Monday, December 24, 2012

KUELEKEA KRISMAS.......Naitamani zamani


Labda ni akili zangu, lakini naona uwiano kati ya mazuri na mabaya ya kile kiitwacho maendeleo unaonekana kunufaisha zaidi upande wa mabaya.
Lakini "MAENDELEO" ya sasa ni yale ambayo watu wanafanya kile walicho na UHURU nacho, hata kama hakina manufaa kwao.
WanaIGA hata yasiyoigika kwao kwa kisingizio cha UHURU NA HAKI hata kama ni cha athari kwao.
Haya ni baadhi ya mambo yanayonifanya niuchukie U-SASA na ndio maana naitamani zamani.
NAITAMANI ZAMANI ambayo sherehe kama Krismas na Idd zilimaanisha uchaji wa kiroho zaidi na kukua kwa mauzo ya bidhaa ziendanazo na masuala ya kidini na sio kama ilivyo sasa ambapo sikukuu hizi ni "fashion-show" na ongezeko la mauzo ni kwenye nyama choma, chips, kondom na oda za vyumba kwenye guest houses.
NAITAMANI ZAMANI ambayo sio tu maisha yalikuwa na unafuu, lakini ambayo tulijawa IMANI baina yetu, UTU, MSHIKAMANO na hata UPENDO.
NAITAMANI ZAMANI ambayo familia zilijaliana na si kubaguana na kuchujana kama ilivyo sasa kwa vigezo kama kipato na muonekano wa wanafamilia.
NAITAMANI ZAMANI ambayo Baba yangu alienda kusomea ualimu kwa kuwa alikuwa na wito na sio sasa ambako wengi wanapelekwa kusomea ualimu kwa kuwa hawakufaulu vema. Zamani ambayo Mama yangu alienda kwenye uuguzi kwa kuwa ana wito na si kwa kuwa alitegemea kupata pesa nyingi ama kwa kuwa hakufanya vema shuleni. (Thanx to them. They're my Forever Heroes)
NAITAMANI ZAMANI ambayo TENDO LA NDOA lilikuwa na maana sawa na jina lake na si sasa ambako linatumika "KULAZIMISHA UHALALI WA NDOA" na kuonesha urijali na utendaji kazi wa "wapendanao" kama sio kuonesha "ustahimilizu" wa mikikimikiki baina ya wajinga katika jamii.
NAITAMANI ZAMANI ambayo watu walijisitiri sehemu za siri tu na hilo halikuwa tatizo walipoangaliana na hawakubakana na hakuna aliyetumia hicho kama kisingizio cha kuhalalisha tabia zao za UZINZI na UASHERATI tunayosikia watu wanasema kuwa inatokana na mavazi ya kinadada.
NAITAMANI ZAMANI ambayo teknolojia ilikuwa yenye nia ya kuboresha maisha na sio sasa ambayo yazidi kuwekeza katika saratani (cancer) zijazo. Kila kitu ni mionzi na kila muonzi una athari na tunasema "tunaendelea"
ZAMANI ambayo hatukuwa na njia nyingi za kurahisisha utendaji kazi na kutembeleana lakini tulipata muda mwingi wa kuonana na kujuliana hali na sio sasa ambako kila mtu yuko "busy".
NAITAMANI ZAMANI ambayo hatukuwa na madaktari wengi kulingana na idadi ya watu na hata madawa hayakuwa utitiri kama sasa lakini ulimwengu ulikuwa na afya njema kuliko ilivyo sasa.
NAITAMANI ZAMANI ambayo tulikuwa na silaha za kutulinda na hatari na si sasa ambako silaha ni matoleo ya kila mwaka kama magari na hazileti usalama zaidi ya ongezeko la hofu.
ZAMANI ambayo tulikuwa wazi "kudumisha fikra za Mwenyekiti" na sio sasa mabko mwenyekiti na watawala wenzake wanadumisha fikra zao kwa mgongo wetu.
NAITAMANI ZAMANI ambayo tulikuwa na "wataalamu" wachache waliojitahidi kila kukicha kujenga kilicho bora kwa nchi yetu na si sasa ambako utaalamu unaweza kupimwa kwa kuangalia ni kiasi gani umeweza kujinufaisha ndani ya muda mfupi uliokuwa kazini z9hasa serikalini). Yaani kuwa na wataalamu wengi ni kuongeza matatizo mengi
NAITAMANI ZAMANI ambayo watu walijitahidi kuongeza maisha katika miaka tuishiyo na si sasa ambako tunahangaika kila kukicha kuongeza miaka katika maisha mafupi tuishiyo.
NAITAMANI ZAMANI ambayo tuliona SIASA isiyo VISA NA MIKASA na ulafi, wizi, uchoyo na ujinga wa kunyonyana uliopo sasa.
ZAMANI ambayo tulikuwa na warembo halisi weeengi japo hatukuwa na mashindano utitiri ya urembo.
NAITAMANI ZAMANI ambayo ukikutana na binti mrembo ungesema umekutana na mtu na sio sasa kukutana na plastiki zilizobandikwa nyusoni mwa watu kwa gharama za juu kuwafanya wawe wanavyodhani wanaweza kuwa.
NAITAMANI ZAMANI ambayo tulikuwa na vyakula vichache vyenye uchunguzi mdogo wa kujua nini kilichomo ndani mwake lakini tukawa na lishe bora na si sasa ambapo tuna vyakula vingi vyenye maelezo mengi na afya ni mbovu kuliko maelezo.
NAITAMANI ZAMANI ambayo watu walijua kuwa kuna maendeleo yetu na "wao" wana maendeleo yao na sio sasa ambako kila chao ni chema na ni maendeleo na kilicho chetu ni cha kupuuzwa.
NAITAMANI ZAMANI ambayo kama ungepata ajali ungesafishwa kidonda na msamaria na si sasa ambako watakimbilia kusafisha mifuko na pochi.

Yaani naitamani zamani japo najua kuwa zamani hiyo mimi na wewe tusingeweza kuwasiliana tuwasilianavyo sasa, japo tungeweza kusakana na kuongea haya badala ya kupitishiana hapa changamotoni.
Naitamani zamani jamaniiiiiiiiiiiiiiiiiii!!!!!!!!!!!!!!!!!!

Tuonane Next Ijayo

1 comment:

Mzee wa Changamoto said...

Nkanku.
Nashukuru kwa kutumia muda wako kupita hapa na kuacha maoni.
Nathamini sana maoni yako.
Happy holiday