabila si kitu cha thamani sana ukilinganisha na fedha.
Hii ilitokea baada ya rafiki yangu mkikuyu kuniambia kuwa naweza kuchukua hata mke au binti wa rafiki yangu ilmradi kuna chapaa. Nilishangaa nusu kufa.
Hivyo kwangu mswahili ni muafrika wa kawaida anayeishi kwa mila na tamaduni za kiswahili.
Wanangu wamezaliwa Kanada, Lakini bado huwezi kuwaita wazungu au waamerika kwa sababu ya kuzaliwa tu.Wala huwezi kuwaita wanyasa kwa vile hawajui kinyasa na mimi si mnyasa pure ikizingatiwa kuwa mama yangu hakuwa mnyasa. Naitwa mnyasa kwa sababu ya urathi wa baba kuwa alikuwa mnyasa pure.Hivyo, kwa vile nimekulia Dar es salaam huwa napenda kujiona mswahili.
Kuondoa dhana nzima ya ule uswahili wa hasara kama vile majungu, kutojali muda na matusi, waswahili wa Dar hujaribu kutofautisha uswahili na uzaramo ingawa na uzaramo si mbaya.
Kama alivyosema mwalimu Matondo, unaweza kuandika msahafu kuhusiana na dhana hii na usimalize.
Kwa hiyo wabongo mkiitwa waswahili na wakenye wakati mwingine ni kutokana na kiswahahili chenu mulua.

Rachel Siwa said...

hapa patamu ngoja tujifunze zaidi!uswahilini kunavituko,mswahili sana yule,acha mambo ya kiswahili wewe, jamani tusiwe waswahili!!!!
hao wote au sote tunaongea kiswahili na majibu au maneno tunayotamka ni kama hayo na mengine mengi!!!!!!!!!

pcmaker said...

Neno mswahili linamaana zaidi ya moja maana ya kwanza mswahili ni mtu anae zungumza kiswahili.maana ya pili ni mtu anayeishi pwani ya afrika mashariki.lakini kwa maana za kimtaani mswahili ni mtu asiye kuwa mkweli.