Saturday, October 16, 2010

Bado naamini WATAWALA hawa wanahitaji somo la awali la uRaia

NI MAREJEO YA JULAI MOSI.
Kama nakumbuka vema, basi URAIA NI ELIMU IHUSUYO HAKI NA WAJIBU WA RAIA KWA NCHI YAKE. Na kwenye haki na wajibu pia huwa laja suala la uongozi. Na kwenye UONGOZI kuna wajibu pia kwa wale uwaongozao.
Lakini mbali na uraia ufunzwao darasani, sote twatambua kuwa ili kuweza kuwa na suluhisho kwa tatizo, ni vema ukawa unalitambua fika tatizo hilo. Na katika mambo ya uongozi wa nchi ambayo yanahitaji mipango na ushauri wa watu zaidi ya "aliye juu" ina maana kunahitajika MUDA WA KUTOSHA KUWEZA KUJADILI NA KUWEKA KIPAUMBELE KWENYE MATATIZO MBALIMBALI.
Hivi majuzi (nikiwa huko nilikojichimbia nikikariri hili na lile) nikaona HARAKATI ZA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2010 zikishika kasi kwa wagombea wa vyama vya CUF na kisha CCM kuchukua fomu za kugombea nafasi ya Urais. Achilia mbali utitiri unaotangaza kugombea ubunge, udiwani nk. Na tena hawa wanachukua fomu kwa ajili ya kura za maoni / uchaguzi wa chama kumpata mgombea.
Rais Jakaya Kikwete akikabidhiwa fomu ya kugombea Urais na Katibu Mkuu wa CCM Yusuph Makamba makao makuu ya chama Dodoma.
Picha:
Dina Marios' Blog
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahimu Lipumba akichukua fomu za kugombea nafasiya Urais kutoka kwa Katibu wa Chama hicho Wilaya ya Kinondoni, Mh. Kassim Chogamawano
Picha:
Michuzi Blog Mwanachama wa chama cha siasa cha TLP Bwn Macmillan Lyimo (kushoto) akirejesha fomu ya kuomba kugombea uraisi kwa tiketi ya chama hicho kwa katibu mkuu wa chama hicho Meja Jesse Makundi huku katibu msaidizi wa TLP Bwn Hamad Tao akishuhudia.
Picha: Robert Oganda / DAILY NEWS
Ninalowaza ni kuwa kati ya siku hii mpaka Oktoba 31, watakuwa wameweza kutembelea majimbo ama sehemu ngapi kuweza kujionea kwa macho yao matatizo yaliyoko huko kisha kupanga mikakati ya kuyatatua kama watapewa ridhaa ya kuingia madarakani?
Labda kuna anayeweza kusema kuwa "kuna watendaji huko vijijini" lakini nani asiyejua UONGO WA KUTUPWA waufanyao watendaji hawa kumfurahisha "mgeni rasmi"? Haya tumeyasoma kwingi mpaka baadhi ya wananchi kufikia hatua ya kuwazomea viongozi na wengine kuchoka na ahadi zisizotekelezeka na kuanza kuwapiga mawe. Unakumbika yaliyotokea kwa Mheshimiwa Rais kule Mbeya? Kuna mengine yaliyotokea kabla ya hayo japo hakuna aliyenena kitu. Jikumbushe aliyoandika Dadangu Happy Katabazi kwenye makala yake HAPA. Na kama hiyo haitoshi, Rais Kikwete akaenda Morogoro mwaka huohuo akapewa takwimu za miaka 12 iliyopita REJEA HAPA. Unadhani kuna mtendaji atampeleka Rais ama Mwenyekiti wa chama chake kwenye "zahanati" kama hii? Ili aulizwe maswali ama? Sina hakika kama wagombea wanajua kuwa maisha ya hivi yapo duniani (achilia mbali ndani ya nchi yetu)
Picha: Beda Msimbe

Sasa nirejee kwenye suala la hawa WATAWALA wanaojiita viongozi.
Ni lini wagombea hawa watapata muda wa kuzungukia nchi, kuangalia na kukusanya mahitaji na matatizo yawakabilio wananchi, wayajadili, wayatengenezee mipango ya kuyatatua ama kuyatimiza (Ilani za uchaguzi) kisha warejee kwenye sehemu hizo na kuwaeleza wananchi namna watakavyowatatulia matatizo yao?
Kwani wenzetu hawa hawajui kuwa wajibu wao kama viongozi ni KUSAIDIANA NA WANANCHI KUTIMIZA YALE YAHITAJIWAYO NA WANANCHI WANAOWAONGOZA?
Ni kweli kuwa wagombea hawa wanalijua hili? Ama wako kwenye kukariri elimu ya uraia iliyo kubwa na kupuuza hii ya awali?
Na kwa kuwa kutakuwa na kambi mbili za chama tawala na vyama vya upinzani, bado wote wana majukumu na LAWAMA za kubeba. Niliwahi kuandika juu ya MASWALI YANGU 10 KWA RAIS JAKAYA KIKWETE (hapa) na kisha nikawa bayana juu ya yale YATAKAYOWAANGUSHA WAPINZANI KWENYE UCHAGUZI MKUU (hapa) na bado naamini hivyo.
Kuona wananchi wanateseka watesekavyo inasikitisha.
Kuona wapigao kampeni wanawafanya wananchi waamini kuwa WAO NDIO SULUHISHO NA SIO SEHEMU YA SULUHISHO INATIA KINYAA.
Na yote haya yanatokea kwa kuwa kila mpiga kampeni anasahau TAFSIRI YA URAIA ambayo ingemfanya yeye azungumzaye na wale wazungumziwao wajue kuwa wana WAJIBU NA HAKI ya kuhakikisha kuwa wanapata mahitaji yao kwa kushirikiana.
Hili lanifanya niamini kuwa WATAWALA HAWA WAGOMBEAO NAFASI ZA URAIS, WANAHITAJI SOMO LA AWALI LA URAIA.
Kwa wenzetu wangeweza sema "Civics 101 ama Introduction to Civics" ama...
Nawaza kwa sauti tuuu

Uchaguzi Tanzania ni "label" inayozungumzia namna niionavyo nchi yangu ya Tanzania ijiandaavyo na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010. Kwa maandishi mengine juu ya mada hii katika "label" hii BOFYA HAPA

No comments: