Monday, September 3, 2012

"Injinia" MIMI na ukarabati wa "nyumba TANZANIA"

PHOTO CREDITS: Cool fun pics
TANZANIA YANGU.
Naitazama Tanzania na matukio kedekede yanayoikumba.
Natazama namna ambavyo inazidi kumomonyoa imani na matumaini kwa wananchi.
Labda wananchi hawajui ukweli na wanaendeshwa na TETESI.
Lakini LABDA wenye kujua ukweli hawajali kuhusu TETESI zinazoiharibia sifa ya kweli nchi yangu.
Kila siku ni matukio, na kila matukio ni KUUNDIWA TUME na kila tume inahusisha wataalamu ambao kwa mujibu wa sheria wana haki ya kuwemo kwenye tume licha ya kuwa WAMO KWENYE MFUMO ULIOHUSIKA KIMAKOSA.
Ni vigumu sana kuunga tume huru nchini bila kuhusisha sehemu ya mfumo uliohusika katika kosa linaloundiwa tume.
Lakini hii haimaanishi kuwa WENYE MADARAKA WANATUMIA MADARAKA YAO VIBAYA.
Linamaanisha kuwa wenye madaraka wamepewa madaraka kuliko wanayostahili.
Ndio nchi yangu TANZANIA.
Ambayo pia naitazama kama NYUMBA ambayo sisi wananchi ni wakaazi na rasilimali zeti ni mali zilizomo ndani.
Ni nani mwenye jukumu la kuijenga Tanzania yetu iwe bora na makini?
Ni sisi wananchi. Wakaazi wa "Tanzaniani" na hata wale waliotoka "ndani" kwenda kusaka riziki nje lakini wanajua kuwa watarejea "nyumbani"
Jambo moja muhimu la kutambua ni kuwa, KABLA HATUJAIJENGA NYUMBA IITWAYO TANZANIA, NI LAZIMA TUIBOMOE. MSINGI WAKE UMEHARIBIKA HIVYO UKARABATI WOWOTE USIOHUSISHA MSINGI NI KUPOTEZA MUDA NA PESA NA MSINGI WOWOTE UTAKAOKARABATIWA BILA KUVUNJA KILICHO JUU NI MIUJIZA.
Ni LAZIMA tuubomoe msingi wa nchi, kisha tuijenge upya.
MIMI na WEWE tuna wajibu mmoja. Kujua ni vipi tutaweza kuibomoa nchi sasa bila kuathiri "watu na mali" zilizo ndani kwani tusipofanya hivyo, "mali na watu" hao wataangukiwa na kuta na kuwa hasara zaidi mbele.
TUCHUKUE HATUA....HATUA SAHIHI...HATUA MAKINI.
  • Tukibomoa kwa umakini, tutapunguza gharama na hata baadhi ya vifaa vya ujenzi vitaweza kutumika tena.
  • Tusisubiri MJENZI aliyeijenga kwa makosa atuambie kuwa alikosea. Lakini tusimpuuze na kutomshirikisha kwenye ukarabati huu.
  • Tusimtishe kuwa tutamfunga kwa makosa ya ujenzi wake lakini tuhakikishe kuwa anajua kosa lake na halirudii tena.
  • Tusitafute sifa kwa kumshutumu mjenzi wa sasa na kusahau kutafuta SIFA ZA ATAKAYEKARABATI.
MWISHO....
Tukumbuke kuwa NI RAHISI KUBOMOA.
Na hata asiyeweza kubeba hata tofali, asiyejua kusoma ramani, asiyefahamu kuchanganya saruji na mchanga na hata asiyejua KWANINI TUNATAKA KUBOMOA anaweza kuwa m'bomoaji mzuri....LAKINI SI MJENZI.
Ninalomaanisha ni kuwa...SI KILA MWENYE UJUZI WA KUBOMOA ATAWEZA KUJENGA.
Tuibomoe Tanzania ili tuweze kuijenga, lakini kabla hatujaibomoa, tuhakikishe tuna mtu sahihi, mwenye ujuzi sahihi, vifaa sahihi, mpango sahihi na maelezo ya muda sahihi atakaotumia kuijenga Tanzania yetu.
La sivyo, ukarabati utakuwa mateso zaidi ya nyumba mbovu tuliyokuwa nayo.

Nawaza kwa sauti tuuuuuu!!!!!!!!!!


Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA


Tuonane "Next Ijayo"

No comments: