Thursday, December 13, 2012

Ya Rais Kikwete na Ray C.....TULENGE SHABAHA

Wiki hii, moja ya habari njema zilizoihusu fani ya muziki Tanzania ni ile iliyohusu "kupona" kwa msanii aliyepata umaarufu sana ukanda wa Afrika Mashariki Bi Rehema Chalamila anayejulikana zaidi kama Ray C.
Rehema ambaye alikuwa ameathirika kwa madawa ya kulevya amenukuliwa kuwa alikwenda IKULU kumshukuru Rais Kikwete "kwa msaada wa matibabu wakati alipokuwa mgonjwa hivi karibuni.
Rehema aliyefuatana na Mama yake Mzazi Margareth Mtweve na Dada yake Sarah Mtweve alimweleza Rais kuwa afya yake imeimarika na kwamba muda si mrefu atarejea jukwaani kukonga nyoyo za mashabiki wake.
Kwa apande wake, Mama Mzazi wa Ray C amemshukuru Rais Kikwete kwa kuokoa maisha ya mwanaye na vilevile ametoa wito kwa watu wanaokusanya michango kwaajili ya mwanaye waache kufanya hivyo kwani matibabu ya Ray C yamegharamiwa na Rais."
Picha zote kwa hisani ya Freddy Maro wa Ikulu.
Hii ilikuwa na bado ni HATUA NZURI kwa uongozi wa nchi kupambana na matumizi ya madawa ya kulevya.
Alilofanya Rais lina faida sasa japo FAIDA KUBWA ITAKUJA IWAPO NAFASI HII ITATUMIWA VEMA.
"Msaada" wa Rais Kikwete umedhihirisha kuwa MATUMIZI YA MADAWA YANATIBIKA na kuwa ni jambo ambalo linapingwa na hata ngazi ya juu ya uongozi wa nchi.
Kwa Ray C kutangaza kuwa "afya yake imeimarika" ni TANGAZO tosha kwa wale wanaohisi kuwa umaarufu wao unawatia aibu kujitangaza, hakuna kosa kufanya hivyo.
Lakini pia limekuwa na udhihirisho kwa wale waliomuona Ray C katika hali ya matumizi na sasa kuweza kukubali kuwa kuna tofauti kubwa uwapo mtumizi na uachapo na ukweli ni kuwa muonekano wa sasa wa Ray C ni mwemza zaidi ya taswira zilizomuonyesha akiwa anatumia madawa ya kulevya
TATIZO......
Tatizo litakuwepo iwapo kilichotokea kitaishia kwenye taswira tulizoziona mitandaoni. NAAMINI kuwa ili juhudi za Mheshimiwa Rais Kikwete ziwe na manufaa, huu ni wakati ambao serikali kuu inaweza kumtumia Ray C kama BALOZI WA KUPINGA MADAWA YA KULEVYA. 
Sote tunajua uwezo wa Ray C jukwaani (na kwengine tunakumbuka uwezo wake mkubwa zaidi alipokuwa radioni), na sote tunatambua kuwa ana uwezo wa kuvuta mashabiki lukuki vijana ambao ndio waathirika wakubwa wa madawa ya kulevya nchini.
NI WAKATI AMBAO SERIKALI INAWEZA KUMALIZIA MATIBABU HAYO YA RAY C na kisha kumuandalia mkakati mzuri wa kuzunguka nchi nzima KUFUNZA VIJANA KUHUSU MADHARA YA MADAWA YA KULEVYA.
Kwa kumtumia mtu huyu ambaye alishakuwa nyota, akaharibikiwa kiasi cha kukaribia kufa na kisha kurejea katika hali njema, kutakuwa USHUHUDA KAMILI wa maisha KABLA, WAKATI NA BAADA ya matumizi ya madawa ya kulevya.
Na naamini
Kwa ushuhuda atakaoutoa Ray C, vijana wengi wataweza kubadilika. Kisha vijana hao nao watumike kama atakavyotumika Ray C kubadili vijana wenzao.
CHANGAMOTO YETU katika tatizo hili ni kujua kuwa TUKIO LA RAIS KUMSAIDIA RAY C NI KAMA UPANGA UKATAO PANDE MBILI, na ni sisi wa kuamua wapi na vipi ukate. Makali ya upanga huu ni namna tutakavyoamua kutumia nafasi hii pekee tuliyonayo kwa ufasaha.
AMA tujikate wenyewe kwa kulipa gharama na kuokoa mtu mmoja kisha tumuache aende zake..
AMA tumtumie yeye, kumpa ajira ya kufunza na kubadilisha ambayo sio tu itamnufaisha yeye, bali na vijana wengine walio katika matatizo haya, ama walio katika HATARI ya kuingia humo. TUMTUMIE RAY C KAMA CHOMBO, TULENGE SHABAHA ILIYO MBELE YETU, ILI KUWEZA KUPUNGUZA TATIZO LA MADAWA NCHINI TANZANIA.
Na huu ni Mtazamo wa namna nionavyo tatizo.....labda namna nionavyo tatizo ndio tatizo

1 comment:

Emmanuel said...

Kaka umesema yote kwa njia iliyo bora kabisa. Bila shaka Mh atapatiwa huu ushauri mwanana ili akaufanyie kazi