Sunday, April 10, 2011

Tunapowaza kuhusu UKWELI wa UONGO huu....

UKWELI una matatizo makuu matatu. Tuanze na haya mawili (kwa mujibu wangu) kisha la tatu LITAFUNGA bandiko hilo. Tatizo la kwanza ni kuwa unapoamua kuufuata na kuuekeleza, unaweza kuwa miongoni mwa wachache Tatizo la pili ni kuwa, Ukweli ndio chanzo cha uongo. Uongo wote husemwa ili ufanane na kuaminika kama UKWELI. Na kabla uongo huo haujagundulika, huaminika na pengine kutekelezwa kama UKWELI. Waongo huamini katika UKWELI wa uongo wao na kwa bahati mbaya, hata WAKWELI huamini UONGO huo mpaka pale watakapokuja kujua ukweli kuwa ule ulikuwa uongo. Lakini sasa tuangalie kauli hizi mbili ambazo si ngeni, lakini UKWELI WA UONGO WAKE haufikiriwi vema. Na sasa tujaribu kuangalia.
1: MIMI NI MSIRI SANA. NIAMINI KWA KUWA SITOI SIRI. Unachotakiwa kuwaza hapa ni kuwa, u-SIRI ni nini na upi? Na je, kwa mtu kuwa msiri si lazima aendeleze kuwa na siri ya siri zake? Na Je!! Kwa kusema kuwa yeye ni m-siri na ana siri nyingine, hudhani kuwa ukimwambia SIRI yako itaongezeka katika orodha ya wale watakaotumika kupata kesi nyingine? Labda mtu aliye m-SIRI hatambuliki kwa kuwa haonekani, labda asemwe na asemwaye kuwa ni m-siri ni yule ambaye alieleza kuwa ana siri na hakuna kuaminika juu ya siri mpaka uiseme na mtu ajue ambacho hakujua, na kama atajua, haitakuwa siri tena na hivyo hatakuwa msiri. Ninalowaza ni kuwa NI KWANINI, ILI UDHIHIRISHE KUWA NI M-SIRI UNASTAHILI KUVUNJA MWIKO WA MTU M-SIRI? Na je, kuna mtu aliye msiri? Asemaye kuhusu hili, huonekana kuwa mkweli ama muongo? Na unaposikia kauli hii, unaamini kuwa ni ya UKWELI ama UONGO? Kwani sasa unawaza nini? Sikia kauli nyingine hii..........
2: MIMI HUDANGANYA MARA ZOTE. Ukiangalia sentensi hii, UNAWAZA NINI? Ninalowaza ni kuwa SENTENSI HII HAITAKUWA KWELI hata iweje. Suala hapa ni kuwa ....KAMA NI KWELI kuwa mtu huyu huwa anadanganya, basi sentensi hii ni ya kweli na hivyo mtu huyu hajadanganya sasa hivi. Kwa hiyo hadanganyi "mara zote" kwa kuwa safari hii kasema ukweli. Lakini KAMA SI KWELI kwamba mtu huyu hudanganya mara zote, basi sasa hivi amedanganya hivyo sentensi hii si ya kweli. Yote juu ya yote, mtu anayedanganya mara zote hatajulikana anadanganya bila kuwepo UKWELI wa UONGO katika UONGO wake. Lakiniiii...binafsi UNAWAZA NINI unapofikiria kauli kama hii? PENGINE nirejee kwenye ahadi yangu hapo juu, kwamba nitakueleza tatizo la tatu la ukweli. Nalo ni kwamba laweza kukufanya uuone kama uongo iwapo unaloamini ama kutaka kuamini ni tofauti na kile kinachoelezwa kama ukweli. Yawezekana KUWAZA nisemayo kwa namna niwazavyo kutakufanya uamini kuwa naeleza UKWELI WA UONGO, lakini kwa KUWAZA tofauti nami, kutakufanya uniwaze kama MUONGO JUU YA UKWELI WA UONGO niuandikao hapa.
Kwani wewe UNAWAZA NINI?


***"Waliwaza nini ni kipengele cha kuelimishana tukifurahia. Hiki kitakuwa kikikuletea habari za kweli na kushangaza kuhusu watu ambao wamefanya yale ambayo unaweza kujiuliza kuwa WALIWAZA NINI? wakati wanatenda haya. Kitakuwa na habari fupifupi kutoka ulimwenguni kote. Kwa habari zaidi kuhusu kipengele hiki
BOFYA HAPA"***

1 comment:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

mimi sio msiri labda sinaga siri. uongo?/ siwezi kusema mimi ni mwongo au mkweli labda niko neutral kwani kuna wakati inadbidi kudanganya na wakati inabidi kusema ukweli au kipande cha ukweli

isipokuwa duniani hamnagasiri na uongo huwa haudumu kwani ukweli wa kuwa ulidanganya huja kujidhiirisha baadaye. unampa mtoto wa watu mimba, unakta kw kudangaya then inazaliwa photocopy yako, haihitaji vipimo vya DNA kwa hiyo labda tusema hamnaga uongo au uongo haudumu bali ukweli!

sidanganyiki