Tuesday, January 24, 2012

Tanzania yangu..."Inayokazana" kuona ilhali imefumba macho (III)

Katika sehemu ya kwanza ya muendelezo huu niliangalia namna ambavyo TANZANIA YANGU inajitahidi "kufa kupona" kuendelea lakini inapuuza ELIMU. Ukweli wa mambo ni kuwa sio tu watu wanaliona suala hili, lakini wenye mamlaka na dhamana ya kusema haya, WANAPUUZA. Na si ajabu kwa kuwa wao ni wanufaika wa hali ilivyo.
Katika sehemu hii ya pili nikaandika namna ambavyo nilisikitishwa na habari niliyoisoma nilipokuwa napitia blogu ya Kaka Michuzi ambapo nilikutana na habari hii toka kwa WAKAZI wa Block 5 na 6 ambao wamelalamikia namna ambavyo shughuli za uchimbaji mchanga zinaathiri mazingira yao. Katika sehemu ya maelezo yao, wanasema "tulikwishatoa taarifa juu ya jambo hili polisi, serikali ya mtaa, kwa mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kwa DC mwezi June. Lakini hadi hivi leo mwezi August watu hawa wanaochimba mchanga wanaendelea kuchimba mchanga na wamediriki hata kututishia sisi wananchi wa eneo hili la Mivumoni".
Lakini leo nageukia upande mwingine. Upande wa MAISHA MAGUMU YA MTANZANIA.
Leo nimesikia TAARIFA ZA MGOMO WA MADAKTARI ambapo "Miongoni mwa madai ya madaktari ambayo wanataka yafanyiwe kazi ni Serikali kuboresha huduma za afya nchini (hospitali na vitanda kwa kila mgonjwa inawezekana), kuboreshwa kwa maslahi kwa watumishi wa sekta ya afya, malipo kwa kazi za ziada kwani madktari wanalipwa sh. 10,000 kwa mkesha na kufanya kazi masaa 36 tofauti na taratibu za Serikali ambapo ilitakiwa walipwe sh. 40,000 (half pediem).
Madai mengine ni pamoja na haki ya kupewa nyumba au posho ya pango kama muongozo wa utumishi wa umma wa serikali ya Tanzania unavyoelekeza ule wa mwaka 1994 na wa mwaka 2009, kulipwa posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi (Risk allowance).
Sharti lingine la madaktari kwa Serikali ni kutaka kuondolewa kwa Katibu Mkuu wa wizara ya afya Bi. Blandina Nyoni ambaye wanadai amekuwa ni kikwazo katika juhudi za msingi katika kuboresha sekta ya afya Tanzania,"
Asiyejua umuhimu wa huduma za Afya ama Elimu kwa Tanzania ni WATAWALA AMBAO HAWATIBIWI WALA KUSOMESHA NYUMBANI. Na ndio maana sishangani kuona hawatilii maanani lile lisemwalo kuhusu sekta hizi. Ninapowaza ATHARI ZA MGOMO WA MADAKTARI na kisha kuona Rais na Makamu wake wakiwa kwenye "ziara" mbalimbali, nawaza namna wanavyowafikiria hawa watabibu na hata waathirika wa mgomo huo.
Kama inavyoonekana hapo chini,
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiongozana na mkewe Mama Zakhia Bilal, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Ludovic Mwananzila na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Lindi, wakati akikagua Daraja la Mingumbi baada ya kuzindua daraja hilo lililopo Kilwa, akiwa katika ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo ya mkoa wa Lindi jana.
Photo Credits: Michuzi Blog
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akikata utepe kuzindua rasmi Jengo jipya la Bwalo la Shule ya Sekondari ya wasichana Ilulu, iliyopo Kilwa, wakati akiwa katika ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo ya mkoa wa Lindi jana Januari 22, 2012. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Ludovic Mwananzila.
Photo Credits: Michuzi Blog
Lakini katika hili kuna jambo la kujiuliza. Ninapoona Makamu wa Rais akiwa na Mkuu wa Mkoa "AKIKAGUA MIRADI YA MAENDELEO MKOANI..." mkoani Lindi ninawaza.
1: Ni lipi analolifanya ambalo mkuu wa Mkoa (ambaye ni mwakilishi wao) hawezi kufanya?
2: Ni lipi atakalosema ambalo hawezi kuliandika likasomwa na mkuu wa mkoa?
3: Kama UKAGUZI WA MIRADI YA MAENDELEO ndio lengo pekee la ziara
(kama ilivyonukuliwa HAPA), kwanini usiwepo utaratibu utakaowawezesha "wasaidizi na wawakilishi" wa ofisi yake mikoani kufanya hivyo? Hizo pesa za kugharamia ziara ya "Mheshimiwa" Makamu wa Rais si zingetosha kukamilisha mradi mwingine?
Hivi huyo Mkuu wa mkoa anaweza kusimama na kueleza analowafanyia wananchi wa Lindi ikiwa hata MIRADI YA MAENDELEO INAMTOA MAKAMU MAGOGONI? Ni kwamba hawaaminia ama vipi?
Sitashangazwa na hili (la kutoaminiwa) kwa kuwa hata Kaka Lukwangule aliripoti hapa jinsi ambavyo Rais alipokwenda Morogoro "alibambikizwa" ripoti ya miaka 12 akaishitukia (japo sikusoma kuwa alichukua hatua) "rais anapopewa taarifa ya matumizi ya fedha halafu anahoji uhalali wake...watendaji wanapojaribu kuziba soni zao kisha wanagutukiwa,wataalamu wa uchumi wanapobabaisha na takwimu zao halafu anawashtukia.wananchi wanapomwambia rais waziwazi kwamba watendaji wake ni wazushi.Rais anaposhangazwa na kauli za watendaji ambazo walistahili kuzifanya zamani halafu wanasingizia mambo ambayo hayana kichwa wala mguu.Rais anaposhangazwa na uuzaji holela wa ardhi za watu kiasi cha kukosa akiba"
Kama haya yanatokea kwa Rais, kwanini aendelee kuwaamini "watendaji" wake?
Lakini bado swali ni lile lile, KWANINI UKAGUZI USIFANYWE NA MKUU WA MKOA AMA WATENDAJI WENGINE WA NGAZI HIYO?
Labda ni mambo ya kawaida, lakini katika hali tete ya Uchumi kama tuliyopo, nahisi baadhi ya "kawaida" zapaswa kuwekwa kando. Kama Tanzania tunataka KUONA UCHUMI WETU UKIKUA, NI LAZIMA TUBANE MATUMIZI na hatuwezi kubana matumizi ikiwa watu walio na heshima, ulinzi na wenye ziara za gharama zaidi nchini wanaweza kufanya "ZIARA YA KUKAGUA MIRADI YA MAENDELEO".
Hii ni zaidi ya UTANI.
Matumizi ya fedha lazima yabanwe kwa kuONDOA NAFASI ZA MADARAKA ZISIZOELEWEKA ZINAINUFAISHA VIPI JAMII. Na moja ya nafasi hizo ni WAKUU WA MIKOA. Niliandika HAPA nikiuliza iwapo Wakuu wa mikoa ni watumishi wa wananchi, watumishi wa Rais ama mzigo kwa serikali na wananchi? na hakuna jibu nililopata.
Maswali yangu makuu yalikuwa
1: Wakuu wa mikoa NI WATUMISHI WA WANANCHI AMA VIBARAKA WA RAIS NA SERIKALI?
2: Hivi kazi yao kubwa ni nini?
3: Wapo kama watendaji wa kuendeleza mikoa na wananchi ama kutekeleza ILANI za uchaguzi za Rais aliyeko madarakani?
4: Hivi Rais awateuaye anajua hali halisi ya uhitaji wa mikoa anayowapeleka wakuu hao?
5: Ni kwanini anawahamisha wakuu hao kabla hawajaweka misingi imara ya maendeleo huko waliko?
Wakuu wa Mikoa hawajawa na kazi inayodhihirika kwa wananchi licha ya kuwa na malipo ambayo yakisitishwa kwa wote tena kwa mwaka, yanaweza kujenga mabweni, ama kuchimba visima, ama kununua vitabu ama kulipa waalimu n.k

Lakini ndio TANZANIA YANGU, inayojaribu kuongeza mapato ikiongeza MATUMIZI YASIYO YA LAZIMA. Inayojaribu kuongeza ufanisi kwa kuongeza msururu wa watekelezaji.

TANZANIA YANGU....."INAYOKAZANA" KUONA ILHALI IMEFUMBA MACHO.

Kumbuka....NAWAZA KWA SAUTI TUUU!!!!!!!!!!!!


Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA


Tuonane "Next Ijayo"

2 comments:

chib said...

Ahsante kwa kuzungumza ukweli halisi. Tatizo lipo pale pale, ujumbe muhimu kama huu unasomwa na watu huku wakiwa wamefumba macho. Je, wanauelewa??!!
Wanahitaji kusisimuliwa na nguvu au nishati ya radi, na sio kuwashtua au kuwapiga shoti kwa umeme wa Tanesco, maana kwa hilo wameshakuwa sugu. Wanhitaji shoti ya umeme unaotoka kwenye radi ili wafumbue macho au ndio iwe kwa heri yao waje wanaojua kusoma wakiwa wamefumbua macho.

Ebou's said...

Inauma sana kwa serekali usiojali matibabu na huduma za afya huniukweli mtupu!