Monday, August 25, 2008

Olimpiki imeisha. Tumejifunza kitu?

Michuano ya Olimpiki ndio imemalizika na pamoja na kupambwa na kupambika kwa sherehe za kufungua na kuhitimisha michuano hiyo, bado kuna maswali ambayo wapenda michezo wengi wanaendelea kujiuliza. Wapo wajiulizao kama kuna nchi yoyote ambayo itajaribu kufanya "sherehe za kufuru" kama walivyofanya waChina na kuna ambao wanaendelea mbele zaidi kuangalia jinsi watu walivyoweza kuvunhja rekodi mbalimbali na kujiweka pamoja na kuziweka nchi zao kwenye ramani ya michezo. Na hapo ndipo nami ninapogota, nikiangalia mafanikio ya nchi mbalimbali katika michezo mbalimbali nikarejesha mawazo hayohayo kwa nchi niipendayo na kuithamini TANZANIA, najikuta nakwazwa na maswali kadhaa. Pengine michezo kama kuogelea itatugharimu saana maana waogeleaji wa kimataifa waliofanya vema wanawekeza gharama kubwa saana kwenye mchezo huo kuanzia chakula mpaka mazoezi. Lakini pia kuna sehemu nyingine ambazo naamini tungestahili kufanya vema kiasi.
Hivi ni kweli kwamba Tanzania hatuna wakimbiaji wazuri? Na iweje kwa jamii kama ya Kenya ambayo tumepakana nayo na tunashabihiana kwa mambo mengi (hasa ukanda wa kaskazini upakanao nao) wanaweza kufanya vizuri katika michezo kama mbio ndefu nasi tushindwe?
Hivi ni kweli kuwa hatuna wapiganaji wenye vipaji vya kuweza kufanya vema kwenye michuano kama hii?
Vipi kuhusu walenga shabaha?
Sina takwimu lakini nakumbuka kuwa walikuwepo wenye vipaji katika nyanja nyingi za michezo (hasa mikoani nilikosomea) tena wengine wakifanya vema saaana hata katika michezo ya mashule kama Umisseta lakini wanapomaliza shule hakuna utaratibu mpango mahususi wa kuwaonesha njia kuelekea kwenye mafanikio na ndio maana wanaishia kuacha kushiriki michezo na kujiingiza kwenye kazi za kusukuma siku kama uvuvi, ukulima na muda mfupi baadae kwenye ujenzi wa familia.
Kwangu mimi nadhani kuna pengo kubwa kati ya serikali, jamii na michezo. Kwa SERIKALI utoweka thamani halisi ya michezo na hata kutoitengenezea njia sahihi ya kuwawezesha wale wenye vipaji halisi waweze kujikita huko na kujiajiri kwa manufaa yao, familia zao na taifa kwa ujumla. Pia JAMII lazima itambue kuwa namna nyingine ya kujiajiri katika michezo ni kupitia elimu. Tumesikia baadhi ya washindi (kama Kirsty Coventry wa Zimbabwe) wakisema namna walivyoamua kujiunga na vyuo vitoavyo scolarship nje ya nchi zao ili kupata vifaa, wakufunzi na mazingirz bora ya kufanya vema katika michezo waipendayo. Tunao kina Hashim Thabit ambao mchezo ni sehemu kuwa ya mwendelezo wake kielimu, lakini twahitaji wengi wenye kujijua vipaji vyao kusaka mazingira mema nje ya nchi ili waweze kujianda na kuwa katika viwango vya kimataifa kisha warejee nyumbani kunyanyua mazingira ya mazoezi kwa waliokosa nafasi ya kuelekea waliko.
Na MICHEZO ama taasisi za michezo ziache kuendeshwa kama mali za kina fulani. Ubadhirifu kwenye vyama na mashirikisho kimekuwa chanzo kikubwa cha kushindwa kupata washiriki wanaostahili na pia kuigeuza Dar Es Salaam kama ndio Tanzania kunanyima walio na vipaji halisi nje ya Dar kutuwakilisha na matokeo yake tunaishia kuwa washiriki na si washindani achilia mbali washindi.
Ni CHANGAMOTO YETU sote kufikiri namna ya kutatua yaliyotukwamisha mwaka huu, ili tujwe tunakotaka kuwa katika Olimpiki zijazo huko London.

1 comment:

Israel Saria said...

Safi sana, ni kama ulijua nini kitafuata kwa watanzania sisi!...