Sunday, May 6, 2012

THAMINISHA.......Voice Of America


Kwa wale wanaofahamu historia ya ULEVI wangu wa kazi, wanatambua kuwa imekuwa safari ndefu sana. Safari ambayo wengine nilioanza nao walishabadili fani na (kulingana na tafsiri yao na / ama yangu juu ya neno MAFANIKIO) wapo ambao wamefanikiwa huko waliko. Lakini kwa ufupi, fani ya utangazaji niliipenda tangu nikiwa mdogo. Nakumbuka nikiwa na miaka kama 7 nilikuwa mpenzi mkubwa wa vipindi vilivyokuwa vikisikika Radio Tanzania. Nawakumbuka nyota wengi waliojenga mazingira ya mimi kuipenda fani (ambao wengi walielezwa kwenye POST HII) Lakini ndoto ya kufanya kazi radio haikutimia mpaka zaidi ya miaka 10 baadae, pale nilipopewa nafasi ya kujaribu nipendacho na Kaka Taji Liundi (mimi humuita Mzee wa Vipaji). Alinipa nafasi ambayo niliipenda kwa miaka, na huo ukawa mwanzo wa kilichopo sasa.
Studioni Times FM 
Nikiwa Times Fm, nikaanza na vipindi vya michezo kisha nikahamia kwenye kipindi cha SUNRISE na baadae kuongeza Matukio ya wiki. Katika kuandaa vipindi hivyo, nikajikita zaidi kwenye HABARIZA KIMATAIFA. Huko nikawa nasikiliza Idhaa za nje kuona wanavyojipanga ili nami niboreshe kazi. Na nikapendezwa zaidi na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika. Nakumbuka mwaka 2002 nilianza kuwaandikia barua pepe kuwaeleza ninavyovutiwa na kazi zao na kuwaeleza ninavyotamani kuja kukaa meza moja nao nikifanya kazi pamoja nao. ILIKUWA NDOTO. Kwa wakati huo sikuwa na ndoto wala njozi za kuja Marekani na hata sikuwa katika fani ya habari. Nilishajikita kwenye UKEREZAJI VIPURI na nia kuu ikiwa kuja kuwa MHANDISI. Miaka miwli baadae, nilikuwa hapa Maryland na nikiwa katika manunuzi ya vyakula na mwenzangu katika "section" ya maharagwe, tukawa tunajadiliana kati ya aina zilizopo ni ipi yenye "rojo" kama ya nyumbani. Tulikuwa tukizungumza kiswahili na ghafla nikasikia mtu akitusalimu kwa kiswahili na kusema ametusikia tukiongea kiswahili na kutambua kuwa tulikuwa tukitoka nchi moja. Ilikuwa ni mshtuko wa furaha na tulisalimiana na kujitambulisha na alipojitambulisha yeye ndipo nilipogundua kuwa aliyesimama mbele yangu alikuwa si mwingine bali ni Mzee Jerome Danford Kassembe. Mtangazaji ambaye kwa miaka mingi nimekuwa nikimsikia "akiunguruma" kupitia IDHAA YA KISWAHILI YA SAUTI YA AMERIKA hapa Washington DC. Nilijitahidi kuwa mtulivu (maana nilishazidiwa na furaha) lakini sikutaka kumuacha aondoke bila kujua kuwa utangazaji ni kati ya vitu ninavyopenda saaana na ningependa kujua wao wanafanyaje. Akasema wala hilo halikuwa tatizo na akanipa kadi yake na pia namba ya simu ya ziada na kuniambia siku yoyote nitakayopanga kwenda basi nimjulishe ili awe mwenyeji wangu. HIYO ILIKUWA KAMA TIMIO LA NDOTO KWANGU. Ni kweli. Nilimpigia simu na kupanga ziara ya kwanza VOA

Ziara ya kwanza VOA. Toka kushoto ni Mr Kassembe, Mr Mwamoyo Hamza, Mr Emmanuel Muganda, mimi, Mr Vincent Makori na Mr Aboudshakur Aboud
Hii ziara ilikuwa ya MAFANIKIO saana kwangu. Nilipata wasaa wa kuzungumza na timu nzima iliyokuwepo na TOFAUTI NA NILIVYOZOEA KWA WATANGAZAJI WENYE HADHI KUBWA NCHINI, wala hakukuwa na majivuno. Hapo akili za kurejea kwenye fani zikaanza kutinga na japo zilichukua muda kushika kasi, lakini ziara hiyo iliniunganisha saana na fikra za kile nipendacho. Nikaanza kuzifanyia kazi. Nikaweza kupata ziara za mara kwa mara pale na kila mara kujifunza mambo mapya kuhusu fani. Lakini funzo kuu zaidi lilikuja nilipopata nafasi ya kufanya mazoezi ya vitendo pale. Niliweza kujifunza mengi kuhsu utayarishaji wa vipindi, umuhimu wa muda na hata ubora. Kuanzia kuandika, kuhariri (kabla ya kuhaririwa), mpangilio wa habari, na mengine mengi. Na zaidi ni namna ambavyo watu wa Idhaa nyingine walinipokea na kunisaidia kukua katika fani. IDHAA YA KIINGEREZA KWA AFRIKA ilikuwa na imekuwa sehemu kubwa ya kile ninachoona kama mafanikio kwani kuwasikiliza, kuwafuatilia na kisha kupokea maoni toka kwa wakongwe kama Shaka Ssali, Vincent Makori, Ndimyake Mwakalyelye, Paul Ndiho, James Butty, mtayarishaji Nicole Lindsey na wa waandamizi wa idhaa waliniwezesha "kufunguka" zaidi katika fani. Na kwa hakika ilikuwa faraja sana kushirikiana nao
 
Dada Ndimyake Mwakalyelye, mimi na Kaka Vincent Makori. Hosts wa InFocus ya VOA 
Na bado nilikuwa nikifunzwa kazi na Mkuu wa Idhaa Mwamoyo Hamza, Esther Githui-Ewart, Abdushakur Aboud na Khadija Riyami ambao wote niliwaandikia wakati huo, na pia nyongeza ya Mary Mgawe, Mkamiti Kibayasi, Sunday Shomari na watayarishaji Aida Issa na Dwayne Collins
Da Aida Issa, mimi na Sunday Shomari punde baada ya kipindi cha KUMEKUCHA AFRIKA 
Na ni mafunzo haya ambayo sasa yameniwezesha KUJIAMINI katika fani, KUWA BORA kwenye nitendalo (hasa shuleni),na KUFANIKIWA katika harakati zangu binafsi katika kazi nje ya shule. Na yote haya natambua kuwa yasingekuwa yalivyo iwapo watu wa SAUTI YA AMERIKA (ambao hawakulazimika kuwa wakarimu kama ambavyo walikuwa) wasingefungua  
Ndani ya studio za kurekodia za Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya America ambako kwa miezi sita nilijifunza mapya. Moja ya mengi ni sehemu ya ushiriki wangu siku ya mwisho ya mazoezi ya vitendo  

 ASANTE SANA SAUTI YA AMERIKA. 
Nilijifunza, najifunza na nitaendelea kujifunza mengi toka kwenu 

  **THAMINISHA ni kipengele kinachounganisha makala ama matoleo mbalimbali ya watu mbalimbali wanaojitolea kuboresha maisha ya wengine na hata wale wanaoona vema kuthaminisha yale waliyotendewa na wengine. Kwa matoleo zaidi BOFYA HAPA**

2 comments:

Rachel Siwa said...

Hongera sana mzee wa Changamoto,asante kwa Changamoto, nimejifunza meengi sana kwenye hili.Mungu azidi kukubariki.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

safi sana ndugu kwa hili nakuonea wivu sana aisee