Wednesday, May 4, 2011

Hesabu za siasa na ki-sisasa

Mara zote ni kinyume; wengi ndio wachache na wachache ndio wengi

Hivi ulibahatika kusoma toleo la Kaka Kamala alilosema MOJA JUMLISHA MOJA SAWA NA MOJA? (BOFYA HAPA KAMA ILIKUPITA). Je maoni ya waliochangia akiwemo Ndugu Born Again Pagan?
Kuna ukweli wa hesabu za wenzetu hawa wanasiasa ambazo kwa namna moja ama nyingine zimekuwa kinyume na zile tulizozoea kwenye masomo na elimu yetu ya kawaida. Wiki hii tumeanza na habari za kuuawa kwa Osama bin Laden. Watu wakasherehekea na kurukaruka wakisema WAMEMPATA MTU ALIYEKUWA AKITISHIA USALAMA. Lakini punde baada ya MTU huyo kuuawa, hali ya usalama ikaimarishwa duniani kote. Swali nililojiuliza na ninajiuliza ni kuwa "iweje mtu anayeonekana kuwa hatari auawe na kisha hali ya usalama iwe mashakani kuliko ilivyokuwa wakati yuko hai?" Unadhani unaambiwa ukweli kuhusu HATA ya mtu huyu? Ndugu yangu mmoja aliandika kwenye ukurasa wangu wa Facebook kwamba kama Osama alikuwa MTU HATARI, basi wamepata kimoja kati ya viwili. Wamempata MTU lakini hawajazuia HATARI. Lakini katika HESABU ZA KISIASA (ambazo naona zinakwenda kinyume na hesabu zetu wananchi), ni USHINDI. KWANINI?
Kwa HESABU ZAO, ni kama vile "wengi wanakuwa wachache na wachache wanakuwa wengi." Hakuna kujali kile wanachoimba na kuahidi kukitetea wakati wa kampeni zao. Hawawajali wananchi na kwao ubinafsi ni maana nyingine ya "manufaa kwa umma"
Labda tuangalie UMOJA WA MATAIFA ambao una wanachama lukuki na unaonekana "kutawala" dunia kimaamuzi lakini bado maamuzi ya mataifa matano yenye kura ya turufu ndiyo yanayoamua dunia iende wapi, iadibike na / kuadibishwa vipi, nani awe rafiki wa nani na nani awe adui wa nani hata kama hawana jibu la kwanini iwe hivyo. Na mataifa mengine yanatulia na kuendelea kutafsiri hiyo kama DEMOKRASIA.
Tukirejea kwenye ngazi ya nchi, tunaona kuwa maslahi ya wananchi pengine ndio kitu cha mwisho kufikiriwa akilini mwa "waheshimiwa" hawa. Wanatanguliza u-mimi na hata maamuzi yao hayaonekani kuwajali wengi ambao ndio waliowachagua. Hawawajibiki, hawaonekani kuwathamini na hawako katika nyadhifa zao kushughulikia lolote lihitajiwalo nao. Kwao, kulinda heshima yao ni jambo la muhimu kuliko kujali wananchi. Wanasikia matatizo, wanayaona na kisha WANAYAPUUZA
Nasema mahesabu yao yako kinyume maana kwao wananchi ndio "minority." Kwao wanaona kama wanahitajika kumaliza mahitaji yao kwanza ndio njia sahihi na ndio maana kwangu mimi ni WATAWALA kuliko viongozi.
Sasa kwanini tunawaamini? Kwanini tunawapigia kura wakati hatuna nafasi kwao kwani jamii nzima kwao ni "minority."
Wasikilize Morgan Heritage katika kibao chao hiki, POLITICIAN hasa wanaposema "why should we trust politicians, why should we vote every election? When there's no place for we, you and me, in the secret society they call us minority."

2 comments:

Simon Kitururu said...

SIjui kwanini nilipoanza kukusoma hasa hapa ``Mara zote ni kinyume; wengi ndio wachache na wachache ndio wengi´´´
Nikamkumbuka Mswidi aliyetuletea vipimo vya joto vya Celsius

yule Anders Celsius . Kwa kuwa yeye alikuwa anapima maji kuchemka katika 0 degree na kupoa katika 100 degrees kitu kilichofanya Carl Linnaeus aingilie kati Anders alipofariki ili kugeuza ili ijulikane maji yanachemka !00 degree na kuganda 0 degree.

Na mpaka leo hakuna anayejua vizuri kwanini aliyegundua kipimo ambacho kinakubalika sana duniani alikuwa kakipindua /kakigeuza kwa mitazamo ya wengi.

Goodman Manyanya Phiri said...

Kama ni hivyo kinyume kweli mimi sitajuwa kwanini wengi wanadai siasa nayo ni sayansi (POLITICAL SCIENCE).


Ladba tuwaachie vizazi vijao kutupatia jawabu hapo.


Aisee! Leo ni siku yangu ya kuzaliwa; na nakuomba utembelee (nakujiunga pia na) blogu yangu mpya http://ninaewapenda.blogspot.com/


Humu najaribu kuelewesha watu ukaribu walugha zetu (Kiswahili na Siswati/Isizulu/Isixhosa).

Pia najaribu niwapate wanablogu wenzangu kama wewe hapo tuwape watoto washule mawaidha ya kufaulu shuleni... mtaalam hapa hamna... na kila mmoja wetu anatoa mawazo yake kusudi Afrika isonge mbele!

Nakushukuru!