Thursday, October 6, 2011
NIONAVYO MIMI. Wapinzani "WAJISEME" kabla "HAWAJAWASEMA"
Wiki hii tumeshuhudia kwa mara nyingine "USHINDWI" katika siasa huko Igunga. Nazungumzia kwenye uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Rostam Aziz ambaye aliamua kujiuzulu nyadhifa zake ukiwemo ubunge. Kwa bahati mbaya, WOTE WALIOSHIRIKI WALISHINDWA (kwa mtazamo wangu) kuifanya siasa kama chombo cha kuihudumia jamii badala yake wakaugeuza uchaguzi huo kuwa NGAZI YA KUPATIA MADARAKA.
Ni harakati hizi zilizoleta mambo mbalimbali kuwezesha harakati za kukwaa madaraka hayo. Tumeshuhudia helikopta, fedha, "majeshi" na kila nguvu zikipelekwa Igunga kwa wiki chache ili kupata KITI hicho cha ubunge. Ni kwa mantiki hii nilipoandika kwenye ukurasa wangu wa Facebook kuwa "Mshindi kashindwa na mshindwi kashinda. Nani ni nani na ni nani aonaye ushindi wa sasa kama ushindwi ujao naye aonaye ushindwi wa sasa kama ushindi ujao? Ni LAZIMA SIASA ZETU ZIWE ZAIDI YA KUSHINDA NA KUSHINDWA. Ziwe UTUMISHI KWA UMMA.
Nasubiri kuona ni wangapi waliokuwa Igunga wiki kadhaa zilizopita watarejea "kuwajulia hali" kabla ya 2015.
Nawaza kwa sauti tuuu!!!!"
Ninalowaza ni kuwa katika uchaguzi huu wa "vuta nikuvute", na ulioshuhudia "MAJESHI" ya aina mbalimbali, ni kiasi gani cha pesa kimetumika huko? Na ni kweli kuwa matumizi hayo yataendana na kasi ya maendeleo kwa wana Igunga? Ni kweli kuwa chama tawala kimeshutumiwa na kutuhumiwa kutumia pesa na kila rasilimali iliyo ndani ya uwezo wao, lakini je, UPINZANI mmefanya nini kusuia hili lisitokee wakati ujao? Sote tumesikia matokeo [kuwa Dk. Kafumu alishinda kwa kura 26,484 sawa asilimia 50.56, mgombea wa Chadema, Joseph Kashindye, alipata kura 23,260 sawa na asilimia 44.32 wakati mgombea wa CUF, Leopard Mahona, aliambulia kura 2,104 sawa na asilimia 4.01.)Stephen Mahui wa AFP (235), Hassan Lutegeza wa Chausta (183), Said Cheni wa DP (76), John Maguma wa Sau (83) na Hemed Dedu wa UPDP (63)]
Ninalowaza ni namna ambavyo MUUNGANO WA WAPINZANI (ambao wote wanaigiza kuwa na nia moja ya kuing'oa CCM) ungeweza kuwa suluhisho (kama sio tishio halisi) kwa chama tawala. Na nia hapa si kukitisha chama kuwtwaa madaraka yake, bali kutisha kuwa kisipowajali wananchi kitakosa ama kupoteza viti vingi.
Ni kwanini hata apataye kura 63 aamini kuwa anaweza kuibadili Igunga peke yake? Kwanini asiwekeze kwenye kuvishawishi vyama kumsomamisha yeye, ama atumie kura zake 63 kuwahamasisha wengine kumpigia mmoja watakayekuwa naye?
UPUNZANI......Mna miaka minne kusawazisha haya. Sote tunajua kuwa upinzani hauko sawa nchi nzima. Ni lazima tukumbuke kuwa kuna baadhi ya sehemu ambapo vyama fulani vyakubalika kuliko kwingine. Ni kwanini chama kisicho na wafuasi wengi mahala fulani kuliko kwingine. Ni kwanini vyama hivi visisimamishe mgombea mmoja kwa mujibu wa kukubaliana walikonako? Ukweli ni kuwa bila muungano hakuna ushindi.
Narejea nilichowahi kusema kuwa "JAPO DALILI ZA MTI KUKOSA MAJI TWAZIONA KWENYE MATAWI / MAJANI, LAKINI WAKATI WA KUTATUA TATIZO HILO HATUMWAGILII MAJANI BALI MIZIZI". Ni ujinga kwa wapinzani kuamini kuwa wanaweza kuleta mabadiliko nchini Tanzania kwa kutwaa nafasi za ubunge na uRais pekee (ambao wote si watendaji wa wananchi nchini mwetu). Naamini ni wakati ambao wapinzani wanatakiwa waanze SAFARI KUELEKEA MASHINANI kueleza sera zao ambazo sina hakika kama wengi wanazijua.
Ni wakati ambao hakuna "danganya toto" ya wasanii, wala kikundi fulani. Hakuna kanga wala kofia wala sukari. Ni wakati ambao utamkuta mtu asiye na munkari wa helikopta ana anayepekeshwa na hisia za kumuona "nyota" fulani. Ni wakati huu ambao wanatakiwa kwenda kwa wananchi KAMA WAO, bila mbwembwe za HELIKOPTA na kwa kuwa kama wananchi na kuwakuta katika fikra tulivu, wataweza kuwaelimisha juu ya kile wanachopanga kufanya, kuhusu ilani zao na mipango yao na kisha itawawia rahisi KUWAELIMISHA NA KUWAELEWESHA wananchi juu ya kile wanachopanga kufanya kwa kutumia ama kupitia sera zao. Na hili ndilo ambalo WANANCHI WANAKOSA. ELIMU JUU YA MAANA, NGUVU NA THAMANI YA KURA ZAO. Narejea kunukuu "status" yangu nyingine kwenye Facebook kuwa "TANZANIA HAITABADILIKA iwapo wananchi hawajui / hawatajua MAANA, NGUVU NA THAMANI YA KURA ZAO. Iwapo hawatajua kuwa KURA NI MAKUBALIANO / MKATABA wa KUSHIRIKI katika kutekeleza (na si kukaa kutekelezewa) ahadi ambazo mgombea amezitoa. Iwapo hawatajua kuwa KURA SIO MAZOEA YA CHAMA na kuwa SI LAZIMA IENDANE NA UANACHAMA BALI SERA ZA MGOMBEA NA MAHITAJI YAO na kuwa wanaweza kumpigia kura mgombea wa chama kingine na hata kuchagua Rais, Mbunge na Diwani toka vyama tofauti KULINGANA NA SERA NA MIPANGO YA KUTEKELEZA MAHITAJI YAO.
Nawaza kwa sauti tuuu!!!!"
Novemba 4 mwaka jana niliandika kuwa AJENDA KUU YA UCHAGUZI 2015 IWE UCHAGUZI 2010. Na sasa ni wakati ambao wapinzani wanatakiwa kukaa chini na KUJIANGALIA UPYA. Kuangalia mipango yao na namna ambavyo wataifikisha na kuielewesha kwa jamii. Kuangalia NIA YAO KAMA WAPINZANI na pia kama vyama vya upinzani, kisha kuchuja washirika na wasio washirika na hapo watapata la kufanya kwa manufaa ya wananchi. Si lazima wao wachukue nchi, lakini "kuwatia jambajamba" watawala itatosha kuwa utumishi. Lakini KWANZA WAMALIZE MGAWANYIKO ULIOMO NDANI MWAO kabla hawajafikiria KUWASEMA WALIO CHAMA TAWALA kwa yale watendayo. Na ndio maana nasema NIONAVYO MIMI. Wapinzani WAJISEME kabla HAWAJAWASEMA
Na huu ni MTAZAMO WANGU kwa namna nionavyo tatizo. Natunza haki zote za kukosea na kukosolewa kwani yawezekana kuwa NAMNA NIONAVYO TATIZO NDIO TATIZO
Tuonane "Next Ijayo"
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
Bonge la MTIZAMO Mkuu!
Post a Comment