Sijawahi kuhusika na mwisho wa maisha ya mwanadamu kama ilivyotokea hivi karibuni kwa Kaka Domitian Rutakyamirwa.
Na katika kuhusika huku, (tangu kuugua mpaka harakati zilizofuata baada ya kifo chake) nimegundua na kujifunza mengi kuhusu mtu, utu na watu.
Ni kwa kupitia maisha ya mwisho ya Kaka Domi, nimeweza kujiakisi na kuakisi mengi yanayoendelea katika maisha yetu wanadamu na kuweka bayana “ndivyo-sivyo” ya maisha yetu.
Binafsi nimeshuhudia maisha yangu yakikaribia kifo tena cha ghafla katika matukio tofauti na bado sikuona ama kujifunza nililojifunza sasa.
Nakumbuka kauli ya mwisho niliyoisikia ikitoka kinywani mwa Kaka Domi ni ile ya kutubu aliyoongozwa na Mchungaji akiwa wodini.
Katika matukio yote niliyokumbana nayo, na ambayo wenzangu baadhi walipoteza maisha, hakuna kati yao aliyepata nafasi ya kutubu na kumuomba Mungu kama alivyofanya Kaka yangu huyu.
Na kama alivyohubiri Mchungaji kwenye ibada ya mazishi, mambo makuu matatu aliyosisitiza ni kuwa…
1: Hatujui tutaondoka lini.
2: Hatujui tutaondokea wapi.
3: Hatujui tutaondoka vipi
Domitian, aliyekuwa Kaka, rafiki, Mume, mzazi na mlezi kwa wengi aliishi maisha ambayo yamekuja kudhihirika katika wakati wa uhitaji wake.
Maisha ya Domi yamedhihirisha UMOJA unaotamaniwa na waTanzania hasa wa Washington DC na vitongoji vyake ambao kwa namna moja ama nyingine unakwamishwa na mambo mbalimbali, lakini pale inapotokea tofauti zetu zikawekwa kando kwa ajili ya mtu aliyekuwa nasi sote licha ya tofauti zetu, tunaona matunda ya umoja. UMATI unaojitolea kufanikisha jambo kwa namna ya kipekee sana.
ASANTENI NYOTE
Nimejifunza mengi katika kuzungumza na watu walioshiriki katika harakati za kumuuguza kaka yetu huyu.
Nimekutana na wengi ambao kwa kuwa tulikusanywa pamoja katika kumhudumia Kaka yetu, utaendelea kuwa pamoja.
Nimewajua (hasa kitabia) wengi ambao katika harakati hizi za kuuguza mpaka kukabiliana na changamoto za msiba wameweza kuonyesha uhalisia wao. Watu ambao sikuwahi kudhani kuwa wanajitoa kama walivyojitoa na wale ambao sikujua kuwa wana fikra pevu hasa katika mambo nyeti kama haya.
Nimejua sehemu na taratibu ambazo sikupata kuzijua mpaka wakati huu ambao nimeunganishwa na watu wazijuazo, lakini yote ni katika kushughulikia “pumziko” la Kaka Domi.
Labda Domi hakujua kila nilichojifunza, lakini maisha aliyoishi yamemuunganisha na watu ambao kila mmoja ana KARAMA tofauti, na kwa umoja wa karama hizo, tunapata kujifunza zaidi na kuishi kwa uraisi zaidi.
Labda Domi hakufahamiana na kila aliyebariki moyo wangu kwa KARAMA aliyonayo, lakini alijihusisha na watu ambao walikuwa wema kiasi cha kuhusiana na wema wengineambao walikuwa ushuhuda kwenye maisha yetu.
Nilipata kusema kuwa “japo waweza kumsifia Mama yako kwa kila chema kilichotokea maishani mwako, lakini pia usisahau kumsifu Baba kwa kumchagua Mama mwema, na kumshukuru Mungu kwa kukuleta katika muunganiko huo wa wazazi wako”
Kaka Domi alijihusisha na wengi wema, ambao nao wanahusiana na wengine wengi wema, na wale wema wa Domi walikuja kufarijiwa na wema wao ambao wametuunganisha nasi ambao kwa hakika tumejifunza mengi.
Kaka yetu Domi AMEANZA MAISHA MAPYA, na katika kufifia kwa maisha yake ya mwili, ametuachia mfano, ama angalizo la namna tunavyotakiwa kuishi. Kwa kuwa wema, kujihusisha na walio wema, kutokuwa sehemu inayogawa watu, ili hata wale wenye upinzani na kutoelewana, wakutane na kuwa wamoja wanapokutanishwa nawe (ukiwa hai ama mfu).
Na ni katika makutano haya, tunapopata ujumbe huu wa maisha yetu tuliopewa kwenye mahubiri ya Mchungaji Ferdnand Shideko ambayo yalionekana kugusa wengi, na wengine kwenda kukiri kuwa WAMEONDOKA WAKIWA WAPYA KULIKO WALIVYOKUJA.
Mwanga wa maisha yako umefifia Kaka Domi, lakini kwa kufifia kwako, umetuunganisha na wengi, tumesikia ya wengi na TUMEPATA MWANGA ZAIDI WA NINI LA KUFANYA NA NINI LA KUEPUKA.
Ulale palipo pema peponi.
7 comments:
Mungu amlaze pema peponi... Mungu huyo aliyekufanya ufanye uchambuzi huu azidi kukutia moyo ili uendelee kuelimisha kondoo zake
Mungu amlaze pema peponi... Mungu huyo aliyekufanya ufanye uchambuzi huu azidi kukutia moyo ili uendelee kuelimisha kondoo zake
Pumzika kwa amani kaka Domitian!
R.I.P Domitian, na pole sana kwa wafiwa!
M/Mungu aileze roho ya marehemu mahala pema peponi....Bandio ndio ukubwa huo, na tutajifunza mengi tugali bado tunaisha na hilo ni somo tosha kwa mwanadamu. nakupongeza sana wewe pamoja na jamii nzima kuwa bega kwa bega mpaka kukamilisha mpango mzima wa kuusafirisha nyumbani mwili wa Ngudu mpindwa Domi. NINAWEZA KUSEMA You 're the Man!
Ohhh kaka wa mimi Poleni sana sana,pia nami nimejifunza meengi sana kupitia hapa.
Raha ya milele umpe eeh BWANA.............Kaka Domi ulale kwa Amani!!!
Post a Comment