Tuesday, October 21, 2008

"Alichopokea Mwl Nyerere toka kwa wakoloni haikuwa "nchi"" Balozi Ombeni Sefue


WaTanzania wameaswa kuendeleza umoja na mshikamano aliouanzisha Hayati Baba wa Taifa mwl J.K Nyerere kama njia mojawapo ya kumuenzi.
Rai hiyo ilitolewa na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Ombeni Sefue wakati wa maadhimisho ya Kazi na Maisha ya Mwalimu Julius K Nyerere yaliyofanyika jioni ya Jumamosi ya tarehe 18 huko Washington DC.
Katika hotuba yake aliyoitoa kama mgeni rasmi, Balozi Sefue alisema wakati Mwalimu Nyerere anapokea nchi kwa wakoloni, ilikuwa ni milki yenye watu wenye makabila mbalimbali na ambao hawakuwa na namna moja ya kuwaunganisha na kuwafanya kuwa taifa, hivyo moja kati ya kazi zake za mwanzo ilikuwa kuiweka jamii pamoja, kuwa na namna moja ya mawasiliano na kisha kuvunja mipaka ya kikabila miongoni mwa wanajamii.
Amesema pia Mwalimu alianza kuwekeza katika elimu kwani wakati akikabidhiwa nchi alikuwa na wasomi wachache saana kiasi cha kumpa wakati mgumu katika hatua za mwanzo za kiutawala.
Balozi Sefue amesema mtazamo wa mwalimu kwamba "kuongea na wananchi kwa kutumia mkalimani hakunitofautishi na wakoloni, zaidi ya rangi" kulimpa changamoto ya kusambaza Kiswahili kama njia kuu ya mawasiliano na kujenga umoja na mshikamano ambao tunajivunia mpaka leo.
Siku hiyo ambayo iliandaliwa na The Nyerere Health & Education Fund ilihusisha Historia ya mwalimu, Harakati zake, mahusiano binafsi yaliyoelezwa na wajukuu wake, maelezo toka wawakilishi wa The Diaspora African Forum, Venezuela Solidarity Network na wageni wengine.

No comments: