Friday, October 25, 2013

Mawazo ya Waziri Muhongo hayana tija wa wizara yake- Mengi


mengi2
Mkutano wa pili wa kimataifa wa masuala ya uendelezaji wa nishati ya mafuta na gesi ulimalizika alhamisi jijini Dar es salaam Tanzania ambapo ulijumuisha serikali, taasisi za umma na makampuni mbali mbali.
Mwenyekiti wa taasisi ya sekta binafsi nchini Tanzania (TPSF) Dkt. Reginald Mengi ambaye alikuwa ni mmoja wa watoa mada akizungumza na Sauti ya Amerika kuhusu pendekezo lake la kusitishwa ugawaji wa vitalu amesema hilo halikufanikiwa kwasababu kinachompa shida ni kwamba hakuna sera ya kugawa au kutoa vitalu.
Aliongeza kuwa wakati huo huo vitalu hivyo vinatolewa kwa wawekezaji wa kigeni, alihoji katika mkutano huo kuwa inakuwaje wagawe rasilimali za taifa bila sera maana ukifanya hivyo ni uporaji tu.
Alisisitiza kwamba mtanzania hafaidiki na hajaona chochote cha kusema kwamba mtanzania atawezeshwa kwasababu sheria ya mwaka 2004 inasema wazi wazi kwamba watanzania watawezeshwa kumiliki uchumi wao.
Kuhusu mazungumzo yake na katibu mkuu wa wizara ya nishati na madini Bw. Eliakimu Maswi amesema hakukuwa na makubaliano ya aina yeyote ni mazungumzo tu , na tunapoendelea kuzungumza vitalu vinauzwa , kwahiyo haoni kama kuna nia njema kushirikisha wazawa wa Tanzania katika sekta ya gesi hasa katika ugawaji wa vitalu.
Kutokana na kauli iliyotolewa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, Dkt Mengi amemshauri arudi darasani akafundishe kwasababu anavyofikiria watanzania siyo wanafunzi wake darasani akiongeza kuwa mawazo yake hayana tija kwa wizara anayoongoza na wafanyabiashara wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Dkt.Mengi waziri huyo alikaririwa na vyombo vya habari nchini humo akisema kuwa wafanyabiashara wa kitanzania wanajua biashara ya kuuza juisi tu jambo ambalo alisema ni tusi.
Mkutano huo ulifanyika kutokana na hatua ya hivi karibuni ya kugundulika kwa mafuta na gesi nchini Tanzania. Waziri Muhongo akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni alisema hakuna Mtanzania mmoja mmoja atakayemiliki kitalu ila watanzania watawakilishwa na TPDC.
Kusikiliza mahojiano hayo ungana na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika kwa kubofya hapa.

No comments: