Thursday, August 15, 2013

Justine Kalikawe....Miaka 10 baada ya maziko yake

Tarehe kama ya leo, miaka 10 iliyopita, niliandika HABARI yangu ya kwanza na kuituma katika gazeti la Spoti Starehe. Ilikuwa ni siku nilipotoka kwenye maziko ya msanii maarufu wa Reggae Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla, Justine Kalikawe.
Habari hii haikuchapishwa gazetini, lakini nafurahi kuwa nikingali na habari hii (kama ilivyotumwa) na katika kuadhimisha miaka kumi ya maziko ya Justine, nimeona ni vema kuirejea

Na MUBELWA BANDIO. Bukoba.
15/08/2003
Safari ya mwisho ya Justine, nyumbani kwake Kitendaguro Bukoba

Maelfu ya wakazi wa mji wa Bukoba na vitongoji vyake alhamisi wiki hii walijitokeza kuusindikiza mwili wa mwanamuziki mkongwe na mahiri katika miondoko ya Reggae Afrika Mashariki Justine Kalikawe ulipokuwa ukizungushwa mjini hapa kabla ya kuelekea nyumbani kwake Kitendaguro kwa mazishi.

Wakazi hao walioonekana kujawa na huzuni, walijipanga kando ya barabara za mji wakati gari lililotangulia msafara uliobeba mwili wa marehemu Justine lilipokuwa likipiga nyimbo zake zenye hisia kali na ujumbe mzito kwa jamii hali iliyofanya wengi wao kushindwa kujizuia na kuangua vilio.

Kalikawe aliyefariki dunia jumatano ya wiki hii katika hospitali ya mkoa wa Kagera mjini Bukoba alipopelekwa baada ya hali yake kugeuka ghafla usiku wa jumanne alizaliwa tarehe 28.08 1967 nyumbani kwao Kitendaguro nje kidogo ya mji wa Bukoba akiwa mtoto wa 7 kuzaliwa kati ya 8 wa familia yao na alipata elimu yake ya msingi darasa la kwanza hadi la nne katika shule ya msingi Kibeta mwaka 1974-1977 na kuendelea darasa la tano hadi la saba katika shule ya msingi Muhimbili jijini Dar-es-salaam alikohitimu mwaka 1980. Mwaka 1981 alichaguliwa kujiunga na shule ya Sekondari Tambaza ambako alihitimu kidato cha nne mwaka 1984 na kubahatika kuwa mmoja kati ya vijana 4 waliochaguliwa kujiunga kufanya kazi katika kiwanda cha kusafisha mafuta cha TIPER cha jijini DSM, kazi aliyoianza mwaka 1985 kabla ya kuiacha kwa hiari yake mwaka 1986 na kujitosa rasmi katika fani ya muziki.

Mwanamuziki huyo ambaye alikwishatoa albamu 8 za audio na 3 za video katika miaka 16 aliyodumu katika muziki wa Reggae, amekuwa kielelezo kizuri cha muziki na utamaduni wa mkoa wa Kagera kwani baadhi ya albamu zake aliziimba katika lugha ya kihaya hali iliyomfanya ajikusanyie mashabiki wengi katika ukanda unaozunguka Ziwa Viktoria, na wakati mauti yakimkuta alikuwa katika maandalizi ya kuzindua albamu yake mpya aliyoirekodi hivi karibuni.

Alifanya ziara za kimuziki katika nchi za Zambia (1988) na Denmark mwaka huu.

Justine aliyelelewa na mama yake Ephrazia Kashebo (71) baada ya baba yake mzazi kufariki akiwa na umri wa miaka (1971) ameacha mke Georgia na watoto wawili wa kike Abayo (7) na niwe(4) na alizikwa nyumbani kwake Kitengule Alhamisi saa 10 jioni kwa taratibu za madhehebu ya Orthodox.

Kifo chake ni pigo jingine katika sanaa ya muziki hapa nchini na ndani ya familia yao baada ya kaka yake aliyekuwa mpiga disko mashuhuri hapa nchini Dj Kalikali aliyefariki mwaka 1991.

Atakumbukwa kama mtetezi wa wanyonge na mpigania haki, amani na utulivu katika jamii, na msanii aliyekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya UKIMWI na zaidi atakumbukwa kwa vibao vyake kama Roho ya Korosho, Wamachinga, Watu, Maisha na vingine vingi vilivyotamba.

MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU JUSTINE KALIKAWE MAHALA PEMA
*************
Niliporejea Dar nikakuta HARAKATI za kuandaa Tamasha la Kumuenzi Justine Kalikawe.
Tukiwa Idara ya Habari Maelezo (2003) na Ras Pompidou, Jah Kimbuteh, Ras Inno, Bi Georgia (Mjane wa Justine) na meneja wake wa zamani Allen Mbaga kuzungumzia Tamasha la HAKUNA lililomuenzi Justine
Nikaungana na FAMILIA ya wanaReggae maarufu Tanzania katika kutengeneza video ya wimbo HAKUNA (ambayo haikutoka / sikubahatika kuiona)
Nikiwa na baadhi ya wasanii walioshiriki wimbo ulioitwa HAKUNA (urejee hapa)Hapa ni ndani ya (iliyokuwa) Bacyard Studio tulipokuwa tumekwenda kurekodi Video ya wimbo huo uliokuwa maalum kumuenzi Justin Kalikawe
Unaweza kuusikiliza hapa chini


Moja ya kazi za Justine Kalikawe nilizokuwa nazipenda (na bado nazipenda) ni ile aliyoiimba kwa lugha na midundo ya nyumbani Bukoba.
Wimbo unaitwa NOIJUKA ambao unazungumzia maisha ya utoto (ama niseme ya zamani) na namna ambavyo kama waHaya tuliishi kabla ya kuingia kwa "u-sasa" ulioondoa utamaduni wetu
Ni MAISHA YETU YA KIJIJINIIIIIIIIII
"Ego ninyijuka amakir'Ago"

No comments: