Sunday, January 15, 2012

TANZANIA YANGU......NA MAPENZI YA "MUNGU WETU" ASIYE NA MAPENZI KWETU.

Moja ya habari zilizotawala vyombo vya habari vya Tanzania na maandishi yahusuyo waTanzania ni kifo cha Mbunge wa vITI maalum kwa tiketi ya ChaDeMa, Dada Regia Mtema. Watu wengi walitoa kauli mbalimbali kuwasilisha masikitoko yao. ikiwemo sala ya kumuomba apumzike kwa amani. Lakini pia kulikuwa na kauli ambazo ni kama DESTURI itokeapo majanga haya. Kati ya mambo ambayo nayasikia saana yatokeapo majanga ndani ya Tanzania yangu ni neno MAPENZI YA MUNGU YAMETIMIZWA.
Ukweli wa mambo ni kuwa MAPENZI YA MUNGU HUTIMIZWA na huyatimiza pale aonapo panafaa. Lakini pia, ni Mungu huyuhuyu ambaye ametupa akili na maarifa ya kujifunza mambo mbalimbali yatutokeayo na kisha kutumia AKILI ZETU, BUSARA ZAKE NA UTII katika kuepusha majanga zaidi.
Lakini kwetu sisi tumekuwa TUKIMSINGIZIA MUNGU kuhusu mengi yatutokeayo na kisha kupuuza kila sababu isababishayo matatizo hayo.
Mungu nimuaminiye mimi ni MUNGU WA UPENDO. Ambaye hawezi "kutuua sisi tu" kwa kiwango tufacho na kuwaacha wale wanaojitahidi kuepusha ajali hizo. Nchi nyingi zimewekeza kwenye maisha ya wananchi wao na kuwafanya viongozi kuwa watumishi halisi wa wananchi na kutatua matatizo yao, lakini kwetu sisi ni kinyume. Tumekuwa tukiona hawa walio madarakani wakifanya kila wawezalo kuepusha majukumu hasa yale yatakayotumia muda na UWEKEZAJI (kumbuka sijasema gharama, nimesema kuwekeza kwa kuwa najua si gharama kuliko thamani ya maisha ya watu)
Nilishaandika sana kuhusu AJALI ZINAZOTUMALIZA nchini Tanzania. Na niliandika haya na bado naandika kwa kuwa mimi ni MHANGA wa ajali mbili TU kati ya maelfu zinazotokea na hasa zitokeazo nchini Tanzania. Na ninaloamini na kuendelea kusema ni kuwa VIONGOZI WETU HAWAJALI KUHUSU ATHARI ZAKE na ndio maana kila siku zinatokea na hakuna hatua za kila siku za kuzuia hili.
Kila kitokeacho, tunaambiwa ni MAPENZI YA MUNGU.
Huyu MUNGU WETU atimizaye mapenzi ndani mwetu ni Mungu gani ambaye atapenda kuona Tanzania ndio tufao kwa ajali za barabarani?
Huyu MUNGU WETU atimizaye mapenzi ndani mwetu ni Mungu gani ambaye ataacha watu wafe kwenye meli kama Mv Bukoba, Spice Islander na hizi mashua na mitumbwi kila uchao?
Huyu MUNGU WETU atimizaye mapenzi kwetu ni Mungu gani anayewasaka wale walio na mazingira machafu na kuwaua?
Huyu MUNGU WETU ATIMIZAYE MAPENZI mbona ni MUNGU ambaye si nifunzwaye wala kumuamini mimi?
Ni kweli kuwa TANZANIA TUNAYE MUNGU ATUPENDAYE AMBAYE ANATUUA KWA MAPENZI YAKE?
Lazima tukubali na tukabili ukweli.
Kuwa......
Mungu hatashuka na kutujengea barabara na kuziboresha ili ziwe na ubora na ukubwa utakaosaidia ama kuwezesha tufike salama.
Mungu hatashuka na kuhakikisha kuwa matairi yasiyo na ubora hayawekwi kwenye magari tusafiriayo
Mungu hatashuka kuhakikisha kuwa yale mabati yasiyo na ubora yanatumika kutengeneza bodi za magari
Mungu hatashuka kukataza mkono wa askari wa usalama baraarani kupokea rushwa.
Mungu hatashuka kuhakikisha kuwa idadi ya wanaostahili kuwemo kwenye meli ndio wanaopanda meli hiyo.
Mungu hatashuka kuzuia watoto wale wanaocheza kwenye mitaro ya maji machafu wasiugue kipindupindu.
Mungu hatashuka kuhakikisha kuwa ile pesa ya kujenga wodi ya kinamama ili wajifungue salama hazichukuliwi na nanilii na kutengeneza mradi wake.
Mungu hatashuka kuhakikisha kuwa yule mfamasia hapeleki dawa za jamii kwenye duka lake binafsi na kuziuza kwa bei ambayo wengi hawamudu.
Mungu hatashuka na kuhakikisha kuwa wale waliopewa kandarasi za kujenga barabara wanajenga kwa ubora.
Lakini kubwa zaidi.......
Mungu hatashuka kuwawajibisha wale ambao wamezembea kwenye ajali kama za MV Bukoba ama MV Spice Islander ama reli ya kati Dodoma ama ajali zituuzazo kila siku.
Mungu hatakuja na kututoa ndani kutupeleka kuziba madimbwi, kujaza barabara na hata kuziba mashimo yanayoachwa wazi baada ya machombo migodini ambayo kila mwaka twasikia yakileta maafa nyakati za mvua
Ninalotaka kusema hapa ni kuwa TUACHE KUMSINGIZIA MUNGU, BALI TUTUMIE AKILI NA BUSARA TULIZOPEWA NAYE MUUMBA KUEPUKA AJALI.
Mapenzi ya Mungu si sisi kufa kwa uzembe wetu.
Mapenzi ya Mungu si sisi kutowajibika kwa kuwawajibisha wasiowajibika.
Mapenzi ya Mungu si sisi kuishi chini ya tawala zinazotunyonya ilhali twajua suluhisho.
Mapenzi ya Mungu si sisi kuendelea kuitwa maskini ilhali tuna malighafi za kutosha.

Huyu si Mungu tufunzwaye, japo ndiye TUHURIRIWAYE NA WANASIASA WANAPOKUJA KUTOA SALAAM ZA RAMBIRAMBI.
Kama ni kweli kuwa huyu Mungu tunambiwaye na wanasiasa yu-hai, basi hili linanifanya niamini kuwa TUNAYE MUNGU WETU (Tanzania pekee), AMBAYE ANATIMIZA MAPENZI YAKE KWETU, LAKINI HANA MAPENZI JUU YA MAISHA YETU.
Na huyu Mungu wetu anaonekana kushika kasi katika maisha yetu ndani ya nchi yangu....
Yaani...TANZANIA YANGU, IHUBIRIYO "MAPENZI YA MUNGU WETU" ASIYE NA MAPENZI KWETU.

Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA

Tuonane "Next Ijayo"

2 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Umeliangalia suala hili kwa jicho la ndani sana. Sijui kama washikilia hatamu huwa wanapita humu vibarazani na kuona changamoto na maoni ya watu wao.

Huyu Mungu hata huko Aliko bila shaka huwa Anatikisa kichwa tu kwa kutupiwa lawama kwa kila kitu kibaya kinachotukumba sisi binadamu hata kama kinatokana na uzembe wetu wenyewe.

Dini, kama ilivyowahi kulalamikiwa na Karl Marx, yaweza kutumiwa kama kasumba tu. Kila kitu ni mapenzi ya Mungu hata kama ni matokeo ya uzembe wetu wenyewe. Basi utawaona washika hatamu hawa wakiangusha sahihi zao katika vitabu vya maombolezo na kupigwa picha nzuri zinazomeremeta wakiwa wamekaa viti vya mbele misibani. Na kiini hasa cha msiba wenyewe kamwe hakigusiwi. Vifo vinaendelea kwa sababu ile ile miaka nenda miaka rudi.

Ni kweli hakuna ambalo tunaweza kufanya ili kupunguza ajali hizi ambazo zinapukutisha maisha ya wenzetu kila leo?

Basi pengine itabidi manabii na mitume waliojaa katika makanisa yetu ya kisasa wainuke na kumtetea Mungu Anayesingiziwa kwa kila kitu!

Samahani kwa kubwabwaja. Ni mada inayogusa moyo sana !!!

Mija Shija Sayi said...

Tatizo ni kwamba tunataka mabadiliko lakini hatutaki mchakato wa kuyafikia mabadiliko, tunategemea yatashuka labda. Tatizo ninaloliona hapa Tanzania ni la Ujinga, yaani hatuna kabisa maarifa na werevu na wala hatutaki kuvitafuta vilipo. Lakini pia tutafutaje ujinga kama wafuta ujinga wenyewe hawatufuti ujinga?
Sina hakika kama wana mapenzi ya kweli na nia ya kweli ya kutufuta ujinga...

Ni hayo tu yangu.

TANZANIA YANGU NA MAPENZI YA MUNGU WETU ASIYE NA MAPENZI KWETU.