Wednesday, April 4, 2012

Brother Lusinde.....Labda ukimya ni njia bora ya kuomba msamaha kuliko ufanyalo.

Katika mafunzo yangu ya habari (tena muhula huu) nikafunzwa kuwa moja kati ya mambo yanayoweza kufanya kitu kikazungumzwa, kuandikwa ama kuonyeshwa kwenye vyombo vya habari na kutambulishwa kama HABARI ni kuwa "IT IS OUT THERE".
Na maana halisi ya hili, ni kuwa jambo linaweza kuwa "covered" kwa kuwa limekuwa GUMZO, na kuwa watu wengi wanafuatilia na wengi wangependa kujua mengi kuhusu hilo. Na kwa maana hiyo, nimeona ni vema nami nikatoa ushauri wangu kwa (aliyestahili kuitwa) Mhe. Livingstone Lusinde. Mbunge wa jimbo la Mtera ambaye katika kampeni ya uchaguzi jimbo la Arumeru Mashariki alitoa kauli mbaya sana ambazo hazikuwa na lolote lihusulo siasa wala wanaArumeru Mashariki. Kwa hakika alisikitisha.
Na leo (kama anavyoonekana hapa chini katika picha iliyobandikwa kwenye ukurasa wa Facebook wa Clouds Fm) alikwenda kwenye kituo cha Clouds Fm na kuzungumza kuhusu hilo na pia kuomba msamaha kwa kauli zake. Unaweza kusikiliza mazungumzo haya HAPA KWENYE TOVUTI YA Dada Subi.
Na namuita "aliyestahili kuitwa Mheshimiwa" kwa kuwa naamini uHESHIMiwA unakuja unapojiheshimu. Na naamini kuwa ni kejeli kumuita Mheshimiwa kwa kuwa wengi hawamheshimu kwa sasa.
Nasikitika kuiweka VIDEO HII HAPA lakini ili nitakachosema kieleweke, naomba nifanye hivyo.
NINAOMBA RADHI KWA HILI

Niliwahi kusema kuwa WAKATI MWINGINE, UKIMYA NI HOTUBA NZURI ZAIDI na naamini kama hii ndio njia pekee ambayo Bwn. Lusinde ameamua kutumia kuomba msamaha, basi ni afadhali angekaa kimya.
Bwn. Lusinde. Huwezi kutukana watu namna ile jukwaani Arumeru kisha ukaenda kuomba msamaha kwenye kituo cha radio Dar Es Salaam. Unastahili kufanya hivyo jukwaani ama uende kwenye kituo cha radio Arumeru ukaombe msamaha.
Na bado nasubiri kujua kile ambacho KAMATI YA MAADILI YA CHAMA CHA MAPINDUZI itafanya juu yake. Niliwahi kugusia suala la maadili ndani ya chama hicho nilipopata nafasi ya kuhojiana na Katibu Uenezi wa Chama Ndg. Nape Nnauye na HAYA NDIYO ALIYOSEMA

Hiviiiiiiii...Bwn. Lusinde anapoomba radhi na kusema anajutia aliyosema, wale "wafuasi" waliokuwa wakishangilia maneno yake wanajifikiriaje? Hawakujua walikuwa wakishangilia yasiyostahili ama walijua na yalistahili ila Lusinde kawasaliti?
Na.......
Ni kweli kuwa angeomba radhi iwapo wangeshinda? Ama ndio angesema "wamewazalia" watoto aliotabiri watazaliwa Aprili mosi?

Ukweli wa mambo ni kuwa Bwn. Lusinde ulikosea, na umefanya vema kuomba msamaha, ila msamaha huo, haujauomba vema, kwa hiyo umefuta nia njema ya kufanya lililo jema.
Na kama hiyo ndio njia pekee ambayo utatumia kuomba msamaha.......Labda ukimya ni njia bora ya kuomba msamaha kuliko ufanyalo.

1 comment:

chib said...

Hotuba hii..... ni sawa na mtu kutembea hadharani bila kuvaa nguo