Friday, March 26, 2010

Ninapowaza KUWAOMBEA VIONGOZI wapate matatizo

NIMECHOSHWA NA MAUMIVU NIHISIYO KILA NIONAPO AJALI NA NINA HAKIKA KAMA VIONGOZI AMA WENYE MAMLAKA WANGEKUWA WAMEHUSIKA KATIKA AJALI KAMA TULIZOPITIA NA KUWA NA MAUMIVU KAMA NILIYONAYO (NA WAHANGA WENGINE), WANGEFANYA JAMBO LILILO NDANI YA UWEZO WAO KUZUIA WINGI WA AJALI HIZI.
Picha zote mali ya FRANCIS DANDE wa Michuzi Blog
Kuna wakati ambao unajikuta ukiwaza visivyowazika ukiamini kuwa NDIO SULUHISHO PEKEE la matatizo tele.
Bushman aliwahi imba "in order for one to survive, sometimes you gotta take another one's life"

Najua kuwa leo ilistahili kuwa siku ya BURUDANI ya muziki wa Reggae ili kuifunza, kuielimisha na kuikomboa jamii kutoka katika utumwa wa kiakili, lakini habari iliyobandikwa jana juu ya ajali imenitibulia wiki yangu.
Ni hapa ninapokuja kujihisi nikikubaliana na msemo kuwa AISIFIAYE MVUA, IMEMNYEA. Na mimi kwa kuona taswira hizo hapo juu nimerejewa na machungu ya kinachowakuta wengi pale wanapopatwa na ajali. Najua kwa kuwa nami ni mhanga wao. Nimeandika saana kuhusu ajali iliyonikuta zaidi ya miaka 10 iliyopita na ambayo bado naendelea kuuguza athari zake. Januari 24 mwaka jana nikaandika kuwa Tumechoshwa na SALAMU ZA RAMBIRAMBI. Na sasa hatuzitaki. Na hii ni kutokana na kutokuwepo kwa sera ama mipango maalum ya kupunguza ama kuzuia ajali zitokeazo kila siku.
Tunaloona ni VIONGOZI KUTOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI kisha wasihimize kinachotakiwa kuhimizwa kusaidia kuzuia ajali hizo.
June 15 2009, SHIRIKA LA AFYA DUNIANI (WHO) lilitoa ripoti yake juu ya takwimu na usalama katika barabara ilionesha kuwa watu 34.3 katika kila watu 100,000 wanapoteza maisha nchini Tanzania ilhali wastani wa dunia ni watu 18.8 kati ya watu 100,000.
Jikumbushe alivyoinukuu Kaka Faustine (hapa)
Wamiliki wana magari ambayo hayastahili kuwa barabarani.
wamiliki wanatumia madereva kama vibarua na hawana mikataba nao.
Wamiliki hawawajibiki na tabia za madereva waendeshao magari ambayo yanabeba ama kupishana ama kutumia njia moja na magai ya abiria.
Wamiliki wa magari hawakamilishi matengenezo na kulinda VIGEZO muhimu juu ya ubora wa "mabati" yatumikayo kutengeneza bodi za magari.
Na bado, SERIKALI HAIFANYI LOLOTE. Sheria inasema hakuna kusafiri alfajiri mapema na usiku lakini tumeona kilichotokea hapo juu.
Nakumbuka mwanzoni mwa miaka ya 2000, kulikuwa na wimbi la ujambazi wa kutumia silaha na polisi walionekana kushindwa kudhibiti mpaka waliouawa askari wenzao tukaona nguvu halisi walizonazo. Walifanya "operesheni" ambayo iliathiri majambazi na mpaka raia wanaosemekana kuwa wema wakifanya biashara zao za madini.
Kisha tukashuhudia ajali zikiendelea kuteketeza watu na viongozi "kutoa salamu za rambirambi" mpaka pale wimbi hilo lilipohamia kwa viongozi wakuu ambapo serikali ikaamka.
UKWELI NI KUWA WATENDAJI WA SERIKALI WANASTAHILI KUAMKA ILI KULINDA MAISHA YA WANANCHI (AMBAYO NI KAZI YAO KUU) NA PIA MAISHA YAO WENYEWE NA WAPENDWA WAO.
Na kama wao kuwa sehemu ya tatizo ndio njia pekee ya kupata suluhisho, basi na iwe hivyo.
Narejea kusema kuwa NIMECHOSHWA NA MAUMIVU NIHISIYO KILA NIONAPO AJALI NA NINA HAKIKA KAMA VIONGOZI AMA WENYE MAMLAKA WANGEKUWA WAMEHUSIKA KATIKA AJALI KAMA TULIZOPITIA NA KUWA NA MAUMIVU KAMA NILIYONAYO SASA, WANGEFANYA JAMBO KUZUIA AJALI HIZI.
Mpumzike kwa amani. SEE YOU IN ZION

10 comments:

Fadhy Mtanga said...

Kipaumbele cha serikali ni pesa za uchaguzi na safari.

Mungu atunusuru!

Fadhy Mtanga said...

Kipaumbele cha serikali ni pesa za uchaguzi na safari.

Mungu atunusuru!

Fadhy Mtanga said...

Kipaumbele cha serikali ni pesa za uchaguzi na safari.

Mungu atunusuru!

Yasinta Ngonyani said...

Labda ni kweli kama kiongozi mmoja angepata ajali hili jambo lingechukuliwa mkazo. Na pia inawezekana madereva wetu labda wanakuwa na haraka sijui? Maana unaposafiri unaomba mungu tu ufike salama. Lakini kiongozi akisafiri anasindikizwa na magari meeengi na kila kitu kinasimamishwa. Hata mimi nimechoshwa na hizi ajali.

Anonymous said...

cha kushangaza hakuna hata magari ya uokoaji, zimamoto hawana lolote ikabidi ikodishwe gari ya mtu binafsi kunyanyua lori la mafuta, pesa serikali haina ila inazo za kupeleka watu kufungua matawi ya ccm ulaya, kukarabati nyumba ya gavana kwa bilioni, nina hakika gavana asingekufa kukaa nyumba ya zamani, nasikia hiyo sehemu kuna kona na daraja halafu eti kuna dereva aliyetaka kuovertake, dereva akipatikana na hatia ni kuhukumiwa kifo kwa kuua kwa makusudi, labda kama ni taahira na aliyempa gari kama ni taahira afungwe maisha,hizi picha zinasikitisha poleni walala hoi wenzangu

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

aisee, sijui niseme nini ila sitolia

Kitoto said...

Kuna haja ya wanahabari na waelemishaji jamii wote kuungana na kuanza kampeni kabambe kuhusiana na udereva wa kizembe, rushwa, magari yasiyofaa kuwa barabarani, nk. Mpaka jamaa wa nchi jirani zilizokuwa mbovu zamani kutuzidi, leo wameanza kuulizia mitaani Ulaya: "Oh nasikia ajali za magari zimezidi kwenu Matizedi."
Hii si aibu? Tanzania nchi ya amani imegeuka nchi ya ajali za vipanya, fuko na nzige? Kampeni yaweza kufanywa hivi. Wanahabari, waandishi, waalimu na waelemishaji kupiga kelele, kuungana kukemea hili tatizo. Mbona UKIMWI umekemewa (Oh vaeni mipira na soksi) ; mbona wanasiasa wabovu (mafisadi) wanasemwa...vipi vibaka wanapigwa hadi wakauawa kwa kuiba nyanya mbili sokoni? Kwanini dereva anayekimbiza kipanya cha "Hiace" hadi akaua hakemewi na waandishi na wale wenye "mikono" ya waelemishaji na vyombo vya habari? Mbona abiria wanakufa na tai, wanajikaza kisabuni; wanakubali eti ajali na uzembe huu eti ni sehemu ya majaaliwa ya " Ubongo" na "Wanabongo"?

Mhanga said...

binadamu wengine tumezidi kulalamika..tukumbuke katika ajali kuna mipango ya mungu na kuna uzembe wa binadamu....na huo uzembe wa binadamu muda mwingine unaoka na tabia au ujinga wa binadamu na sio kuilaumu serikali moja kwa moja...zipo ajali ambazo zinatokea tunaweza kusema ni kutokana na serikali....TUKITAKA KUKOMESHA AJALI KWANZA TUANZE KWA SISI WENYEWE ABIRIA.

Abiria mnapokuwa ndani ya gari na mkagundua kuwa dereva anakwenda speed sana kwanini msimfokee na kumshitaki kwa matrafiki walioko njiani??? abiria 65 mtashindwaje na watu 2?? dereva na kondakta??

Na kuna ajali kama ya juzi ni uzembe tu wa madereva...labda serikali ifanye utaratibu mmmoja kwamba MTU YOYOTE ANAETAKA LESENI APATE MAFUNZO KWENYE VITUO VINAVYOTAMBULIKA NA SIKU YA KUPATA LESENI BASI ZOEZI HILO LISIMAMIE NA MATRAFIK WENYEWE NDO WATOE LESENI NA KUPATA LESNI IWE SIKU HIYO HIYO MTU AKIPASI, NA HAO MATRAFIC WANAOKULA RUSHWA KWA MADEREVA WAZEMBE WAFICHULIWE NA WANANCHI AMBAO WANAWAONA KANDO KANDO YA BARABARA..ni wakati wa WANANCHI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI NA SIO KUILAUMU KWA KILA JAMBO....

Mzee wa Changamoto said...

Shukrani kwa wote.
@Mhanga. Kama ulivyosema ni kuwa wananchi wanastahili kuwa mstari wa mbele kupigania hili. Lakini umeshawahi kuwa miongoni mwa abiria wanaojaribu kufanya hilo? Binafsi nimewahi. Na ni kwa kuwa nilikuwa naogopa kutokewa na kile kilichonitokea miaka kadhaa kabla.
Kwanini naamini serikali ina sehemu ya lawama?
Kwanza haisimamii MIKATABA kati ya madereva na wamiliki wa magari. Walitakiwa wawe wanafanya random audiring kwenye mabasi na kuwachukulia hatua za kweli wamiliki ambao hata hawajui aendeshaye gari ni nani.
Serikali imepiga marufuku magari kama hayo ya mizigo kuwa barabarani mapema (muda ambao ajali hiyo imetokea). Jiulize ama subiri uone kama kuna litakalomkuta huyo mwenye lori ambaye ndiye mwenye dhamana ya kujua kuwa amemkabidhi gari dereva mtiifu atakayefuata sheria.
Subiri uone kama serikali itasaidia wananchi wahanga wa ajali hiyo kupata FIDIA za kuwapoteza ndugu zao kwa uzembe wa lori. Huyo mwenye gari akilipishwa fidia kubwa, bima yake itam'bana kuhakikisha harudii hilo.
Serikali haiangalii ubora wa magari yaliyo barabarani. Iwe ni bodi, breki, matairi na hata uwezo wa kubeba ilichobeba.
Serikali HAIWAJIBIKI katika kile kisichoiathiri yenyewe ama wahusika wake wakuu. Ninakuhakikishia kama kwenye hiace angekuwepo mkubwa yeyote ungefanyika uchunguzi na isingechukua masaa zaidi ya 3 kuja kutoa lori juu ya hiace. Natumai una kumbukumbu ya kilichotokea Mv Bukoba. Sitaki ata kukumbuka namna ambavyo UJINGA na TAMAA YA PESA vilivyosababisha maamuzi yaliyosababisha vifo vyote vile.
Kama ingekuwa nchi ambazo serikali inawajibika, ingefanyika autopsy na kama ineonekana kuna aliyekufa muda mrefu baada ya ajali, basi serikali ingeshitakiwa kwa uzembe uliosababisha kifo chake.
Suala hapa ni kuwa pesa zilipwazo na wenye magari zinaelekezwa wapi badala ya kusaidia vifaa vya uokozi na matibabu kwenye sehemu ambazo "highways" zetu zinapita?
Tatizo linalosababisha yote haya ni RUSHWA IIMUNG'UNYAYO JAMII.

Anonymous said...

tatizo la usafiri na ajali zitakuwa kero hadi usafiri utakapokuwa ni wa serikali madereva waajiriwe na serikali, vinginevyo magari binafsi ni ushindani, kukimbilia abiria na kukimbiza gari ili kupata watu mapema, kukataa wanafunzi kutojali hali ya gari kwakuwa ni kupoteza muda wa kupata watu, na pia mwenye gari ndio anatafuta dereva na jinsi ya kulipana,enzi za railway dereva alikuwa dereva gari ikiharibika hakorokochoi anapiga simu mafundi wa railway waje watengeneze muda ulipangwa na yalikuwa hayakimbizwi hovyo ajali zilikuwa finyu tena si za kutisha.hivi dsm kuna watendaji kazi wa serikali?na wabunge je? tena wao ndio wangepiga kelele jinsi watu wanavyoteketea kwa ajali, uzembe, rushwa au kwa kuwa wao hawana taabu familia zao wanamashangingi, hawana habari na wanaominywa na malori masaa kadhaa hadi kufa, sijui nani atasikiliza kilio cha walala hoi