Wednesday, May 13, 2015

Zaidi ya $1,500 zachangishwa Canada kusaidia maafa ya hali ya hewa Tanzania

Kwa hisani ya SwahiliVilla Blog
Jumuiya ya Wazanzibari waishio nchini Canada (ZANCANA), imechangisha zaidi ya Dola 1500 za Canada kwa ajili ya waathirika wa hali ya hewa nchini Tanzania.
Wanajumuiya ya ZANCANA wakipata picha ya pamoja baada ya ibada ya dua maalum ya kuwaombea walioathirika na mvua za masika, nchini Tanzania
Katika taarifa yake ambayo Swahilivilla imeipata nakala yake, Zancana imesema kwamba mnamo tarehe 9 Mei, 2015, jumuiya hiyo iliandaa mkutano maalum wa wanachama wake katika jiji la Toronto nchini Canada.
Mkusanyika huo uliofanyika katika ukumbi wa Zancana, ulifunguliwa kwa ibada maalum ya kuwaombea na kuwakumbuka ndugu jamaa na marafiki waliokumbwa na maafa ya hali ya hewa katika maeneo ya Pemba, Unguja na Dar-es -Salaam.
Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa, baada ya ibada, mawaidha na dua, kilifuatia chakula maalum kilichoandaliwa kwa ajili ya uchangishaji wa fedha kwa lengo la kuwasaidia wahanga wa mvua za masika katika maeneo ya Unguja na Dar, na waathirika wa kimbunga katika eneo la Kisiwapanza kisiwani Pemba.
Taarifa ya Zancana imemalizia kwa kusema kuwa, bado michango inaendelea kupokelewa, na kuwaomba wale wote wenye moyo na uwezo kuchangia kwa kupitia accounti inayopatikana katika tovuti yao ya www.zancana.org

No comments: