Wanafunzi wa kidato cha nne wako kwenye mitihani yao ya kumaliza elimu ya sekondari
Wakati watahiniwa hawa wakiendelea kusaka "UFUNGUO WA MAISHA" yao, bado mjadala mkuu nje ya vyumba vya mitihani kuwahusu wao si kuhusu mitihani wanayofanya, bali kuhusu MKANGANYIKO KUHUSU KUFUTWA na kisha KUREJESHWA kwa DARAJA LA SIFURI katika matokeo ya mitihani yao.
Wala sina mpango na hilo, maana SIO TATIZO KUBWA KATIKA ELIMU YETU.
Tatizo kubwa lipo kwa wale wanaosoma, wanachosoma, wanavyosoma na matokeo ya kipimo cha wanachosomeshwa.
Mei 13, 2010 niliandika bandiko lenye kichwa kisomekacho Tunapofelisha kizazi kwa kufaulisha mitihani ambalo ndani mwake kulikuwa na aya zisomekazo "mifumo iliyojengwa na waalimu wetu (ambao yawezekana wamejengewa na waalimu wao) ni kuwa unastahili kupata daraja fulani ili uonekane umefaulu. Na ndio maana msisitizo hauko kwenye kuelewa na kuweza kutumia elimu katika maisha na kutatua matatizo ya jamii, bali ni katika kufaulu mtihani kwa kupata maksi kadhaa.
Tusemeje kuhusu WASOMI wetu wa IDARA YA MAWASILIANO IKULU? Unadhani hawakufaulu? Unadhani kuna sehemu yahitaji watu "waliofaulu" vema kama sehemu nyeti kama hizo? Umeshajiuliza wafanyalo huko? Basi SOMA HAPA ama HAPA uone WAFAULU MITIHANI HAWA WANAVYOLIFELISHA TAIFA KWENYE MAMBO NYETI KAMA MAWASILIANO HUKO IKULU
Na pia nimekuwa nikiona maswali meengi kuwa "kwanini wahandisi wa Tanzania hawabuni vitu vya kuisaidia jamii wakiwa nyumbani" na nahisi hili ndilo jibu lake. Kuwa waandisi ambao wamekuwa na alama nzuri darasani na kutunukiwa vyeti mbalimbali kuonesha UFANISI DARASANI lakini wanapoingia kwenye "ulimwengu wa kazi" inakuwa ni shughuli nyingine kabisa kwani wafunzwacho kwa nadharia hakionekani kuwa halisi kwenye utendaji wao. Ni hapo waajiri wanapoanza kusaka kama waajiriwa wao wana vyeti visivyo halali ama walipata matokeo hayo isivyo halali. Lakini mwisho wa siku ni kuwa WALIFUNZWA KUFAULU MITIHANI NA SIO KUFANIKISHA KAZI WASOMEAZO."
Sasa nikirejea kwenye mjadala wa leo... TUANZE KWA KUANGALIA NAMNA ELIMU YETU INAVYOTUFAA Elimu ya Tanzania imeshindwa kumfanya mTanzania kuitumikia jamii yake kutokana na alichofunzwa ndani ya nchi yake kwa MTAALA wa nchi yake, uliotengenezwa maalum kwa ajili yake.
Kwa ufupi ni kuwa...TUMEJITWIKA UKOLONI na kuwafunza watoto kisicho na manufaa kwao.
Achilia mbali wanachofunzwa...ANGALIA WANAVYOFUNZWA.
Kwa kuwa kifunzwacho hakina mahusiano ya moja kwa moja na mazingira yetu ya kiTanzania, ZAO PEKEE LA ELIMU YETU NI KAZI NA MAZINGIRA YA KIKOLONI.
Elimu yetu haimuandai mtu kuyakabili maisha ya mahala alipo. Na ndio maana mtu anayemaliza elimu yake Rubafu ama huko Kasulu ama Nanjilinji anaweza kuishi vema kwa kubangaiza ndani ya Dar Es Salaam kuliko kule aliko"gradueti"
Umejiuliza kwanini?
Kwa kuwa ELIMU YETU IMEWATENGENEZA WATAHINIWA KUWA TEGEMEZI WA MFUMO WA KIKOLONI.
Na kwa kuwa kifunzwachwo chaweza kutopatikana katika mazingira tuliyopo, mfunzwaji anatumia nguvu za ziada kukielewa.. Na hilo lanirejesha kwenye lile bandiko la awali kuwa katika elimu yetu, "msisitizo hauko kwenye kuelewa na kuweza kutumia elimu katika maisha na kutatua matatizo ya jamii, bali ni katika kufaulu mtihani kwa kupata maksi kadhaa." Na ndio maana, wale wanaofanya vema, si kwamba wanajua yanayoendelea katika jamii ya kiTanzania, bali WALIOJITENGA NAYO KUWEZA KUJUA KISICHO CHAO.
UKWELI NI KWAMBA........
Wale wanaofanya vema ni wale ambao wanatumia muda mwingi kutofanya lolote zaidi ya kusoma / kukariri mambo ambayo HAYATAISAIDIA JAMII YA MTANZANIA MOJA KWA MOJA.
Na......
Wale wenye majukumu na shughuli za kiTanzania wanashindwa kukariri wafunzwalo na mwisho wake wanaonekana wamefeli.
Lakini....
Naamini kuwa YULE ambaye anajihusisha na jamii akingali anasoma, anakuwa na UJUZI NA UZOEFU wa yale yanayoendelea katika jamii. Na kwa "KUJICHANGANYA" na jamii, kuisaidia jamii, kuwa sehemu ya matatizo na suluhisho la jamii....ANAFELI.
Lakini bado tunajua fika kuwa wale watakaomaliza kidato cha nne, ukampata yule wa DIVISION ONE na wa DIVISION V/O kisha ukawapeleka TANZANIANI (namaanisha kule ambako asilimia kubwa ya waTanzania wanaishi) na kuwaweka ukitaka wawe sehemu ya suluhisho la matatizo ya jamii, wale wanaohitaji msaada kutoka kwa waTanzania wenzao, basi UTAGUNDUA KUWA YULE ALIYELAZIMIKA KUJITENGA NA JAMII YAKE ILI AFAULU HIYO "DIVISION ONE" ATAKUWA NA UWEZO MDOGO WA KUMSAIDIA MTANZANIA KUTATUA MATATIZO YAKE.
Ninalomaanisha ni kuwa.....
Kufaulu kwa wanafunzi wetu kunawalazimu wajitenge na masuala ya jamii yetu, wajitenge na matatizo na hata suluhisho la jamii yetu, kwa kuwa MASOMO HAYAAKISI MAHITAJI YA MTANZANIA
Na ndio maana nasema......
Nionavyo mimi..... KiTanzania.....labda atakayepata "Division One" ndiye atayekuwa amefeli zaidi.
1 comment:
Umegusa kwenye sehemu nyeti sana kuhusu elimu itolewayo Tanzania. Cha msingi ni kwamba elimu yetu imekosa madhumuni. Jiulize ni nini madhumuni ya elimu itolewayo katika shule za Tanzania? Bila madhumuni kila jambo linaishia shaghalabagala.
Kimsingi elimu hujengwa kufuatia miono mine ya kielimu. Kwanza, ni elimu inayomfanya mwanafunzi kuelewa mazingira yake (matatizo na opportunities) iliaweze kuyatatua na kuzitumuia opportunities zilizopo. Pili, ni elimu inayojali uelewa wa nadharia na vitendo ili wanafunzi waweze kuwa wagunduzi wa nyanja mbalimbali za kuitatulia jamii matatizo yake. Tatu, ni elimu inamfundisha mwanafunzi kutambua kuwa jamii kama ilivyo inamapungufu na kumpa mwanafunzi mbinu za kuyaondoa mapungufu yaliyopo katika jamii yake. Na nne, ni elimu inayompa mwanafunzi mbinu chanya (skills)ili aweze kuitumikia jamii kama ilivyo bila kuuliza maswali magumu kuhusu mapungufu mbalimbali yaliyopo katika jamii yake.
Kwa kifupi elimu itolewayo Tanzania haijajengwa katika msingi wowote wa kielimu. Kihivyo imekosa muelekeo wa dhati. Kama tunataka wanfunzi waweze kujielewa, tunahitaji tuwafundishe jinsi ya kujielewewa. Ni makosa makubwa kwa elimu inayotolewa Mwanza kuwa sawasawa na elimu inayotolewa Dodoma. Mazingira ya sehemu hizo mbili hayalingani. Kwahiyo kimaoni yangu nafikiria kuwa elimu yetu inahitaji kukidhii mahitaji ya jamii inamotolewa. Lakini hili si kweli kwa elimu itolewayo Tanzania sasa hivi.
Kwa upande wa mitihani. Sina hata la kueleza kuhusu hili. Kuna aina nyingi sana za jinsi ya kuutambua uelewa wa wanafunzi. Cha ajabu ni kwamba tunatumia mitihani ya kupima ukariri na elimu finyu. Kiasi kwamba mitihani utumiwayo imekosa muelekeo katika upimaji.
Kila la kheri kwa hili Bubelwa.
Post a Comment