Thursday, March 1, 2012

Wewe ni ZAIDI YA WEWE

Mimi ni zaidi ya umuonaye pichani. Nawe pia. Isake "nguvu uliyo ndani mwako" utafanikiwa
Maswali ya wewe ni nani yanaweza kuleta mjadala mkubwa na pia kujiuliza kama umefikia kiwango cha juu cha u-wewe nalo laweza kuwa swali gumu. Lakini kuna ukweli kuwa "wewe ni zaidi ya wewe". Niliwahi kuandika kuwa tuko tulivyo kutokana na maisha yetu kutokana na maisha yetu yaliyopita na kwa ajili ya maisha yetu yajayo. Pia Kaka Bwaya na wachambuzi / watambuzi wengine wameandika kuhusu mada zihusianazo na hizi. Kaka Kaluse alishaandika juu changamoto za kufikiri vizuri na hofu ya kesho ilivyo dubwana la kutisha mambo ambayo kwa hakika yanatukwamisha katika kufikiri juu ya uwezekano mwingine wa kujaribu kuwa na maisha zaidi ya haya tuliyonayo.
Lakini ukweli halisi ni kwamba maisha yetu yanakwamiswa na namna tunavyochukulia mafanikio yetu na ama namna tunavyoogopa kusaka mafanikio zaidi ama tunavyoshindwa kuamua kujaribu namna nyingine za mafanikio pale kile tufanyacho kinapogoma. Kuogopa kwetu kujaribu (ambazo ni athari za hofu, fikra mbovu na zenye mtazamo hasi tunazojijengea) ndiko kunakotufanya kushindwa kujipa ama kusaka changamoto zaidi ambazo ni chachu ya ukuaji wa kila mtu. Nakumbuka msemo wa kikwetu usemao "kama hujala nje ya kwenu utaamini kuwa mamako ndiye mpishi bora ulimwenguni" ambao kwa tafsiri ya isiyo rasmi wamaanisha bila kukubali / japo kufikiri na kuangalia changamoto za maisha mengine, kwingine na kwa namna nyingine, utabaki kuamini kuwa umefikika kwenye kilele cha mafanikio yako. Kwa ujumla katika suala lolote, kuna kuona tatizo, kisha kulitambua na baada ya hapo kuangalia kama unataka kupata changamoto na kukua ama unataka kuachana nazo (nikimaanisha kuzikimbia changamoto) na hapo ndipo utakapoamua juu ya kuwa ulivyo, kuporomoka toka ulipo ama kuwa zaidi ya ulivyo.
Ndipo linapokuja suala la UTUMWA WA KIAKILI ambapo mawazo ya "nimeshapitwa na wakati" ama "hizo zi fani zangu" na hata "vina wenyewe" vinapokuja na kujikosesha nafasi muhimu na pengine adimu ya kuwa mtu wa pekee ulimwenguni. Nikimsikiliza Bob Marley anaposema "emancipate yourselves from mental slavery, none but ourselves can free our minds" napata maana halisi ya namna tunavyoweza kuwa zaidi ya sisi kama tutakuwa na fikra chanya juu ya kile tutakacho kutenda.
Kumbuka kila mwenye mafanikio alipitia maanguko mengi na kutokata tamaa ni sifa mojawapo ya shujaa hivyo hatustahili kukata tamaa maana kwa kuendeleza tuaminiyo, tupendayo na tutakayo tutafanikiwa tu. CHANGAMOTO ni sehemu ya maisha na kila uwazapo kitu na kukawa na uwezekano wa mafanikio basi ujue waweza kuwa hapo uwazapo kama utafanya hicho uwazacho kwa njia na mpangilio sahihi.
Ni muda wa kujitazama wewe kama wewe, kuangalia ulipo na kisha kutazama uwezo wako katika utendaji mambo, ndoto zako, na uwezekano wa kuwa zaidi ya ulipo na kisha ujiulize HIVI WEWE SI ZAIDI YA WEWE? Kama ndio basi "fuata ndoto zako"
Labda Luciano atukumbushe kuwa "trade winds will keeps on blowing, my life keeps on going, Jah's Love keeps on flowing. So i never give up my pride".


Jicho la ndani ni kipengele ambacho huangalia mambo kwa "undani" zaidi na kujaribu kutafuta suluhisho kutokana na tafakari ya tatizo. Kwa maandiko mengine kuhusu kipengele hiki, BOFYA HAPA

1 comment:

Yasinta Ngonyani said...

"WEWE NI ZAIDI YA WEWE" Nimefurahi sana kusoma hii mada kwani imenikumbusha sana baba yangu ambaye kila mara tulipokuwa wadogo alikuwa akisema. Lazima kuanzia mwanzo na ndipo utafika pazuri. Lakini hakuna hata siku moja unaweza kuanzia pazuri...Na pia ni lazima kujituma/kujitegemea na kusema mimi naweza ni muhimu sana katia kutaka kufanikiwa. Ahsante kwa kumbukumbu.