Tanzania yangu ni kati ya nchi ambazo tunaweza kusema kuwa zinajenga mahusiano makubwa na hai na nchi ya Marekani.
Tukumbuke kuwa marais watatu waliopita wa Marekani wameitembelea Tanzania wakiwa madarakani.
Na hivi sasa, kuna ujio wa Rais Barack Obama nchini Tanzania ikiwa ni kama "majibu" ya ziara ya Rais Xi Jinping wa China aliyeitembelea Tanzania kama nchi ya kwanza katika nchi tatu alizotembelea ikiwa ni siku 10 tu tangu aingie madarakani. Na akiwa nchini Tanzania, Rais Jinping alisaini mikataba 16 inayohusu Biashara, Utamaduni na diplomasia.
Kwa mujibu wa CNN, kuna wafanyabiashara wa kiChina zaidi ya 8,000 nchini Tanzania ambao wanajishughulisha na biashara mbalimbali kuanzia magenge (kiosk) mpaka makampuni makubwa ya kandarasi.
Na sasa, Rais Obama amekwenda Tanzania kwenda kuhamasisha mahusiano ya kibiashara baina ya nchi hizi mbili.
Lakini kubwa zaidi, Rais Obama amekwenda Afrika akiwa na lengo kubwa la kuhimiza mkakati wa kuongeza nishati kwa bara hili ambalo licha ya harakati za kusaka maendeleo, ni theluthi moja tu ya wakazi wake wenye nishati ya umeme.
Katika mpango huo, Obama aliyeambatana na wafanyabiashara wa Marekani anahimiza uwekezaji (na sio msaada) ambao utawanufaisha wafanyabiashara hao na waAfrika kwa ujumla.
Lakini kama alivyosema Jonathan Berman alipohojiwa na NPR, wafanyabiashara wengi wa Marekani wanasita kuwekeza barani Afrika kutokana na mambo mbalimbali ikiwemo MIUNDOMBINU, UTAWALA WA KISHERIA, NA MAZINGIRA YA BIASHARA HAYAJARASMISHWA
Na hilo ndilo hasa ninalotaka kuzungumzia hii leo.
TANZANIA YANGU ina nafasi kubwa ya kufanikiwa katika biashara iwapo ITAAMUA KUWAJIBIKA NA KUTUMIA VEMA USHINDANI WA UWEKEZAJI UNAOFANYWA NA NCHI HIZI MBILI kubwa.
Ushindani huu wa uwekezaji nchini mwetu unaweza kuwa BARAKA iwapo tutakuwa na wazalendo katika nafasi za kusimamia uwekezaji huu, lakini pia utakuwa LAANA iwapo wale wenye mamlaka wataamua kujinufaisha.
Kichwa cha "bandiko" hili kinasomeka "Tanzania yangu....Na mkono "usioaminika" ndani ya KOPO LA HAZINA" si kwa kuwa ninapenda kuwa mtazamo hasi kuhusu hili, bali kwa kuwa TUNA HISTORIA YA KUTOTUMIA VEMA HAZINA TULIZONAZO.
Tuna historia ya kutowajibisha wale waliotuletea HASARA
Tuna historia ya kutoona mianya ya mafanikio na maendeleo iliyo mbele yetu
Leo hii, TANZANIA INATAJWA KAMA NCHI YENYE HAZINA KUBWA YA NISHATI na hilo pekee linaweza kuwa MKOMBOZI WA MWANANCHI
Lakini hili si la uongozi tu.
WANANCHI NI LAZIMA WAKUBALI KUTHUBUTU, WAKUBALI KUFUATA SHERIA NA KUJARIBU KILICHO CHA TOFAUTI.
Licha ya matatizo ya uongozi, bado wananchi tumekuwa WAZEMBE na wenye kupenda NJIA ZA MKATO katika harakati za kuelekea mafanikio ya nchi yetu.
Hii ni nafasi kubwa kwetu waTanzania kusonga mbele.
UKWELI NI KUWA, kopo hili la HAZINA (uwekezaji) liko mbele yetu, na ni sisi tusioaminiana katika "mkono unaotumbukizwa humo" kujua kilichomo.
Tuliyaona Angola.
Tunayaona Kongo.
Hatutaki kuyaona Tanzania.
HAZINA IWE BARAKA NA SI LAANA.
Katika kumalizia "bandiko hili", narejea ONYO alilotoa Rais Obama katika HOTUBA KUU KUHUSU ZIARA YAKE BARANI AFRIKA katika Chuo Kikuu cha Cape Town kuhusu WAJIBU WA SERIKALI KUFANYA KILA IFANYALO KWA MANUFAA YA WANANCHI akisema "History tells us that true progress is only possible where governments exist to serve their people, and not the other way around."
Na naamini historia ya nchi yetu itadhihirisha ukweli huu kutokana na yale yanayoendelea katika sekta ya uwekezaji.
Mungu Ibariki Tanzania.
Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA
Tuonane "Next Ijayo"
1 comment:
Kweli mkuu, najiuliza hivi kweli kuna `uhuru' ...nawaza tu!
Post a Comment