Monday, April 23, 2012

Tanzania yangu nyuzi 360. Ni kama hadithi ya kuku na yai

Japo kuwa nilikuwa nimeahidi kuweka bandiko jingine hii leo, wacha "nitoe hili kifuani" mwangu. Disemba 7 2009 niliandika post yenye isemayo KABLA YA KUWA WAO WANAKUWA SISI....NI SISI WA KUBADILIKA (irejee hapa) ambapo sehemu ya post hiyo ilisomeka ikiuliza 
"JE!!!!! Tunajiona tuna nafasi gani ya kutekeleza mafanikio ama kubeba lawama ya lile linaloendelea nchini mwetu? 
Ni kweli twatambua kuwa VIONGOZI TULIONAO WALIKUWA WANANCHI KABLA HAWAJAWA VIONGOZI? 
Ni kweli twakumbuka kuwa TABIA MBAYA walizonazo viongozi wetu (rushwa, ufisadi, kutojali wananchi, kujilimbikizia mali nk) ni tabia wanazojifunza na kuziona wakiwa WANANCHI KABLA HAWAJAWA VIONGOZI? 
Labda la kukumbuka ni kuwa, KABLA YA KUWA WAO (VIONGOZI), WANAKUWA SISI (WANANCHI) HIVYO NI WAJIBU WA KUIBADILI JAMII ILI KUWEZA KUBADILI UONGOZI" 
Kubwa hapa lilikuwa kueleza kuwa kama hatutamfundiaha mtto nidhamu ya matumizi ya umma, usitegemee akaja kuijua na kuitekeleza akishakuwa kiongozi. Kama tusipoonyesha sasa kuwa uchaguliwapo unawajibika kwa waliokuchagua, tusitegemee wakalitambua hilo baada ya uchaguzi. NIMEAMUA KUZUNGUMZA HAYA kutokana na yaliyotokea hivi karibuni ambayo yanaonyesha ama kudhihirisha kile nilichowahi kuandika kuwa Bado naamini WATAWALA hawa wanahitaji somo la awali la uRaia (irejee hapa)
Leo hii, Mhe. Rais wangu atakuwa Blantyre nchini Malawi kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Bingu wa Mutharika. Rais ameelekea huko siku moja baada ya kuwasili kutoka Brazil na kisha kuomboleza kifo cha Brigedia Jenerali Mstaafu Adam Mwakanjuki.
Kilichonifanya niwaze ni kuwa
1: KWANINI RAIS AENDE KUMZIKA MTU AMBAYE HAJAWA NA MCHANGO MKUBWA NCHINI TANZANIA NA AMBAYE ANAKABILIWA NA TUHUMA NYINGI ZA KUENDESHA NCHI KINYUME NA MAADILI NA KUPUUZA MAZISHI YA MWANAJESHI MSTAAFU ALIYEITUMIKIA NCHI TANGU ENZI ZA AFRO SHIRAZ PARTY? Ni kweli kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi asingeweza kuwa mwakilishi tosha?
2:  Ni nani anayejali AFYA YA RAIS na kumuacha apige safari hizi za kila uchao na ZISIZO NA MASLAHI KWA TAIFA ilhali tunakumbuka kuwa uchovu wa safari ulishasababisha akaanguka wakati wa kampeni zilizopita?
Sishangai, kwani ni Rais huyuhuyu ambaye alienda kwenye msiba wa msanii na kusema ameahirisha safari. Ni Rais huyuhuyu aliye kiongozi wa nchi ambayo Bunge lake lilisemekana kusimama dakika moja kwa heshima ya Kanumba licha ya kuwa hawakusikika kufanya hivyo kwa watu kama Prof. Haroub Othman ama Prof Chachage.
Ni bunge hilohilo lenye wabunge ambao wanawatetea wananchi waendelee kuishi mabondeni na yanapotokea mafuriko yakawaathiri hakuna anayemwajibisha wala kuwajibisha shirika la umeme linalopeleka huduma mahala pasipo na makazi, lakini wanasimama kidedea kutaka kumuwajibisha Waziri aliyewaambia wana Kigamboni kuwa kama hawawezi kulipa nauli "wapige mbizi".
Nchi imekuwa kama sehemu ya maigizo sasa. Na wakati mwingine naamini kuwa WATAWALA WETU WANAONGOZWA NA NGUVU ZA KAMERA kwa kufuata walipo waandishi hata kama kitokeacho hakiifai nchi,. Ni aibu kuwa na nchi kama hii, lakini si jambo la ajabu sana, kwani NI SISI WANANCHI WA KUAMKA NA KUWAWAJIBISHA HAWA WATAWALA WAJIITAO VIONGOZI. Tukiendelea kusubiri, hawatajiwajibisha. Hayati Baba wa Taifa aliwahi kusema kuwa "Inawezekana tatizo la paka kwa panya lingekwisha kama paka angefungiwa kengele shingoni: taabu ni kumpata panya wa kuifanya kazi hiyo. Na panya watakuwa wajinga sana wakidhani kuwa paka watajifunga au watafungana kengele shingoni!"
 Lakini hii ndio Tanzania yangu niiangaliayo kwa nyuzi 360. Na niyaonayo humo, ni kama hadithi ya kuku na yai.


Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA


Tuonane "Next Ijayo"

7 comments:

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

I wish kama kungekuwa na msikizaji....naona wote wapaswao kusikiza wako bize na ma-v8!

Albert Kissima said...

Tanzania inahitaji mapinduzi ya dhati kabisa. Kabla ya kuwa wao, walikuwa sisi, bila shaka, sisi ndio wa kuwafanya wao wawe tena kama sisi maana sisi wenyewe ndiyo tuliwafanya wakawa wao. Kwa Tanzania ya sasa, nguvu ya umma ndio njia pekee, wananchi sasa tuchoke kuvumilia.

Watu waundao chama tawala ni tatizo, hivyo hatuna budi kuangalia upande mwingine wa shilingi. Tamani sana watanzania wote tungetambua kuwa mbali na kuimarisha zaidi nguvu ya uma, lakini kubadilisha chama kilichotawala miongo mingi nalo bila shaka ni suluhisho. Labda tutaweza kupata viongozi na si watawala wa misingi ya kikoloni tulionao, tutaweza kupata viongozi wawajibikaji, watakaojiwajibisha na kukubali kuwajibishwa.

Mzee wa Changamoto said...

Ndugu zangu Chacha na Albert mmenena vema.
Na hasa ninukuu kauli yako Albert kuwa "Kabla ya kuwa wao, walikuwa sisi, bila shaka, sisi ndio wa kuwafanya wao wawe tena kama sisi maana sisi wenyewe ndiyo tuliwafanya wakawa wao."

Tutafika tuuuuu

Baraka kwenu wapendwa

Tmark said...

Yaani huyu jamaa kila nikimtathimini sipati thamani yake.
Ananipa wakati mgumu sana kumuelezea sifahamu yeye ni mtalii au kiongozi.
hivi inawezekana vipi nyumbani kwako kuna matatizo wewe unakazi ya kuzunguka tu katika nchi za wenzako,akirudi anaweza akakaa wiki tu utasikia anasafiri tena wa ajabu sana,yaani watu tuliowakabidhi madaraka ya kutuwakilisha wanalumbana yy hajali,yeye anakwenda msibani wakati kwake pia kuna msiba.

MKUMBWA said...

Binafsi sielewi kama raisi wetu anaelewa kama hali ziko taabani yaani wao wamekuwa wao na kutusahau sisi bila kujua kuna siku wanaweza kuwa sisi japo siamini kama inawezekana manake wanayachota mabilioni ambayo kuyamiliki sisi hatuwezi kamwe. Kuna uhalali wa raisi kikwete kutoa rambirambi y 10Milioni kweny msiba w kanumba wakati kuna watu kibao wanahitaji hata laki 1 tuuu ya matibabu wanakosa!!

Ebou's said...
This comment has been removed by the author.
Ebou's said...

Anayaelewa basi tu ila kumbukeni hizo ni mbio za sakafuni, watu wanakuja na kasi za ajabu, 2015 sio mbali kabisa nika kufumba na kufumbua waelewe hilo!